Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Profesa Safari Amfananisha Rais Magufuli na Lumumba, Nkurumah

Na Mwandishi Wetu.

Siku moja baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kuagiza kupitiwa upya kwa sheria za madini, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Profesa Abdallh Safari, amemfananisha Rais huyu na aliyewahi kuwa Rais wa kwanza wa Ghana, Kwame Nkurumah na Waziri Mkuu wa kwanza wa Kongo, Patrice Lumumba kutokana na juhudi binafsi anazofanya kutetea rasilimali za nchi

Profesa Safari ameaongea hayo ofisini kwake leo alipofanya mahojiano maalumu na Idara ya Habari-Maelezo kutoa maoni yake juu ya agizo la Rais kutaka iundwe timu ya wataalam kupitia upya sheria za madini nchini na kupelekwa bungeni ili zifanyiwe marekebisho.

“Ninampongeza  Rais kwa kazi kubwa anayoifanya kutetea rasilimali za nchi. Anafanya kazi kama walivyokuwa wanafanya baadhi ya viongozi wazalendo barani Afrika ya kupigania haki za wananchi wao kufaidika na rasilimali za nchi,” alieleza Prof. Safari huku akitoa mfano wa hayati Patrice Lumumba, Kwame Nkurumah na Mwalimu Julius Nyerere kama viongozi waliojitolea kwa ajili ya wananchi wao.

Alieleza kuwa maamuzi anayoyafanya Rais yanasimama katika kifungu cha tisa (kifungu kidogo C) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na marekebisho ya mwaka 2000, ambacho kinasisitiza kwamba utajiri wa Taifa uendelezwe, uhifadhiwa na kutumiwa kwa manufaa ya wananchi wote kwa ujumla na pia kuzuia mtu kumyonya mtu mwingine.

Profesa Safari ambaye pia ni Wakili wa Kujitegemea, amewaomba Watanzania na Wataalamu wa sheria za mikataba kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais katika kutetea maslahi ya Taifa.

“Nchi hii ina Wanasheria wengi wazuri katika masuala ya madini na mikataba. Ninashauri watafutwe wataalam hawa ambao watakuwa sio wala rushwa ili wamsaidie Rais katika vita hii ya rasilimali”, aliongeza Profesa Safari.

Akiongea kwa niaba ya Wazee waliofika Ikulu kusikiliza ripoti ya Kamati ya pili ya kuchunguza mchanga wenye madini, Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku alielezea ujasiri unaofanywa na Rais Dkt. Magufuli kuwa ni mfano wa kuigwa na kuomba wazee na wananchi kwa ujumla kuunga mkono juhudi za Rais katika kutetea rasilimali.

“Nchi hii ina wasomi wengi sana lakini tumepata msomi mmoja tu jasiri”, alieleza Butiku.

Jana Rais Maguli alipokea ripoti ya Kamati ya Pili ya Madini ya kuangalia masuala ya kisheria na kiuchumi ambapo ilionesha Serikali imekuwa ikipoteza mapato ya Shilingi Trilioni 108.46 kutokana na udanganyifu unaofanywa katika usafirishaji wa mchanga wa dhahabu ‘makinikia’ nje ya nchi katika kipindi cha kuanzia mwaka 1998 hadi mwezi Machi 2017.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama