Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Rais Dkt. Magufuli Afanya Mazungumzo na Prince William

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Mjukuu wa Malkia wa Uingereza Prince William mara baada ya kuwasili Ikulu jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mazungumzo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 27 Septemba, 2018 amekutana na kufanya mazungumzo na Mjukuu wa Malkia Elizabeth II wa Uingereza, Prince William (Duke of Cambridge) Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo hayo Prince William ameelezea kufurahishwa na uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Uingereza, na amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kupata nafasi ya kuzungumza nae.

Prince William amezungumzia juhudi anazozifanya katika uhifadhi wa wanyamapori na amemuomba Mhe. Rais Magufuli kuendelea kushirikiana katika kukabiliana na vitendo vya ujangili hasa wa Tembo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimkabidhi Mjukuu wa Malkia wa Uingereza Prince William picha ya wanyama wanaopatikana katika mbuga mbalimbali nchini mara baada ya kuwasili Ikulu jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli amemkaribisha Prince William kuja hapa Tanzania wakati wowote, na amemhakikishia kuwa Tanzania itaendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano wake na Uingereza ikiwemo kushirikiana nae kuhifadhi wanyamapori.

“Naomba ufikishe salamu zangu kwa Malkia Elizabeth II, mwambie Watanzania tunaipenda Uingereza na tutaendeleza na kuuimarisha zaidi ushirikiano wetu mzuri kwa manufaa yetu sote” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimkabidhi Mjukuu wa Malkia wa Uingereza Prince William Kamusi ya Kiswahili mara baada ya kuwasili Ikulu jijini Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipokea zawadi ya Picha kutoka kwa Mjukuu wa Malkia wa Uingereza Prince William Ikulu jijini Dar es Salaam. Picha hiyo inamuonesha Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akiwa anazungumza na Malkia wa Uingereza Elizabeth II

Mhe. Rais Magufuli ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imefanya juhudi kubwa za kukabiliana na ujangili hasa wa Tembo ambapo kwa sasa umepungua kwa kiasi kikubwa na kwamba anatarajia Prince William ataunga mkono ili kukomesha kabisa ujangili katika hifadhi zote za wanyamapori hapa nchini.

Prince William aliyeingia hapa nchini jana atakuwepo kwa siku 4 hadi tarehe 29 Septemba, 2018.

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika mazungumzo na mgeni wake Mjukuu wa Malkia wa Uingereza Prince William aliyeambatana na Balozi wa Uingereza hapa nchini Sarah Cooke pamoja na ujumbe wake mara baada ya kuwasili Ikulu jijini Dar es Salaam. Wengine katika picha ni Waziri wa Maliasili na Utalii Hamisi Kigwangalla akiwa pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Mjukuu wa Malkia wa Uingereza Prince William mara baada ya kumaliza mazungumzo yao Ikulu jijini Dar es Salaam.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

27 Septemba, 2018

135 thoughts on “Rais Dkt. Magufuli Afanya Mazungumzo na Prince William

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama