Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Miundo Mipya Serikalini Kupunguza Gharama za Uendeshaji

Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Mhandisi, Balozi John Kijazi akizungumza katika Kikao Kazi cha siku tatu cha Makatibu Wakuu, Makatibu Tawala wa Mikoa na Manaibu Katiku Wakuu wa wizara kilichoanza jana tarehe 19 Septemba 2018 jijini Dodoma.(Picha na: Frank Shija – MAELEZO)

Na:Frank Mvungi- MAELEZO

Miundo mipya ya Wizara na Taasisi za Serikali Imetajwa kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za uendeshaji wa Serikali hali inayoongeza kasi ya kutoa huduma Bora kwa wananchi hasa wale wanyonge.

Akizungumza wakati wa Kikao Kazi cha Makatibu  Wakuu, Makatibu Tawala wa Mikoa na Manaibu Katibu Wakuu wa Wizara kinachofanyika Jijini Dodoma, Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Balozi John  Kijazi amesema kuwa  Serikali ya Awamu ya Tano imeazimia kujenga uchumi wa Viwanda utakaowanufaisha wananchi wote.

“ Mikutano hii itakuwa ikifanyika kila mwaka baada ya kutofanyika mwaka 2016 na mwaka 2017 kutokana  na zoezi lililokuwa linaendelea  la kupanga upya safu ya watendaji Wakuu ndani ya Serikali na Taasisi zake katika Serikali mpya ya Awamu ya Tano, pamoja na kuboresha mifumo ya uendeshaji wa Serikali” ; Alisisitiza  Balozi Mhandisi Kijazi

Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhandisi, Balozi John Kijazi(kushoto) akiteta jambo na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzabar, Dkt. Adulhamid Yahya Mzee wakati wa Kikao Kazi cha siku tatu cha Makatibu Wakuu, Makatibu Tawala wa Mikoa na Manaibu Katiku Wakuu wa wizara kilichoanza jana tarehe 19 Septemba 2018 jijini Dodoma.

Akifafanua Balozi Kijazi amesema kuwa kwakuzingatia  dhamira ya Serikali ni dhahiri kuwa lengo la kufikia uchumi wa kati litafikiwa katika muda uliopangwa.

Aliongeza kuwa Watendaji  wote Serikalini wanapaswa kusoma na kuelewa mazingira ya sasa na kutekeleza majukumu yao kulingana na mipango, maelekezo na mahitaji ya wakati huu wa Serikali ya Awamu ya Tano, na azma ya Kiongozi wetu Mkuu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Baadhi ya washiriki wa Kikao Kazi cha siku tatu cha Makatibu Wakuu, Makatibu Tawala wa Mikoa na Manaibu Katiku Wakuu wa wizara wakifuatilia hotuba ya Katibu Mkuu Kiongozi Balozi, Mhandisi John Kijazi (hayupo pichani) wakati wa kikao hicho kilichoanza jana tarehe 19 Septemba 2018 jijini Dodoma. (Picha na: Frank Shija –MAELEZO).

Pia Balozi Kijazi aliwaasa washiriki wa Kikao Kazi hicho kuepuka tabia ya kufanya kazi kwa mazoea kama ilivyozoeleka huko nyuma kwa kuzingatia sheria , Kanuni na Taratibu za Serikali ya Awamu ya Tano kwa maslahi ya wananchi.

Katika Kikao Kazi hicho mada mbalimbali zinawasilishwa ikiwemo ; Uzingatiaji wa Sheria, Kanuni na Miongozo, Matumizi ya TEHAMA Serikalini, Utawala Bora na Mapambano Dhidi ya Rushwa, Ulinzi na Usalama, Mkakati, Mwongozo na Mwelekeo kuhusu agenda ya Tanzania ya Viwanda na mifumo ya Udhibiti wa ndani Serikalini na jumuiya za Kiraia.

Kikao Kazi cha Makatibu Wakuu na Makatibu Tawala wa Mikoa kinafanyika Jijini Dodoma ikiwa ni sehemu ya mikakati ya Serikali kuimarisha utendaji wa Serikali na utoaji wa huduma bora kwa wananchi hasa wanyonge ili kutimiza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kujenga Tanzania mpya.Kikao hicho pia kimehudhuriwa na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Abdulhamid Yahya Mzee.

25 thoughts on “Miundo Mipya Serikalini Kupunguza Gharama za Uendeshaji

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama