Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Milanzi Afagilia JWTZ kwa Mchango Wake Katika Uhifadhi, Ulinzi wa Maliasili

Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi akizungumza na wanajeshi wa nchi mbalimbali za Afrika (hawapo pichani) ambao wapo nchini kujifunza mambo mbalimbali ya sekta ya utalii nchini na mchango wake kwenye uchumi na namna ambavyo jeshi linashiriki kwenye ukuaji wake.

Na Mwandishi Maalum-Dar es Salaam

JESHI la Wananchi licha ya kuwa na majukumu yake ya msingi ya ulinzi, limetajwa kuwa na mchango mkubwa kwenye utunzaji wa maliasili za nchi na uhifadhi kwa ujumla.

Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi, alipokuwa akizungumza na wanajeshi wa nchi mbalimbali Afrika, ambao wanasoma kwenye chuo cha ukamanda na unadhimu cha nchini Ghana.

Wanajeshi hao, ambao wapo nchini kwa siku saba kwa ziara ya mafunzo, walikutana na Meja Jenerali Milanzi ili kufahamu juu ya masuala mbalimbali ya sekta ya utalii nchini na mchango wake kwenye uchumi na namna ambavyo jeshi linashiriki kwenye ukuaji wake.

Akizungumza kwenye hotuba yake, Milanzi alisema sekta ya utalii pamoja na faida zake lukuki kwenye taifa lolote ikiwemo Tanzania, ina changamoto nyingi ambazo kwa namna moja au nyingine utatuzi wake unaweza kufikiwa haraka kama jeshi litashirikishwa.

“Sekta ya utalii ina changamoto kadhaa ikiwemo suala la ujangili ambalo kwa Tanzania tumejitahidi kupambana nayo kwa msaada wa majeshi yetu ambapo kwa kufanya hivyo tumefanikiwa pakubwa,” alisema.

Alitumia nafasi hiyo kuwataka wanajeshi hao kutumia ziara hiyo ya kimafunzo, kujifunza namna ya kusaidia ukuaji wa sekta ya utalii nchini mwao na Afrika kwa ujumla huku pia akiwashauri wajifunze kuhusu utangamano wa bara la Afrika.

“Nchi za Afrika ni ndugu, nimewaambia waendelee kujifunza vitu vingi kuhusu utalii wa nchi mbalimbali hasa ikizingatiwa wanyamapori hawana mipaka, kwa hivyo kama udhibiti wa ujangili utafanyika sehemu moja na nyingine pakawa hapana chochote, tatizo litaendelea kuwepo,” alifafanua.

Wakitoa shukrani kwa Wizara ya maliasili na utalii, askari hao kwa nyakati tofauti walisema wamejifunza mengi kutokana na uwasilishaji wa Katibu Mkuu Milanzi na kwamba itawasaidia kwenye kukamilisha mafunzo yao mara watakaporudi chuoni.

Kwa mujibu wa Kanali Hamza Mzee, ambaye ni mwenyeji wa ugeni huo, msafara wa askari hao unahusisha watu 16 na kwamba ni ziara ya kawaida ya mafunzo kwa askari kama wanavyofanya askari wa JWTZ, wanaosoma chuo cha ukamanda na unadhimu Duluti, Arusha.

 

41 thoughts on “Milanzi Afagilia JWTZ kwa Mchango Wake Katika Uhifadhi, Ulinzi wa Maliasili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama