Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Naibu Waziri Ikupa Alipongeza Shirika la Compassion International kwa Kusaidia Watoto na Vijana Nchini

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu Mhe. Stella Ikupa akizungumza na washiriki waliohudhuria katika Maadhimisho ya Miaka 20 ya Shirika la Compassion International Tanzania yaliyofanyika Aprili 27, 2019 katika ukumbi wa Kanisa la TAG lililopo Kata ya Miyuji, Jijini Dodoma.

Na. Mwandishi Wetu

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu Mhe. Stella Ikupa amelipongeza Shirika lisilo la kiserikali la Compassion International Tanzania (CIT) kwa kuwahudumia na kuwapatia watoto na vijana stadi za maisha zinazowawezesha kujitegemea.

Naibu Waziri Ikupa ametoa pongezi hizo wakati wa Maadhimisho ya Miaka 20 ya Shirika hilo yaliyofanyika leo Aprili 27, 2019 katika ukumbi wa Kanisa la TAG lililopo Mipango, Jijini Dodoma. Maadhimisho hayo yalikuwa na Kauli Mbiu isemayo; “Wekeza kwa Watoto na Vijana kwa Uchumi Endelevu.”

Alieleza kuwa Shirika la Compassion International Tanzania limekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha watoto na vijana nchini wanahudumiwa na kuondokana na hali ya umasikini kwa kuwa chachu ya maendeleo kwa jamii na Taifa.

“Shirika hili ni la mfano na limeendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuwalinda watoto na kuwapa fursa ya kufikia ndoto zao na kuwapatia vijana ujuzi wa stadi za maisha zinazoleta mabadiliko chanya kwao na kuwaletea maendeleo yao binafsi na Taifa kwa ujumla,” alisema Ikupa

Baadhi ya Maaskofu kutoka kwenye Makanisa ya Kiinjili hapa nchini wakifuatilia hotuba ya Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu Mhe. Stella Ikupa (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza wakati wa hafla hiyo.

Aliongeza kuwa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amekuwa akionesha watanzania namna gani nchi yetu imeweza kujitegemea katika kutekeleza shughuli mbalimbali, hivyo Mhe. Rais ni mfano tosha wa kuigwa na vijana nchini kwa kuona wanauwezo wa kujitegemea.

Aidha, Naibu Waziri Ikupa alitoa rai kwa vijana kuacha kukaa kwenye vijiwe bila sababu za msingi na kubadili mitazamo, bali watumie muda wao kutafakari shughuli za kufanya kwa bidii ambazo zitawaletea maendeleo na kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.

“Serikali imekuwa ikitoa mikopo kwa vijana ili waweze kuanzisha shughuli mbalimbali zitakazo wawezesha kukua kiuchumi, tumieni fursa ya ujuzi mliopata kupitia shirika hili na ubunifu mlionao kuchangamkia fursa hiyo muhimu itakayowawezesha kuanzisha miradi mbalimbali ikiwemo viwanda,” alisema Ikupa

Pia alitoa wito kwa jamii kuripoti haraka vitendo vya unyanyasaji wa watoto katika madawati ya jinsia na watoto yaliyopo kwenye vituo vya polisi nchini na kwa maafisa ustawi wa jamii ili kutokomeza vitendo hivyo kwa kumjengea mazingira salama motto na kumuonesha jamii yake imejaa upendo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taifa wa Shirika la Compassion International Tanzania, Bi. Agness Stanley Hotay alisema kuwa wataendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha wanawatetea na kuwasimamia watoto na kuwapatia nafasi vijana ya kujitambua kwa kuchangamkia fursa ambazo zipo katika jamii na kuleta ufumbuzi wa kimaendeleo.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu Mhe. Stella Ikupa akisikiliza kwa mmoja wa vijana wanaohudumiwa na Shirika la Compassion International Tanzania namna wanavyotengeneza bidhaa za Viatu vya ngozi.

“Maono ya shirika ni kuona wanufaika wanatoka katika uhitaji na kujijengea dhana ya kujitegemea, vilevile kuwa wahisani wa watu wengine,” alisema Hotay

Shirika la Compassion International Tanzania (CIT) ni sehemu ya Compassion International ambalo ni shirika la kimataifa la Kikristo linalojihusisha kuhudumia watoto na vijana wanaotoka katika kaya maskini kwa njia ya ufadhili. Shirika hili limekuwa likifanya huduma hii hapa nchini toka mwaka 1999.

Kwa sasa Shirika hilo lipo katika Mikoa 19 ya Tanzania Bara ambayo ni Arusha, Dar es Salaam, Kigoma, Manyara, Pwani, Morogoro, Iringa, Dodoma, Kilimanjaro, Singida, Shinyanga, Mwanza, Mara, Tabora, Lindi, Geita, Mtwara, Simiyu na Kagera.

185 thoughts on “Naibu Waziri Ikupa Alipongeza Shirika la Compassion International kwa Kusaidia Watoto na Vijana Nchini

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama