Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Matumizi ya TEHAMA Kuboresha Huduma za Afya Katika Halmashauri

Mkuu wa Timu ya Mifumo ya Rasilimali Watu Dkt. Josephine Kimaro akisisitiza  umuhimu wa matumizi ya mfumo unaotoa taarifa kuhusu uhitaji wa watumishi katika kituo cha kutolea huduma (WISN) na Mfumo unaogawa watumishi kulingana na vipaumbele (POA) leo Jijini Mbeya, ambapo mafunzo hayo yatawashirikisha watumishi wa sekta hiyo  Mkoa wa Mbeya na yataendelea kwa watumishi wa sekta hiyo wa Mikoa yote Tanzania bara.

Frank Mvungi- MAELEZO, Mbeya

Mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) imetajwa kuwa chachu ya kuboreshwa kwa huduma za Afya katika Mamlaka za Serikali za Mitaa (MSM) kote nchini.

Akizungumza leo Jijini Mbeya wakati wa mafunzo ya matumizi ya mifumo ya WISN na POA kwa Watumishi wa Sekta ya Afya, Utawala, na Serikali za Mitaa, Mkuu wa Timu ya Mifumo ya Rasilimali Watu kutoka mradi wa kuimarisha mifumo ya sekta za umma (PS3) Dkt. Josephine Kimaro, amesema kuwa lengo la mifumo hiyo ni kusaidia kuboresha  huduma zinazotolewa kwa wananchi kupitia vituo vya kutolea huduma za afya.

PS3 ni mradi unaofadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID).  Mradi huu wa miaka mitano unatekelezwa katika mikoa 13 ya Tanzania bara.

Mkuu wa Timu ya Mifumo ya Rasilimali Watu Dkt. Josephine Kimaro akisisitiza  jambo kwa washiriki wa mafunzo ya matumizi  ya Mfumo unaotoa taarifa kuhusu uhitaji wa watumishi katika kituo cha kutolea huduma  (WISN ) na Mfumo unaogawa watumishi kulingana na vipaumbele (POA) leo Jijini Mbeya.

“Mifumo ya WISN na POA inatumika kubaini mahitaji ya watumishi katika vituo vya kutolea huduma za afya na vipaumbele katika maeneo husika, hivyo itasaidia kuleta mgawanyo wa watumishi kwa kuzingatia mahitaji ya kila kituo,” alisisitiza Dkt. Kimaro

Akifafanua, Dkt. Kimaro amesema kuwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa kushirikiana na mradi wa PS3 wanafanya kazi ya kuhakikisha watumishi katika sekta ya afya wanapelekwa kwenye maeneo yenye uhitaji, ili kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa kwa kuzingatia dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

Mafunzo hayo katika ngazi ya Halmashauri yanawashirikisha Waganga Wakuu wa Wilaya, Maafisa Utumishi na watumishi wengine katika kada ya afya kama Makatibu wa Afya.

Katibu wa Afya wa Jiji la Mbeya Bi. Kalunde Mbeyu (Katikati) akifurahia  Kiongozi cha Mafunzo ya Awali  kwa Watumishi Wapya wa Mamlaka za Serikali za Mitaa sekta ya afya,  wakati wa mafunzo  kwa Watumishi wa Sekta ya Afya, Utawala na Serikali za Mitaa wa Mkoa wa Mbeya ambapo mafunzo hayo yatawashirikisha watumishi wa sekta hiyo mikoa yote Tanzania Bara ili waweze kutumia mfumo wa WISN na POA kwa ufanisi , kulia ni mtaalamu wa Takwimu za afya wa Jiji la Mbeya Bi. Claudia Kaluli na kushoto ni Afisa Afya wa Jiji hilo Bw. Johnson  Ndaro.

Sehemu ya washiriki wa mafunzo ya Mfumo unaotoa taarifa kuhusu uhitaji wa watumishi katika kituo cha kutolea huduma  (WISN ) na Mfumo unaogawa watumishi kulingana na vipaumbele (POA) wakifuatilia namna mfumo huo unavyofanya kazi  leo Jijini Mbeya.

Aidha, mafunzo hayo yanayoendelea mkoani Mbeya yameanza kwa kushirikisha Mkoa wa Mbeya na kufuatiwa na Mikoa ya Katavi na Songwe. Pia, mafunzo hayo yanaendelea katika Mikoa ya Dodoma, Iringa, Mtwara  na  Mwanza.

Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi Utawala na Rasilimali watu mkoa wa Mbeya, Bw. Marko Masaya, amesema kuwa mifumo hiyo imekuja wakati muafaka na itasaidia kurahisisha uandaaji wa mipango ya ajira kwa watumishi wapya kulingana na mahitaji, na kubainisha maeneo watakapopelekwa baada ya kuajiriwa.

“Mifumo hii inaongea, hali itakayosadia kubainisha uwiano wa majukumu kati ya mtumishi mmoja na mwingine katika vituo vya kutolea huduma, hivyo tutabaini watumishi wanatekeleza majukumu mengi zaidi kuliko inavyotakiwa ili tuweze kuongeza watumishi wengine katika eneo hilo,” alisisitiza Masaya

Akieleza zaidi amesema kuwa moja ya hatua zitakazochukuliwa ili kuhakikisha kuwa mifumo hiyo inaleta matokeo chanya, Mkoa huo utaongeza usimamizi kwa watoa huduma katika vituo vya kutolea huduma ili takwimu zinazokusanywa kupitia mifumo hiyo ziwe halisi na hivyo kusaidia katika kuimarisha huduma kwa wananchi.

Mifumo ya WISN na POA iko chini ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, pamoja na Ofisi ya Rais Utumishi, ikiwa ni moja ya hatua zinazochukuliwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kuboresha huduma za afya hapa nchini.

Mtaalamu wa mifumo ya taarifa za sekta ya Afya kutoka Wilaya ya Rungwe Bw. Melchizedeck Stephen akisisitiza jambo kwa Mkuu wa Timu ya Mifumo ya Rasilimali Watu Dkt. Josephine Kimaro kutoka Mradi wa Kuimarisha Mifumo ya Sekta ya Umma (PS3) wakati wa mafunzo ya Mfumo unaotoa taarifa kuhusu uhitaji wa watumishi katika kituo cha kutolea huduma  (WISN ) na Mfumo unaogawa watumishi kulingana na vipaumbele (POA)  leo Jijini Mbeya.

 

(Picha zote na Frank Mvungi – MAELEZO, Mbeya)

43 thoughts on “Matumizi ya TEHAMA Kuboresha Huduma za Afya Katika Halmashauri

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama