Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Nchi za Mashariki Mwa Afrika Zadhamiria Kuimarisha Uchumi kwa Kuuziana Umeme

Baadhi ya Mawaziri/Naibu Mawaziri wanaohusika na Umeme kutoka nchi za ukanda wa Mashariki mwa Afrika ambazo zimeunganishiwa mifumo ya kusafirisha umeme baina yake (Eastern Africa Power Pool – EAPP). Katikati ni Mwenyekiti wa Baraza hilo la Mawaziri la EAPP, Mhandisi Irene Muloni (Uganda) na wa pili kutoka kushoto ni Naibu Waziri wa Nishati (Tanzania), Subira Mgalu. Walikuwa katika Mkutano wao wa 14 uliofanyika Entebbe, Uganda, Februari 21. 2019.

Na Veronica Simba – Entebbe

Nchi zilizopo Mashariki mwa Afrika, zimedhamiria kwa nia moja kuimarisha uchumi wao kwa kuuziana umeme kupitia mifumo ya kusafirisha nishati hiyo iliyounganishwa katika ukanda husika.

Hayo yalibainishwa jana Februari 21 mwaka huu, katika Mkutano wa 14 wa Baraza la Mawaziri wanaohusika na umeme kutoka nchi za ukanda huo, ambazo zimeunganishiwa mifumo ya kusafirisha umeme baina yake (Eastern Africa Power Pool – EAPP).

Akizungumza mara baada ya Mkutano huo uliofanyika mjini Entebbe nchini Uganda, Naibu Waziri wa Nishati (Tanzania) Subira Mgalu, alieleza kuwa nchi wanachama wa EAPP wamelenga kuhakikisha wananchi wao wanakuwa na umeme wa kutosha, uhakika na wenye gharama nafuu.

Akifafanua zaidi, Naibu Waziri alitoa mfano wa Ethiopia na Misri ambao alisema wanazalisha umeme mwingi hivyo wanaweza wakauzia nchi nyingine za ukanda husika ikiwemo Tanzania kwa bei nafuu.

Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe wa Tanzania ulioshiriki katika Mkutano wa 14 wa Baraza la Mawaziri wanaohusika na Umeme kutoka nchi za ukanda wa Mashariki mwa Afrika zilizounganishiwa mifumo ya kusafirisha umeme baina yake (Eastern Africa Power Pool – EAPP). Kulia kwa Naibu Waziri ni Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Dkt. Aziz Mlima. Mkutano huo ulifanyika Februari 21, 2019 Entebbe, Uganda.

Awali akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Umoja huo, Mhandisi Irene Muloni (Uganda), alibainisha kuwa hakuna nchi yoyote duniani iliyoendelea katika sekta ya viwanda  pasipo kuwa na umeme mwingi wa uhakika na wenye gharama nafuu.

Aliongeza kuwa, ni kwa sababu hiyo nchi wanachama wa EAPP zimedhamiria kwa dhati kuimarisha uchumi wa viwanda kwa kuungana na kushirikiana katika kutumia kikamilifu vyanzo vyake vyote vya uzalishaji umeme ambavyo zimejaaliwa.

“Pamoja na nchi zetu kujaaliwa vyanzo mbalimbali vya kuzalisha umeme vikiwemo maji, upepo, jua, gesi asilia na vingine vingi lakini bado tunakabiliwa na umaskini wa nishati hiyo adhimu,” alifafanua.

Akizungumzia mifumo mbalimbali ya umeme inayounganisha nchi hizo ambayo ikitumika vizuri itaunufaisha ukanda husika; aliitaja kuwa ni pamoja na njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 500 kutoka Ethiopia hadi Kenya, kilovolti 400 kutoka Tanzania hadi Kenya na msongo wa kilovolti 220 kutoka Kenya hadi Uganda.

Nyingine ni njia ya kusafirisha umeme wa kilovolti 220 kutoka Uganda hadi Rwanda pamoja na mifumo unganishi ya umeme kati ya Rwanda, Burundi na DRC.

“Ni matumaini yangu kuwa mifumo unganishi mingi zaidi ya umeme, itaendelea kujengwa katika ukanda wetu ili itusaidie kupata matokeo chanya zaidi na hivyo kuimarisha uchumi wa nchi zetu,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Mgalu, akizungumzia manufaa mengine ambayo Tanzania inayapata kupitia umoja huo wa EAPP, alisema ni pamoja na kusaidiwa na Washirika wa Maendeleo ambao wanafadhili miradi mbalimbali ya umoja huo.

“Kwa mfano sasa tumeanza ujenzi wa mradi mkubwa wa laini ya msongo wa kilovoti 400 ambayo inatoka Singida hadi Namanga pamoja na ujenzi wa laini ya msongo wa kusafirisha umeme wa kilovoti 400 ambao unatoka Iringa, Mbeya, Tunduma, Songea hadi Sumbawanga. Miradi hii inafadhiliwa na Benki ya Dunia,” alifafanua.

Suala jingine muhimu lililojadiliwa na kupitishwa na mkutano huo ni maboresho ya mkataba wa ushirikiano kwa nchi wanachama wa EAPP.

Mkutano huo wa Baraza la Mawaziri ulitanguliwa na Mkutano wa Kamati Tendaji ambayo ni ngazi ya wataalamu kutoka nchi za umoja huo, uliofanyika Februari 20, 2019.

Naibu Waziri alimwakilisha Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani katika mkutano huo ambapo pia aliambatana na Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Dkt. Aziz Mlima pamoja na timu ya wataalamu akiwemo Kamishna wa Umeme na Nishati Mbadala, Mhandisi Innocent Luoga na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Dkt. Tito Mwinuka.

Nchi wanachama wa EAPP ni Tanzania, Uganda, Kenya, Burundi, Ethiopia, Libya, Sudan, Misri, Rwanda, DRC na Djibouti.

 

55 thoughts on “Nchi za Mashariki Mwa Afrika Zadhamiria Kuimarisha Uchumi kwa Kuuziana Umeme

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama