Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Rais Dkt. Shein Akemea Wasanii Kuibiwa Kazi Zao

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa ni jambo baya sana na halikubaliki katika jamii kwa wasanii kuibiwa kazi zao na wajanja wachache ambao hujinufaisha wao.

Dk. Shein aliyasema hayo katika ukumbi wa Ikulu ndogo Kibweni mjini Zanzibar alipokutana na uongozi wa Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo wakati ilipowasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mpango Kazi wa Wizara hiyo kwa kipindi cha Julai 2018 hadi Machi 2019.

Rais Dk. Shein alisema kuwa ni vyema sheria ikatazamwa na kama kuna haja ya kuangaliwa kwa kufanywa marekebisho basi ni vyema jambo hilo likafanyika kazi ipasavyo ili kuondosha kabisa dhulma hiyo wanayofanyiwa wasanii wakiwemow asanii wakongwe.

Alisema kuwa imekuwa ni utamaduni hivi sasa kwa baadhi ya watu kuzitumia kazi za wasanii kwa kujinufaisha wao huku wakiwaacha wasanii husika kutopata kipato ama faida zozote za kazi zao na badala yake wajanja hao wakajinufaisha wao.

Hivyo, Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya kuwekwa mikakati maalum katika kutafuta taratibu na ufumbuzi wa suala hilo kisheria na kusisitiza haja ya kutizamwa sheria iliopo hivi sasa kama inakidhi haja juu ya suala hilo ama inahitaji marekebisho.

Aidha, Rais Dk. Shein alieleza haja kwa uongozi wa Wizara hiyo kwa kupitia Idara yake ya Utamaduni na Sanaa ikalifanyia kazi suala zima la kivazi cha Mzanzibari mwanamke na mwanamme na jinsi kinavyovaliwa.

Rais Dk. Shein pia, alisisitiza haja kwa Wizara kutizama jinsi ya matumizi na kazi za  studio mpya ya kisasa iliyojengwa na Serikali kwa fedha nyingi hapo Rahaleo ambapo iwapo ingelitumika vyema ingekuwa mkombozi mkubwa kwa wasanii wa Zanzibar.

Alieleza kuwa wasanii wa Zanzibar wana uwezo mkubwa wa kutengeneza filamu mbalimbali kwa kutumia studio hiyo mpya zikiwemo za maigizo na maonesho na kuipa sifa kubwa Zanzibar kama ilivyo kwa nchi nyengine  duniani.

Rais Dk. Shein pia, alieleza haja kwa Wizara hiyo kubuni shughuli mbali mbali za kuwaendeleza vijana kwa kuwapatia miradi mbali mbali sambamba na kutoa taaluma kwa kuwafanya wawe wazalendo ili waweze kuilinda nchi yao.

Alisisitiza haja kwa Wizara kuwadhibiti vyema vijana kwa kuwasaidia kwa nyenzo mbali mbali za kujiimarisha miradi ya kielimu baada ya kujiunga katika vikundi.

Nae Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee aliipongeza Wizara hiyo kwa kuwasilisha vyema Mpango Kazi wake na kutoa nasaha zake kwa Wizara katika kuwasimamia vijana ambao ndio kundi kubwa katika jamii.

Dk. Mzee alieleza kuwa Rais ameiunda Wizara hiyo kutokana na kushabihiana sekta zake ikiwemo Sanaa, utamaduni na michezo ambazo nazo iwapo zitafanyiwa kazi vizuri zinaweza kuzalisha ajira.

Mapema Naibu Waziri wa Wizara ya hiyo Lulu Msham Abdalla alieleza kuwa Wizara kwa kushirikiana na Wizara nyengine imekamilisha zoezi la utambuzi wa mahitaji ya vijana kwenye maeneo ya kilimo, ufugaji, mafunzo ya kazi na ushonaji ambapo jumla ya vijana 4029 watanufaika.

Alieleza kuwa Wizara imefanikiwa kuhakikisha kuwa utamaduni, mila, silka za Wazanzibari zinaenziwa, zinaendelezwa kwa manufaa ya Taifa kwa kumia matamasha mbali mbali, vikundi vya Sanaa ikiwemo Kikundi cha Taifa cha Taarab na kikundi cha ngoma asilia.

Aidha, alieleza kuwa Wuzara hiyo imefanikiwa kulinda haki za wasanii na Sanaa zao  kupitia BASSFU na Ofisi ya Hakimiliki ambapo pia jumla ya matamasha manane yamefanyika, kazi za Sanaa 379 zimekaguliwa, jumla ya watumiaji 305 wa kazi za Hakimiliki kibiashara wamekaguliwa na mirahaba yenye thamani ya TZS 105,128,266 itagaiwa kwa wasanii na wabunifu 1,277.

Pia, Naibu Waziri huyo alieleza kuwa Wizara imefanikiwa kukamilisha Kongamano la Pili la Kitaifa la Kiswahili na maonyesho ya vitabu vya lugha na elimu, lililoshirikishs wataalamu 237 kutoka nchi mbali mbali zikiwemo Marekani, Pakistani,Misri, Rwanda, Sweeden, Japan, Kenya, Uganda, Austria, Tanzania Bara na Zanzibar.

Pamoja na hayo, alisema kuwa Wizara imefanikiwa kukamilisha Sera ya Michezo na imeanza kutumika huku akieleza jinsi Wizara ilivyofanikiwa kukamilisha matengenezo makubwa ya kiwanja cha Mao-Zedong na matengenezo madogo kwa kiwanja cha Gombani na Amaan Stadium.

Sambamba na hayo alieleza kuwa kwa upande wa mradi wa ujenzi wa viwanja vya Wilaya eneo la Mkokotoni Wilaya ya Kaskazini “A” limeshapatikana na hatua ya kukamilisha michoro zinaendelea pamoja na kupatikana kwa eneo la Kama JKU Wilaya ya Magharibi “A”, limeshapatikana na taratibu za awali zinaendelea.

Pia, alieleza kuwa viwanja vya Wilaya ya Kusini (Kangani) na Kaskazini (Kishindeni) Pemba vimo katika hatua za kukamilika.

Akisoma Utekelezaji wa Mpango Kazi Katibu Mkuu wa wizara hiyo Omar Hassan (King) alieleza mikakati iliyowekwa na Serikali katika kuiendeleza Wizara hiyo.

Wakati huo huo, Rais Dk. Shein alikutana na uongozi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais na kutoa pongezi kwa mashirikiano na juhudi kubwa zinazochukuliwa na uongozi wa Ofisi hiyo kwa kumsaidia Makamo wa Pili wa Rais katika shughuli zake za kazi.

Dk. Shein alieleza kuridhika kwake na uwasilishaji na utayarishaji wa Mpango Kazi wa Ofisi hiyo ambao umewasilishwa vizuri huku akiusisitiza uongozi wa Ofisi hiyo kuendelea kushauriana kwani ndio msingi wa kazi.

Nae Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd alieleza mashirikiano na umoja wa viongozi pamoja na wafanyakazi wa Ofisi hiyo ambayo yamekuwa chachu ya mafanikio yaliopatiana huku akimpongeza Dk. Shein kwa kuendelea kumuongoza vyema.

Mapema akitoa muhtasi wa taarifa ya Utekelezaaji wa Mpango Kazi wa mwaka 2018/2019 kwa kipindi cha robo tatu kuanzia Julai 2018 hadi Machi 2019 Waziri wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Mohamed Aboud Mohamed alitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa uongozi wake wenye ufanisi mkubwa.

Waziri Aboud alisema kuwa Zanzibar imepata mafanikio makubwa ambayo yameimarisha ustawi bora wa maisha ya wananchi, misingi ya usawa, demokrasia na utawala bora inayopelekea kuimarika kwa uwajibikaji wa viongozi na watendaji wa Serikali.

Alieleza kuwa Ofisi imeendelea kupambana na uharibifu na uchafuzi wa mazingira kwa kutoa elimu kwa jamii juu ya uhifadhi wa mazingira ikiwa ni pamoja na upigaji marufuku mifuko ya plastiki pamoja na kufanya operesheni ya kusimamia maliasili zisizorejesheka.

Pia, aleleza jinsi Ofisi hiyo ilivyoendelea kufuatilia na kuipatia ufumbuzi migogoro inayojitokeza katika maeneo mbali mbali hapa nchini pamoja na kutoa elimu kwa jamii juu ya masuala ya kukabiliana na maafa.

Aidha, alieleza kuwa Ofisi imechukua jitihada za kulihami eneo la fukwe la Msuka ili lisiendelee kumungonyoka kutokana na maji ya bahari kwa kuandaa utaratibu wa kujenga ukuta maalim utakaogharamiwa na serikali.

 

161 thoughts on “Rais Dkt. Shein Akemea Wasanii Kuibiwa Kazi Zao

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama