Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Naibu Waziri Ardhi Aigiza Kigamboni Kusitisha Utoaji Hati.

Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Bw.Hashim Mgandilwa akimkaribisha Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Angelina Mabula katika ofisi za Wilaya hiyo kukagua mfumo mpya wa ukusanyaji kodi ya pango la ardhi kwa njia ya kielektroniki katika ziara yake ya kikazi leo Jijini Dar es Salaam.

Na. Paschal Dotto

 Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Angelina Mabula ameitaka Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni kusitisha utoaji hati kwa eneo la mradi wa kampuni ya AVEC ambalo lina mgogoro wa umiliki ili kuepusha migogoro ya ardhi iliyoko katika Manispaa hiyo.

Akizungumuza na watumishi wa manispaa ya Kigamboni Mhe. Mabula alisema kuwa kwa maeneo ambayo bado hayajapatiwa hati na vibali vya ujenzi wahakikishe yanatolewa hati sahihi bila kuleta migogoro kwa wananchi.

“Migogoro ya ardhi mingi husababishwa na utoaji hati bila kufanya uchunguzi wa umiliki wa maeneo. Mkurugenzi na na watu wake wanaweza kukaa na kufanya upembuzi maalum ili kutoa hati sahihi, bila kufanya hivyo msitoe hati maana hii ndiyo husababisha kuwepo kwa migogoro ya ardhi kwenye Manispaa nyingi nchini”, alisema Mhe. Mabula.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Angelina Mabula akikagua orodha ya wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi kwa Manispaa ya Kigamboni kulia ni Mkuu wa Wilaya hiyo Bw. Hashim Mgandilwa na kushoto ni Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Bw. Stephen Katemba katika ziara yake leo Jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Angelina Mabula akikagua mafaili ya umilikishaji ardhi katika Masjala ya Manispaa ya Kigamboni wakati wa ziara yake katika Manispaa ya Kigamboni leo.

Aidha aliwataka watumishi wa Manispaa hiyo kuwabana wamiliki wa viwanja mbalimbali ilikubaini kama wana hati kamili na kulipa kodi ya ardhi ili kuiwezesha idara hiyo kujiendesha katika shughuli zake lakini pia aliwaonya wasitoe hati hizo kwa maeneo yenye utata.

“Kwa wale ambao wanajenga nyumba za kawaida huwa ni miezi 36 na mashamba ni miezi 48 kwa hiyo kama hajalipa kwa miezi yote hiyo anatakiwa kufikishwa kwenye Baraza Kuu, sasa fanyeni ukaguzi wa maeneo yenu kwa sababu mji huu uko kwenye  mpango mji”, alisisitiza Mhe. Mabula.

Aliongeza kuwa katika ujenzi wa mji huo, watumishi wanapaswa kuwajibika kuwaelimisha wananchi kujenga kwa kufuata sheria za ujenzi ili kuondo usumbufu wa badae. Aidha, Naibu Waziri aliwasisitiza watumishi hao kufanya ukaguzi ili kubaini watu waliojenga vibali kwa sababu migogoro mingi katika Manispaa ya kigamboni inasababishwa na watu kutokuwa na vibali.

Maneja Masoko wa Kampuni ya Ujenzi Makazi ya Hamidu City Park Bi. Judith Eminice (kulia) akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Angelina Mabula (kushoto) kuhusu mradi wa nyumba ulioko katika Manispaa ya Kigamboni katika ziara yake kukagua mfumo mpya wa ukusanyaji kodi pango la ardhi kwa njia ya kielektroniki leo Jijini Dar es Salaam. Wapili kushoto ni Mkuu wa Wilaya hiyo Bw. Hashim Mgandilwa. (Picha na: Paschal Dotto)

Mtu anaweza kuwa na kiwanja halali na hati ya umiliki, lakini anapojenga amaepata kibali kutoka Manispaa, kama hana kibali lazima mfuatilie, na lazima apigwe faini ili alipe tozo zote  za Serikali”, aliongeza Mhe. Mabula.

Akibainisha chanzo cha migogoro Mhe.         Mabula alisema kuwa katika Manispaa hiyo kumekuwa na Wenyekiti wa vijiji kujiingiza katika ununuzi wa viwanja na utoaji hati kitu ambacho kinaleta migogoro mingi kwa wananchi.

Aliwataka wenyeviti wa mitaa kuacha kujihusisha kabisa na masuala ya umilikishaji wa ardahi ili kuondoa migogoro ya ardhi katika Manispaa ya Kigamboni.

110 thoughts on “Naibu Waziri Ardhi Aigiza Kigamboni Kusitisha Utoaji Hati.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama