Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Nditiye Apiga Marufuku Umeme wa Solkit Wilayani Kibondo

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akihutubia wananchi wa kata ya Busunzu iliyopo jimboni kwake Muhambwe wilayani Kibondo mkoani Kigoma wakati akikagua maendeleo ye ujenzi wa kituo cha afya cha kata hiyo baada ya kushiriki mbio za mwenge wa uhuru wa kitaifa wilayani humo mkoani Kigoma

Na Mwandishi Wetu

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye amepiga marufuku kampuni ya Solkit inayosambaza na kuuza vifaa vya umeme wa jua kwa wananchi wa jimbo la Muhambwe lililopo wilayani Kibondo mkoani Kigoma

Nditiye amesema hayo akiwa kwenye ziara jimboni kwake Muhambwe wakati akiwahutubia wananchi alipofika kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo cha afya cha Busunzu kilichopo wilayani Kibondo mkoani Kigoma. Aliwasili Wiayani humo wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru za kitaifa kwenye wilaya hiyo ambapo alijumuika na wananchi wake kukimbiza Mwenge na kukagua na kuzindua miradi mbali mbali ya maendeleo Wilayani humo.

Amesema kuwa Kampuni ya Solkit ni kampuni binafsi inayouza na kusambaza vifaa vya umeme wa jua kwa wananchi wa jimbo lake hilo kwa gharama kubwa ambazo ziko nje ya uwezo wa wananchi kwa kuingia nao mikataba ya utata isiyokuwa na uwazi ambayo inawataka wananchi walipie kiasi cha shilingi 38,000 kwa ajili ya kununua vifaa vya kampuni hiyo na kuendelea kulipia shilingi mia saba kwa siku kwa kipindi cha mwaka mzima kwa muda wa miaka mitatu.

Muonekano wa kifaa cha umeme cha kampuni ya Solkit iliyopigwa marufuku na Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye kusambaza umeme kwa gharama kubwa kwa wananchi wa jimboni kwake Muhambwe wilayani Kibondo mkoani Kigoma

Amefafanua kuwa kiwango hicho ni kikubwa kwa wananchi wa jimbo lake ukilinganisha na gharama nafuu zinazotozwa na taasisi ya Serikali inayohusika kusambaza umeme vijijini, taasisi ya REA ambapo mwananchi anaweza kulipa kiasi cha shilingi elfu tatu hadi tano tu kwa mwezi ambapo gharama za kampuni ya Solkit zipo nje ya uwezo wa kiuchumi wa kaya husika na fedha wanazotumia kununua umeme wa kampuni hiyo zingeweza kutumika kuipatia familia husika mahitaji mengine ya kijamii na kiuchumi.

Amewaeleza wananchi wa jimbo lake kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli ina lengo na dhamira ya dhati ya kuwapatia wananchi umeme wa gharama nafuu kupitia taasisi ya Serikali ya REA inayosambaza umeme vijijini.

“Wananchi tumeshuhudia uzinduzi wa Awamu ya Tatu ya umeme wa REA ikifanyika kwenye kata yetu ya Mabamba ambapo ulifanywa na Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani, hizi zote ni jitihada za Serikali yetu kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata umeme ili kutekeleza majukumu yake, kuendesha shughuli za kiuchumi na kijamii ambazo zitawawezesha kuongeza kipato cha familia na taifa kwa ujumla” amesema Nditiye.

 

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akikagua maendeleo ya ujenzi wa choo cha wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Misezero ambapo aliwapatia sementi kwa ujenzi wa choo hicho kilichopo jimboni kwake Muhambwe wilayani Kibondo mkoani Kigoma

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akiwapongeza wanafunzi wa shule ya sekondari ya Olivegreen iliyopo kwenye jimbo lake la Muhambwe wilayani Kibondo, Kigoma kwa ufaulu mzuri katika ngazi ya mkoa na hivyo wilaya hiyo kuongoza kitaifa

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Busunzu Bwana Zacharia Mbumba alimshukuru Nditiye kwa kupiga marufuku Kampuni ya Solkit kwenye Wilaya ya Kibondo kwa kuwa gharama za ununuzi na malipo ya umeme wa kampuni hiyo kwa siku kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo ni kubwa ukilinganisha na gharama za umeme wa vijijini unaotelwa na Serikali kupitia REA pamoja na hali ya kipato cha mwanakijiji.

Pia Ameongeza kuwa wanakijiji wameitikia wito wa kuchangia asilimia 20 za gharama za ujenzi wa kituo cha afya cha kata ya Busunzu ili kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi ambapo kituo hicho kinahitaji jumla ya shilingi milioni 133 ili ujenzi wake uweze kukamilika ambapo wananchi wanatarajia kuchangia shilingi milioni 13 na tayari wamekusanya kiasi cha shilingi milioni mbili na wananchi wamekubaliana kuchangia shilingi elfu mbili kwa kila mmoja kwa mwananchi aliyefikisha umri kati ya miaka 18 hadi 59.

Mwenyekiti wa CCM wa Kata ya Busunzu Bwana Gilesi Kagoma amesema kuwa, “ujenzi wa kituo cha afya inatuhusu wote na haichagui huyu wa CCM au CHADEMA kwa kuwa sote ni wanufaika na kituo kikikamilika tutanufaika wote,” amesema. Aidha, Nditiye ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Muhambwe ambapo kituo hicho cha afya kipo ndani ya jimbo hilo amechangia mifuko mia moja ya sementi kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho na amewaahidi kuendelea kuchangia kadri ujenzi unavyoendelea. Pia, amewapongeza wananchi kwa walivyojitoa na kuchangia ujenzi wa kituo hicho.

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akikagua maendeleo ya ukarabati wa bweni la wanafunzi wa shule ya sekondari ya kiislamu ya Kakangaga baada ya kuunga na moto ambapo amewapatia mifuko ya sementi 20 na mabati 24 iliyopo jimboni kwake Muhambwe wilayani Kibondo mkoani Kigoma

Nditiye pia amefanya ziara ya kukagua maendeleo ya shule za sekondari za Misezero na Olivegreen ambapo amechangia mifuko ya sementi, kompyuta, vitabu vya waalimu kwa ajili ya kufundishia, matengenezo ya barabara zinaingia shuleni, kufikisha umeme kwenye majengo ya shule, kukagua ujenzi wa miundombinu ya madarasa na vyoo ambapo alitoa sementi kwa ajili hiyo na kukaguabweni la shule ya sekondari ya Kakangaga iliyoungua na moto ambapo amewapatia mifuko 20 ya sementi, mabati 24 na kompyuta mbili ili kukamilisha ujenzi wa bweni hilo.

 

54 thoughts on “Nditiye Apiga Marufuku Umeme wa Solkit Wilayani Kibondo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama