Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Kamati ya Bunge Yasisitiza Mradi wa Maji Nzuguni Kukamilika kwa Wakati

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji imeisisitiza Wizara ya Maji na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) kumaliza kwa wakati au kabla ya wakati mradi wa maji unaotekelezwa katika Kata ya Nzuguni iliyoyopo jijini Dodoma.


Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Dkt. Christine Ishengoma ametoa rai hiyo jana jijini Dodoma wakati kamati hiyo ilipofanya ziara ya kutembelea mradi huo wa maji unaotarajiwa kuhudumia wananchi takriban 33,000 wa Mitaa ya Nzuguni, Ilazo na Kisasa.

Mhe. Dkt. Ishengoma amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuijali sekta ya maji na kujitahidi kutatua changamoto za maji hasa kwa wakati huu ambao miji mingi inakuwa na kusababisha ongezeko la watu.


“Leo tumetembelea eneo hili la Nzuguni ambalo wananchi wake walikuwa na changamoto kubwa ya maji, hatimaye tatizo hili linaenda kutatuliwa kupitia visima hivi vitano vilivyochimbwa vinavyotoa maji safi na salama yasiyo na chumvi. Nawaomba mmalize mradi huu ndani ya miezi sita mliyoahidi au kabla ya miezi hiyo ili wananchi wasiendelee kuteseka na kero hii”, alisema Mwenyekiti wa Kamati hiyo.

Tanzania Yatajwa Miongoni mwa Nchi Chache Barani Afrika Katika Kuwashirikisha Wananchi Kwenye Uhifadhi

Tanzania imetajwa kuwa ni miongoni mwa nchi chache barani Afrika ambazo zinatekeleza dhana ya ushirikishwaji wa Jamii katika uhifadhi wa kivitendo kwa kutoa fursa kwa wananchi kushiriki moja kwa moja katika kusimamia rasilimali za wanyamapori.

Hayo yamesemwa  na  Naibu Katibu wa Maliasili na Utalii, Juma Mkomi  wakati akifungua warsha ya kupitia na kuthibitisha mkakati wa usimamizi na uendeshaji wa maeneo ya Jumuiya za Hifadhi ya Wanyamapori (WMAs)  iliyofanyika leo Jijini Arusha.

Amesisitiza kuwa  WMAs ni kinga (buffer) muhimu kwa maeneo ya Hifadhi za Taifa, Mapori ya Akiba, Hifadhi ya Ngorongoro na Mapori Tengefu.

Mkomi amesema bila WMAs changamoto za kiuhifadhi zitaathiri moja kwa moja Hifadhi za Taifa, Mapori ya Akiba, Hifadhi ya Ngorongoro na Mapori Tengefu.

Kutokana na umuhimu huo, Mkomi ametoa wito kwa  Wadau wa Uhifadhi nchini kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali za kuendeleza WMAs ili kuziwezesha kujisimamia na kujiendesha.

Mitaa Isiyo na Umeme Handeni Kupata Huduma Hiyo Ifikapo Disemba 2022

Imeelezwa kuwa, Mitaa 28 ambayo bado haina umeme  katika Jimbo la Handeni mjini ipo katika mpango wa kupatiwa umeme kupitia mradi wa umeme vijijini Awamu ya Tatu mzunguko wa Pili unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Hayo yamesemwa  bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato wakati akijibu swali la Mbunge wa Handeni Mjini, Mheshimiwa Reuben Nhamanilo Kwagilwa ambaye aliuliza kuhusu mpango wa Serikali wa kupeleka umeme katika mitaa 28 ya Jimbo la Handeni Mjini ambayo bado haijapata umeme.

Dkt. Mpango Atoa Wito wa Kuondolewa kwa Upinzani Dhidi ya Ufadhili wa Kimataifa katika Utekelezaji wa Miradi ya Mageuzi katika Nchi za Afrika

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amehutubia Mkutano wa Baraza Kuu la 77 la Umoja wa Mataifa (UNGA) unaondelea Jijini New York nchini Marekani. Makamu wa Rais ametoa hotuba hiyo akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

Akitoa hotuba hiyo, Makamu wa Rais amesema Tanzania na nchi za Afrika kwa ujumla zinahitaji mabadiliko ya haki na ya utaratibu katika kufikia matumizi ya nishati mbadala kwa kuzingatia hali za maisha ya watu wa bara hilo wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali za upatikanaji wa nishati hizo. Ametoa wito wa kuondolewa kwa upinzani dhidi ya ufadhili wa kimataifa katika utekelezaji wa miradi ya mageuzi katika nchi za Afrika ambayo inalenga kutumia rasilimali ikiwemo gesi kwa ajili ya nishati na matumizi mengine katika kufikia maendeleo.

Makamu wa Rais ameongeza kwamba biashara ya hewa ukaa barani Afrika inapaswa kufanyika kwa uwazi na kuwanufaisha wananchi waliotunza mazingira na misitu inayozalisha hewa hiyo kwa matumizi ya dunia huku akiitaja Tanzania kama nchi iliowekeza zaidi katika uhifadhi wa misitu ambapo asilimia 30 ya eneo la ardhi ya taifa hilo imehifadhiwa.

Katika kudumisha amani na usalama, Makamu wa Rais amesema Tanzania siku zote inaamini kuwa diplomasia na meza za mazungumzo ndiyo chombo bora cha kutatua migogoro duniani. Amesema licha ya migogoro iliyopo duniani mataifa yanapaswa kulinda maisha ya binadamu hasa watoto na wanawake pamoja na ustawi wa watu. Aidha, ameongeza kwamba ni muhimu kushiriki katika kutafuta utatuzi wa migogoro kwa amani ili kukabiliana na athari zitokanazo na migogoro hiyo kama vile ongezeko kubwa la bei za chakula na mafuta pamoja na kushuka kwa uzalishaji wa kilimo na viwanda duniani kote.

Bunge Lapitisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali za Fedha wa Mwaka 2022

Na Farida Ramadhani na Saidina Msangi – WFM – Dodoma

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali za Fedha wa mwaka 2022 (The Written Laws (Financial Provisions) Amendment Act, 2022), ambao unalenga kufanya marekebisho ya Sheria 6 za kodi, mirahaba na uwekezaji.

Akiwasilisha Muswada huo bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba alisema lengo la Muswada huu ni kufanya marekebisho kwenye Sheria zinazosimamia kodi na mrabaha kwa kubadili viwango vya kodi na mrabaha.

Aliongeza kuwa, Muswada huo unalenga kuweka taratibu za utoaji vivutio kwa wawekezaji ili kuhamasisha uzalishaji kwa viwanda vya ndani ya nchi vinavyozalisha mbolea na magunia ya mkonge pamoja na kuondoa changamoto zilizopo katika utekelezaji wa Sheria ya uwekezaji Tanzania, Sura 38.

Mhe. Nchemba alizitaja Sheria zinazopendekezwa kufanyiwa marekebisho kupitia Muswada huo kuwa ni Sheria ya Ushuru wa Bidhaa Sura 147, Sheria ya Kodi ya Mapato Sura 332, Sheria ya Madini Sura 123, Sheria ya Ushuru wa Barabara na Mafuta Sura 220 na Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani Sura 148.

“Sehemu ya pili ya Muswada yenye ibara za 3 hadi 5 inapendekeza kurekebisha Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, Sura ya 147, ambapo kifungu cha 128 kinapendekezwa kurekebishwa ili kumpa mamlaka Waziri mwenye dhamana na masuala ya fedha, baada ya kupata idhini ya Baraza la Mawaziri kusamehe ushuru kwenye bidhaa zitakazotumika katika utekelezaji wa miradi ya uwekezaji mahiri na mahiri maalumu itakayoidhinishwa na Kamati ya Taifa ya Uwekezaji (NISC)”, alifafanua Dkt. Nchemba.

Matukio katika Picha: Waziri Mkuu Akiwa Bungeni Leo

Rais Dkt. Mwinyi Akutana na Mabalozi Walioteuliwa Hivi Karibuni

Makamu wa Rais Atoa Wito kwa Mataifa Kuchangia Mfuko wa Global Fund

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa mataifa ulimwenguni kuungana katika kutoa mchango kwa Mfuko wa Kimataifa wa Kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund) ili uweze kufikia lengo la kukusanya kiasi cha Dola za Marekani bilioni 18 zitakazotumika kutokomeza magonjwa hayo duniani kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo.

Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati akihutubia Mkutano wa saba wa kuwezesha mfuko huo uliofanyika New York nchini Marekani.

Amesema migogoro ya sasa ya kimataifa imepunguza juhudi za kurejesha uchumi wa nchi nyingi ulioathirika na janga la UVIKO-19 na kuongeza changamoto mpya katika kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu, hivyo hakuna budi wote kwa pamoja kuona haja ya kuunga mkono kazi nzuri ya Mfuko huo wa Kimataifa ili kuendeleza mafanikio katika kukabiliana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria.

Wavunaji Mkaa Watakiwa Kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) akizungumza bungeni jijini Dodoma leo akiwataka wavunaji wa mkaa kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu.


Serikali imewataka wananchi wanaofanya biashara ya mkaa kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu kwa kuwa kumekuwa na wimbi la uvunaji wa mazao ya misitu, ukataji na uchomaji wa mkaa bila kufuata sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia biashara hiyo.

Hayo yamesemwa leo Septemba 22, 2022 na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii alipokuwa akijibu swali la Nicodemus Maganga (Mbogwe).

“Inapotokea mwananchi anasafirisha mazao ya misitu (mkaa) bila kufuata utaratibu, mazao hayo hutaifishwa na Serikali”, Mhe. Masanja amesisitiza.

Amesema uvunaji holela wa mkaa umesababisha kutoweka kwa kasi kwa maeneo ya misitu na hatimaye kujitokeza kwa athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Zaidi ya Shilingi Milioni 183 Kuhudumia Timu za Taifa

Na Shamimu Nyaki

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe.Pauline Gekul, amesema kiasi cha Shilingi milioni 183.5 zimetengwa katika mwaka wa fedha 2022/23 kwa ajili ya kuhudumia timu za Taifa.

Mhe. Gekul ameeleza hayo bungeni jijini Dodoma leo Septemba 22, 2022 wakati akijibu swali la Mhe. Janeth Elius Mahawanga (Viti Maalum) aliyeuliza ni lini Serikali itawekeza katika Sekta ya Michezo hasa kwenye timu za Wanawake ili kuibua vipaji kwa watoto.

ev eşyası depolama