Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Naibu Waziri wa Maliasili, Japhet Hasunga Afungua Kituo Cha Mafunzo ya Misitu Mkoani Iringa

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kulia) na Balozi wa Finland nchini, Mhe. Peka Huka wakikata utepe kuashiria ufunguzi rasmi wa Kituo cha Mafunzo ya Misitu na Uchakataji wa Magogo kilichoanzishwa mwezi  Desemba, 2016 katikamji wa Mafinga, Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa chini ya ufadhili wa Serikali ya Finland katika hafla iliyofanyika jana mkoani humo.

 
Na: Hamza Temba-WMU-Iringa
 
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga amefungua Kituo cha Mafunzo ya Misitu na Uchakataji wa Magogo ambacho kimeanzishwa katika Mji wa Mafinga, Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa chini ya ufadhili wa Serikali ya Finland kupitia mradi wa Panda Miti Kibiashara.
 
Akizungumza kwenye hotuba yake ya ufunguzi wa kituo hicho jana mjini hapa, Naibu Waziri Hasunga ameishukuru Serikali ya Finland kwa msaada huo na misaada mingine ambayo imekuwa ikiitoa katika kuimarisha sekta ya Misitu nchini toka miaka ya 1970s.  
Katika hatua nyingine amemuagiza Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki wa Wizara hiyo, Dk. Ezekiel Mwakalukwa kukagua viwanda vyote vya misitu nchini kwa ajili ya kujiridhisha kama vinakidhi vigezo vilivyowekwa na wizara ikiwemo kuwa na wafanyakazi wenye ujuzi unaostahili.
 

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kulia) akipanda mti wa kumbukumbu muda mfupi baada ya kufungua rasmi Kituo cha Mafunzo ya Misitu na Uchakataji wa Magogo kilichoanzishwa katika mji wa Mafinga, Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa chini ya ufadhili wa Serikali ya Finland. Kutoka kushoto wa tatu ni Balozi wa Finland nchini, Mhe. Peka Huka, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Amina Masenza.

Balozi wa Finland nchini Tanzania, Mhe. Peka Huka akipanda mti wa kumbukumbu muda mfupi baada ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kulia) kufungua rasmi Kituo cha Mafunzo ya Misitu na Uchakataji wa Magogo kilichoanzishwa mwezi Desemba, 2016 katika mji wa Mafinga, Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa chini ya ufadhili wa Serikali ya Finland. Kutoka kulia wa tatu ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Amina Masenza, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Christina Mndeme na Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi.

Alisema lengo la kituo hicho ni kusaidia kutoa elimu kwa vitendo na ujuzi kwa makundi mbalimbali ambayo yapo katika mnyororo wa kuongeza thamani ya mazao ya misitu ikiwemo watu binafsi, viwanda vya misitu na taasisi za Serikali kuanzia hatua za mwanzo za upandaji wa miche ya miti hadi kwenye hatua za mwisho za uchakataji wa magogo.

Aidha, kutokana na kituo hicho kuwa chini ya mradi huo, Naibu Waziri Hasunga amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Meja Jenerali Gaudence Milanzi kuangalia uwezekano wa kukiweka kituo hicho chini ya Wizara yake ili mafunzo yanayotolewa yawe endelevu hata kama mradi husika utafikia ukiongoni.

Pia, ameagiza mitaala ya kituo hicho ipitiwe na isajiliwe kupitia Mfumo wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi– VETA ili yaweze kutambulika na wahitimu wapewe vyeti kulingana na mahitaji ya soko katika sekta ya viwanda vya misitu nchini.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kulia) akimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Gaudence Milanzi jana muda mfupi baada ya kufungua rasmi Kituo cha Mafunzo ya Misitu na Uchakataji wa Magogo kilichoanzishwa mwezi  Desemba, 2016 katika mji wa Mafinga, Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa chini ya ufadhili wa Serikali ya Finland. Wengine pichani ni Balozi wa Finland nchini, Mhe. Peka Huka (wa pili kushoto) na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Christina Mndeme.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (wa pili kushoto) ambaye alikuwa mgeni rasmi akiwasilisha hotuba  yake wakati wa hafla hiyo.

Alisema uwepo wa kituo hicho cha mafunzo utawezesha viwanda hivyo kuwapatia mafunzo kwa vitendo wafanyakazi wake ambao hawana vigezo ili waweze kukidhi vigezo na ujuzi stahiki ikiwemo kuwa na Fundi Misumeno, Fundi Mwendesha Mashine ya Kuchakata Magogo na Fundi Mitambo.
Alitoa wito kwa wananchi wa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini pamoja na maeneo mengine nchini kujiunga na kituo hicho waweze kupata mafunzo ya kitaalamu na ujuzi wa kuotesha miti kwa njia za kisasa iweze kuzalisha mbao na samani zenye ubora zaidi.

Kwa upande wa Balozi wa Finland, Mhe. Peka Huka amesema nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuboresha sekta ya misitu nchini iweze kutoa mchango chanya kwa jamii na taifa ujumla.

Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi (kushoto) akitoa salamu za shukurani muda mfupi jana baada ya Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Japhet Hasunga (wa tatu kushoto) kufungua rasmi Kituo cha Mafunzo ya Misitu na Uchakataji wa Magogo kilichoanzishwa mwezi Desemba, 2016 katika mji wa Mafinga, Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa chini ya ufadhili wa Serikali ya Finland. Wengine kushoto kwake ni Balozi wa Finland nchini Tanzania, Mhe. Peka Huka, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Amina Masenza na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Christina Mndeme.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kulia) akimsikiliza Mshauri wa Masuala ya Misitu kutoka sekta binafsi, Sangito Sumari wakati akitoa maelezo juu ya miche ya kisasa ya miti iliyoboreshwa muda mfupi baada ya kufungua rasmi Kituo cha Mafunzo ya Misitu na Uchakataji wa Magogo kilichoanzishwa mwezi  Desemba, 2016 katika mji wa Mafinga, Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa chini ya ufadhili wa Serikali ya Finland. Kushoto kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Amina Masenza na Balozi wa Finland nchini, Mhe. Peka Huka.

Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Ezekiel Mwakalukwa (kulia) akiongoza hafla hiyo ya ufunguzi.

 

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (wa pili kulia) akiangalia mbao zinavyoandaliwa katika moja ya karakana ya kituo hicho. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Gaudence Milanzi na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Christina Mndeme (wa tatu kulia).

Baadhi ya wanafunzi kutoka Chuo cha Misitu Olmotonyi na Chuo cha Viwanda vya Misitu Moshi (wanaopunga mikono) ambao wanapatiwa mafunzo kwa vitendo katika kituo hicho.

Naye Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi amesema kituo hicho kitatoa fursa pana ya mafunzo kwa makundi mbalimbali katika sekta ya misitu nchini tofauti na vituo vingine ambavyo huitaji vigezo mbalimbali vya kitaaluma kujiunga. Alisema maelekezo yote yaliyotolewa na Naibu Waziri Hasunga yatafanyiwa kazi ili kuimarisha sekta hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alisema Serikali ya Mkoa wake imefurahishwa kwa kuanzishwa kwa kituo hicho cha mafunzo katika mkoa wake na kuahidi kushirikiana na mamlaka zingine kukilinda na kukiendeleza. Alisema katika maeneo aliyopanga kumpeleka Mhe. Rais kwenye ziara zake mkoani humo ya kwanza itakuwa katika kituo hicho.

Toka kuanzishwa kwake mwezi Desemba mwaka jana, 2016 mpaka sasa kituo hicho cha mafunzo kimeshaandaa na kuendesha zaidi ya kozi 20 kwa ajili ya usimamizi wa misitu, afya na usalama kazini, huduma ya kwanza, ujasiriamali na ufundishaji. Wastani wa muda wa mafunzo yanayotolewa kituoni hapo ni siku nne ambapo jumla ya washiriki 400 wameshapatiwa mafunzo hayo huku wanawake ikiwa ni asilimia 35.

Aidha kwa sasa jumla ya wanafunzi 40 kutoka Chuo cha Misitu Olmotonyi na Chuo cha Viwanda vya Misitu Moshi wanapatiwa mafunzo kwa vitendo katika kituo hicho.

 

91 thoughts on “Naibu Waziri wa Maliasili, Japhet Hasunga Afungua Kituo Cha Mafunzo ya Misitu Mkoani Iringa

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama