Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Wakuu wa Wilaya Waaswa Kutatua Migogoro Sehemu za Machimbo

Mashine ya kuchimba na kupakua mchanga wa Jasi katika mgodi wa Yusufu Kabila ambao ni General Business and Equipment Suppliers ltd

Na. Rhoda James, Manyoni

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula ameagiza Wakuu wa wilaya nchini kutatua migogoro ya wachimbaji wa  madini inayojitokeza katika maeneo yao ili kuepusha madhara yatokanayo na ucheleweshwaji wa utatuzi wa migogoro hiyo inayopelekea migogoro hiyo kufikishwa katika ngazi za juu.

Profesa Kikula ametoa kauli hiyo leo tarehe 15 October, 2018 wakati alipokuwa kwenye ziara yake katika wilaya ya Manyoni mkoani Singida.

Akizungumza katika kikao hicho, Profesa Kikula aliwaasa Wakuu wa Wilaya kushirikiana na viongozi wa vijiji, viongozi wa kata kuelewa vyema vyanzo vya migogoro sehemu za machimbo pamoja  na kuitatua.

Muonekano wa Machimbo ya mgodi wa dhahabu wa Muhintiri kijiji cha Muhintiri wilaya ya ikungi

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (kulia kwa mkuu wa wilaya) akizungumza jambo mbele ya Mkuu wa wilaya ya Manyoni Rahabu Mwagisa (katikati), wengine ni Makamishna wa Tume ya Madini Abudulkarim Mruma ( mwenye shati la draft) na Kamishna wa Tume Dkt. Athanas Macheyeki wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wilayani humo.

“Tume ya madini haiwezi kutatua migogoro yote nchi nzima, lazima tushirikiane katika hilo ili kuwasaidia wanachi kupata haki yao kwa wakati” alisema Profesa Kikula.

Profesa Kikula aliongeza kuwa, wapo wenyeviti wa wachimbaji wadogo kila mkoa hivyo fanyeni kazi kwa karibu na hao viongozi wa wachimbaji wadogo ili kubaini changamoto zao na kutatua migogoro inayojitokeza.

Aidha, Profesa Kikula alitoa wito kwa wachimbaji wadogo pamoja na Wakuu wa Wilaya kusoma marekebisho ya sheria ya madini ya mwaka  2017 na kuielewa ili kuwa na uelewa wa uendeshaji wa shughuli za uchimbaji na biashara ya madini.

Akizungumzia lengo la ziara hiyo, Profesa Kikula alisema kuwa ni pamoja na kuangalia usalama wa wachimbaji wadogo, kufuatilia na kujiridhisha na utuzwaji wa kumbukumbu za mapato na tozo mbalimbali, kujiridhisha endapo wachimbaji wanazingatia uchimbaji salama bila kuathiri mazingira pamoja na kufuatilia endapo wachimbaji wanajishughulisha na masuala ya kijamii kama vile kujenga shule, zahanati.

Kwa upande wake Kamishna wa Tume ya madini, Abudulkarim Mruma amewasihi Wakuu wa Wilaya kufatilia taarifa za wachimbaji wadogo ili kujua leseni ya eneo husika inamilikiwa na nani na je ameajiri watumishi wangapi jambo litakalosaidia katika kupunguza na kutatua migogoro itakayojitokeza kwa wakati.

Muonekano wa madini ya Jasi yakiwa yanawekwa pembeni mwa barabara ikiwa pia ni mali ya Yusufu Kibila mgodi wa General Business and Equipment Suppliers ltd

Akizungumzia umuhimu wa utunzwaji wa kumbukumbu kwa wachimbaji wadogo,  Dkt.Athenas Macheyeki Kamishna wa Tume ya madini aliwasisitiza  Wakuu wa Wilaya kuhakikisha kuwa wachimbaji wadogo wanatuza kumbukumbu za uzalishaji na uuzaji ili kujua kiasi sahihi cha uzalishaji na kilichouzwa ili kwa njia hiyo Serikali ijipatie mapato yanayostahili.

Mkuu wa wilaya ya Manyoni, Rahabu Mwagisa alimshukuru Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Kikula kwa ujio wao

Na kuahidi kuwa watatekeleza kwa umakini mkubwa suala la kutatua migogoro maeneo ya wachimbaji  kwa kushirikiana na viongozi wa madini waliopo katika maeneo yao pamoja na viongozi wa wachimbaji wenyewe.

Aidha, aliahidi kupitia kwa upya na kuhakikisha marekebisho ya sheria ya madini ya 2017 ameielewa kikamilifu na kuifanyia kazi katika shughuli za kila siku ili kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata haki yake lakini pia serikali inajipatia mapato yake stahiki.

Mwagisa alikamilisha hotuba yake kwa kuahidi kuwa  ataendelea kusimamia na kudhibiti suala la utoroshaji wa madini na kuhakikisha kinachopatikana kinauzwa sehemu maalumu lakini baada ya kumbukumbu kuwekwa sawa na tozo stahiki zimewasilishwa ipasavyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama