Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Rais Dkt. Magufuli Ametoa Wito kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Musimamia Vizuri Rasilimali

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia katika Mkutano huo Maalum wa Wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) unaofanyika Kampala nchini Uganda.

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza jambo na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta wakati wakielekea kwenye ukumbi wa Mkutano Maalum wa Wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC unaojadili masuala mbalimbali ikiwemo Maendeleo ya Sekta ya Miundombinu na Afya.

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa amekaa pamoja na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Rais wa Uganda Yoweri Museveni wanne kutoka kulia, Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta pamoja na Rais wa Sudani ya Kusini Salva Kiir wakati wa mkutano huo Maalumu wa Wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki unao endelea jijini Kampala.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametoa wito kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kusimamia vizuri rasilimali walizonazo na kukusanya kodi vizuriili waweze kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi wa miundombinu na kuimarisha huduma za afya kwa wananchi.

Mhe. Rais Magufuli ametoa wito huo leo tarehe 22 Februari, 2018 mjini Kampala nchini Uganda wakati akichangia katika mkutano wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unaojadili maendeleo na upatikanaji wa fedha kwa ajili ya miradi ya sekta ya miundombinu na afya.

 

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Rais wa Uganda Yoweri Museveni akifungua Mkutano huo maalum wa Wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki Kampala nchini Uganda.

 

Kabla ya Mhe. Rais Magufuli kutoa mchango wake, Marais walioshiriki mkutano huo wamepokea taarifa ya mkutano wa majadiliano ya kisekta (Round Table) kuhusu mahitaji ya fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya sekta ya miundombinu na afya ambapo imeelezwa kuwa katika miaka 10 ijayo nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zitahitaji Dola za Marekani Bilioni 78 kutekeleza miradi ya miundombinu inayopendekezwa.

Taarifa hiyo imechangiwa na wadau mbalimbali wakiwemo Marais, wawakilishi wa sekta binafsi na washirika wa maendeleo ambao wameelezea njia mbalimbali za kupata fedha za kutekeleza miradi hiyo ikiwemo kutumia mfumo wa ushirikiano kati ya Serikali na Sekta binafsi (PPP).

Katika mchango wake Mhe. Rais Magufuli amesema pamoja na kutumia mfumo wa PPP ni muhimu kwa Serikali za kila nchi kusimamia vizuri ukusanyaji wa mapato ya kodi na rasilimali nyingine ili kutekeleza miradi ya miundombinu, afya na sekta nyingine.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Rais wa Uganda Yoweri Museveni katika picha na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli wa kwanza kulia, Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, pamoja na Rais wa Sudan ya Kusini Salva Kiir mara baada ya Mkutano Maalum wa 19 wa Jumuiya hiyo uliofanyika Kampala nchini Uganda.

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akifurahia jambo na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta mara baada ya kupiga picha ya pamoja katika eneo la Munyonyo Kampala nchini Uganda

 

Ametahadharisha kuwa japo kuwa mfumo wa PPP ni mzuri, ni vyema wataalamu wakachukua tahadhali za kutosha ili kuepusha Serikali kuingia katika mikataba isiyokuwa na maslahi kwa nchi zao kutokana na baadhi ya wadau wa sekta binafsi kutaka kutengeneza faida kubwa kwa kupandisha gharama za miradi.

Mhe. Rais Magufuli ametolea mfano wa miradi mikubwa iliyoanza kutekelezwa nchini Tanzania ukiwemo ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) na ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stieglers’ Gorge), kuwa Serikali ya Tanzania imeamua kuanza kutekeleza miradi hiyo kwa kutumia fedha zake baada ya kufanikiwa kusimamia vizuri rasilimali zake na kubana matumizi.

“Mimi naamini tukiamua tunaweza, nchi zetu zina rasilimali nyingi za kuweza kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, mathalani tafiti zinaonesha kuwa kama nchi zetu zitaweza kukusanya vizuri mapato ya kodi, zinaweza kutekeleza nusu ya miradi yake ya maendeleo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Rais wa Sudan ya Kusini Salva Kiir kabla ya kuanza kwa mkutano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Lakini ukiachilia mbali mapato ya kodi, tunapoteza fedha nyingi kupitia utoroshaji wa rasilimali zetu, ripoti ya jopo la Umoja wa Afrika lililoongozwa na Rais Mstaafu wa Afrika Kusini Mhe. Thabo Mbeki imeeleza kuwa nchi za Afrika zinapoteza Dola za Marekani Bilioni 150 kila mwaka kutokana na utoroshaji wa rasilimali” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Marais waliohudhuria mkutano huo ni Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Kenya Mhe. Uhuru Muigai Kenyatta, Rais wa Sudan Kusini Mhe. Salva Kiir Mayardit na Marais wa Rwanda na Burundi wamewakilishwa.

Kesho tarehe 23 Februari, 2018 Mhe. Rais Magufuli atahudhuria mkutano wa 19 wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Kampala

22 Februari, 2018

43 thoughts on “Rais Dkt. Magufuli Ametoa Wito kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Musimamia Vizuri Rasilimali

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama