Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Nditiye: Shule za Sekondari Kibondo Zaongoza Ufaulu Kitaifa

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa pili kushoto) akishiriki uzinduzi wa Kituo cha Afya cha Mabamba kilichopo kwenye jimbo lake la Muhambwe wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru za kitaifa uliofanyiwa na kiongozi wa kitaifa wa mbio hizo Bwana Charles Kabeho (wa tatu kushoto) kwenye kata ya Mabamba wilayani Kibondo, Kigoma.

Na: Mwandishi Wetu

Shule za sekondari za Wilaya ya Kibondo zaongoza kwa ufaulu wa elimu katika ngazi ya kitaifa kwa miaka miwili mfululizo na kushika nafasi kati ya shule kumi bora za kitaifa na kuzishinda wilaya nyingine zote nchini

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (Mb) wakati akipokea mbio za mwenge wa Uhuru ulipowasili Wilaya ya Kibondo kwenye jimbo lake la Muhambwe ukitokea Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma. Amesema kuwa Wilaya ya Kibondo imeongoza kwa ufaulu wa shule za sekondari kwa miaka miwili mfululizo ya masomo mwaka 2016 na 2017 ambapo kidato cha pili wameshika nafasi ya nane kitaifa na kidato cha nne wameshika nafasi ya tisa kitaifa na kuzibwaga sekondari nyingine zilizopo kwenye jumla ya Wilaya 187 nchini.

Nditiye amefafanua kuwa shule hizo zimezawadiwa kiasi cha shilingi milioni 680 na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Mpango wa Elimu kwa Matokeo (E4P) ambao umeleta chachu, ari na ushindani kwenye kiwango cha ufaulu kwenye shule mbalimbali nchini. Amefafanua kuwa fedha hizo zimetumika kugharamia upatikanaji wa miundombinu mbalimbali kwenye shule ya sekondari ya Malagarasi na ya Wasichana ya Kibondo.

Mkuu wa Wilaya ya Kibondo Mheshimiwa Loyce Bura (kulia) akipokea mbio za Mwenge wa Uhuru wa Taifa kwenye kijiji cha Mkubwa kilichopo mpakani mwa Wilaya ya Kibondo na Kakonko.

Ameongeza kuwa ushindi huo umeleta chachu na mwamko zaidi kwa wanafunzi, walimu, wazazi, walezi na wadau wa elimu kwenye Wilaya hiyo ambapo wamejipanga kuchangia ujenzi wa miundombinu mbali mbali kwenye shule za Wilaya hiyo ili kuongeza ufaulu kwa wanafunzi ambapo imeendana na kauli Mbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu isemayo, “Elimu ni Ufunguo wa Maisha, Wekeza Sasa kwenye Elimu kwa Maendeleo ya Taifa”.

Mhandisi Nditiye amesema kuwa Wilaya ya Kibondo inaunga mkono jitihada za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muunano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli za kutoa elimu bure nchini kote kwa shule za msingi na sekondari ambapo wazazi hawalipi ada yeyote hivyo inawawezesha kushirikiana kuendeleza miundombinu ya shule na mahitaji ya huduma nyingine ili wanafunzi waweze kujisomea na hivyo kuongeza ufaulu wao.

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akigawa chandarua kwa wanawake wenye watoto baada ya uzinduzi wa kituo cha Afya cha Mabamba kilichopo kwenye jimbo lake la Muhambwe wilayani Kibondo, Kigoma wakati wa mbio za Mwenge wa uhuru za kitaifa

Naye kiongozi wa kitaifa wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu Bwana Charles Kabeho amewataka wazazi na walezi kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha kuwa wanamuunga mkono Mhe. Rais wa nchini yetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata sare za shule, vitabu vya masomo mbali mbali na miundombinu mingine ili kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia kwa manufaa ya wanafunzi na walimu.

Amefafanua kuwa azma ya Dkt. Magufuli ni kuwa na nchi ya viwanda na kufikia uchumi wa kati ambapo haya yote hayawezekani pasipo kuwa na taifa lenye rasilimali watu yenye elimu, ujuzi na maarifa ya kuendesha na kusimamia viwanda vyetu.

Bwana Kabeho amemshukuru na kumpongeza Mhandisi Nditiye kwa kutambua umuhimu wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa na kujumuika na wananchi wa jimbo lake la Muhambwe lililopo kwenye Wilaya ya Kibondo. “Mheshimiwa Nditiye, natambua majukumu uliyonayo katika kipindi hiki cha Bunge la bajeti ambalo linaendelea mkoani Dodoma lakini umejali na kuja kujumuika nasi katika kuzindua miradi mbali mbali ya maendeleo kwenye Wilaya hii,” amesema Kabeho.

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye, Mbunge wa jimbo la Muhambwe wilayani Kibondo, Kigoma akipiga ngoma kuburudisha wapiga kura wake wakati wa kupokea mbio za Mwenge wa Uhuru za kitaifa uliowasili kwenye Wilaya hiyo.

Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa zimepokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Kibondo Mheshimiwa Loyce Bura kwenye kijiji cha Mkubwa mpakani mwa Wilaya ya Kibondo ukitokea kwenye Wilaya ya Kakonko. Mwenge umetembezwa kwenye Wilaya ya Kibondo na kuzindua miradi mbali mbali ya maendeleo yenye jumla ya thamani ya shilingi 1,512,000,000 ikiwemo kituo cha Afya cha Mabamba, kiwanda cha kusindika na kuzalisha unga wa muhogo, ofisi ya ushauri wa kibiashara, hoteli na kugawa asiimia kumi ya mapato ya Halmashauri hiyo kwa vikundi vya wajasiriamali wanawake, vijana na walemavu kiasi cha shilingi milioni 58.

Mwenge umekabidhiwa kwenye Wilaya ya Kasulu ili kuendelea na mbio zake na kuzindua miradi mbali mbali ya maendeleo nchini ambapo makabidhiano hayo yamefanyika kwenye kijiji cha Mvugwe mpakani mwa Wilaya ya Kibondo na Kasulu.

Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,

Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

 

90 thoughts on “Nditiye: Shule za Sekondari Kibondo Zaongoza Ufaulu Kitaifa

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama