Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Prof. Mbarawa Aridhishwa na Ujenzi wa Jengo la 3 la Abiria JNIA

Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania Prof. Ninatubu Lema, (aliyenyoosha mikono) akimweleza jambo Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa  (wa tatu kutoka kulia), leo wakati akianza ziara ya kutembelea jengo la tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA_TBIII).

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amekagua ujenzi wa jengo la Tatu la Abiria la uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), na kuelezea kuridhishwa kwake kwa hatua ya ujenzi iliyofikiwa.

Akizungumza mara baada ya kukagua ujenzi huo Waziri Profesa Mbarawa amemhakikishia mkandarasi BAM International anayejenga jengo hilo kuwa Serikali italipa madai yake kwa wakati kwa kadri atakavyoyawasilisha.

“Nia yetu ujenzi huu ukamilike ifikapo Septemba mwakani, hivyo tunamtaka mkandarasi kuongeza kasi ya ujenzi na wasimamizi kumsimamia kikamilifu ili vifaa vinavyofungwa katika jengo hilo viwe na ubora uliokusudiwa na vidumu kwa muda mrefu”, amesisitiza Profesa Mbarawa.

Prof. Mbarawa amesema kukamilika kwa jengo la tatu la abiria la uwanja wa ndege wa Julius Nyerere kutawezesha uwanja huo kuweza kuhudumia abiria wapatao milioni nane na  nusu kwa mwaka na hivyo kukuza uchumi wa nchi kwa kuwezesha watalii na wageni wengi zaidi kufika nchini.

Meneja wa Mradi wa Jengo la tatu la abiria la Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBIII), Bw. Ray Blumrick (kushoto) akitoa ufafanuzi wa kuhusu ujenzi wa jengo hilo, kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof Makame Mbarawa (wa tatu kutoka kushoto).

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Profesa Ninatubu Lema amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa ujenzi huo unasimamiwa kikamilifu na utamalizika kwa wakati.

“Kama wasimamizi tumejipanga kuhakikisha zoezi la ufungaji vifaa katika jengo hili, linakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa,” amesisitiza Prof. Lema.

Naye Meneja ujenzi wa BAM International, Bw. Rey Blumrick amesema kazi iko katika hatua nzuri na itakamilika kwa wakati.

Mradi wa ujenzi wa jengo la tatu la abiria ni sehemu ya uboreshaji wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere lengo likiwa ni kuwezesha ndege na abiria wengi kutumia uwanja huu na kuhuisha sekta ya usafiri wa anga hapa nchini.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Meneja Mradi wa jengo la tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBIII) Bw. Ray Blumrick  akimwelekeza namna paa lilivyo imara, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa  wakati wa ziara yake kwenye jengo hilo leo.

141 thoughts on “Prof. Mbarawa Aridhishwa na Ujenzi wa Jengo la 3 la Abiria JNIA

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama