Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

MKURABITA Yawezesha Wajasirimali Mkoani Njombe Kukopeshwa Zaidi ya Milioni 600 Baada Ya Kurasimisha Ardhi.

Mratibu wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) Bi. Seraphia Mgembe akizungumzia faida za mafunzo waliyopata Wajasiriamali zaidi ya 700 wa mjini Njombe yakilenga kuwajengea uwezo ili warasimishe Biashara zao na hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi ambapo wajasiriamali mkoani Njombe wameweza kukopeshwa zaidi ya milioni 600 kutoka katika Taasisi za Fedha yakiwemo Mabenki.

                      Frank Mvungi- Njombe

Zaidi ya Milioni 600 Zimekopeshwa kwa Wajasiriamali Mkoani Njombe Baada Kurasimisha Ardhi   hali iliyowawezesha kupata mitaji ya kuanzisha  Biashara hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi.

Akizungumza katika Mahojiano  maalum wakati wa mafunzo kwa wajasiriamali hao Mjini Njombe yaliyolenga kuwajengea uwezo zaidi ili kuongeza tija katika huduma na shughuli wanazofanya na hivyo kupanua wigo wa uzalishaji, Meneja wa Benki ya NMB  mkoani  humo Bw. Daniel  Zake amesema kuwa kazi inayofanywa kupitia Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara  za Wanyonge (MKURABITA) inalenga kuwainua wajasiriamali wadogo.

“ Tunatoa mikopo kwa kutumia Leseni za Makazi na hati za kimila ambazo wananchi wanapata baada ya kurasimisha maeneo yao na kupimwa na hatimaye kupata hati na katika swala hili tunapongeza Mpango wa Taifa wa  Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania  (MKURABITA)”.   Alisisitiza Bw.  Zake

Akifafanua Zake amesema kuwa Benki ya NMB imeshiriki kutoa mada  katika mafunzo yaliyoandaliwa na MKURABITA kufuatia mwaliko wa  Mpango huo kwa Benki hiyo ambapo wajasiriamali wameweza kujifunza kuhusu taratibu za kupata Mikopo, namna ya kutunza kumbukumbu katika Biashara zao.

Aliongeza kuwa wajasiriamali wanaporasimisha  Biashara zao wanapanua wigo wa Biashara zao, masoko, Ajira na pia kuiwezesha Serikali Kuongeza ukusanyaji wa Kodi na mapato ya Serikali kutokana na kukua kwa uzalishaji na shuighuli za ujasiriamali.

Kwa upande wao baadhi ya wajasiriamali walionufaika na Urasimishaji  ardhi katika Mkoa wa Njombe akiwemo  Bw.  Apolynary   Haule amesema  kuwa Urasimishaji wa Ardhi umemuwezesha kupata hati ya umiliki ardhi iliyomuwezesha kukuza uwezo wake wa kukopa kutoka shilingi laki 500,000/- hadi milioni 40,000,000/ kwa sasa baada ya kupata  hati.

“Kwa sasa Taasisi za Fedha zinatuamaini na tumeweza kukuza uwezo wetu wa kukopa kwa kuwa tunaaminika na Taasisi za fedha hali inayochea ukuaji wa uzalishaji na kupanua wigo wa Biashara katika mkoa wa Njombe”. Alisisitiza Haule

Akifafanua  amesema kuwa kwa sasa anamiliki Duka la vifaa vya ujenzi na karakana ya kuzalisha zana mbalimbali yakiwemo matoroli  viti na madirisha ya chuma.

Tunaipongeza MKURABITA kwa kutuwezesha sisi wajasiriamali wadogo kurasimisha ardhi na hivyo kupimwa hali iliyotuwezesha kupata mikopo yakukuza biashara zetu na tumetoa ajira kwa vijana hapa mjini Njombe.

MKURABITA  imewajengea uwezo wajasiriamali  mkoani Njombe ili waweze kurasimisha Biashara zao na hivyo kushiriki katika kujenga uchumi na kupanua wigo wa Serikali kuwawezesha wananchi wake kupitia Mpango wake wa kujenga uwezo kwa wajasiriamali ili waweze kurasimisha Biashara zao.

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama