Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Mapinduzi ya Matumizi ya Tehama na Mitandao ya Kijamii Yatakavyowasaidia Vijana

 

Baadhi ya aina za mitandao ya kijamii

Na. Immaculate Makilika na Bushiri Matenda.

Kumekuwepo na tafsiri mbalimbali kuhusu  maana ya Tekinolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambapo wengine husema ni aina ya tovuti au aplikesheni inayowaruhusu watumiaji kuwasiliana  kwa kuchapisha au kutumiana jumbe za maandishi, picha,video kwa kutumia kompyuta au simu za mkononi zenye huduma ya intaneti.

Kwa hali hiyo Tekinolojia ya Habari na Mawasiliano  imezalisha mitandao ya kijamii ambayo inatoa fursa ya watu kuweza kujadiliana kuhusu masuala ya siasa, uchumi, afya, biashara na mambo kadha  wa kadha ya kijamii. Fursa hiyo inaruhusu mawasiliano baina ya mtu au watu kutoka maeneo mbalimbali duniani.

Tanzania inakisiwa kuwa na watumiaji wa  huduma za intaneti zaidi ya milioni 20, wengi wao wakiwa vijana hasa wanaoishi maeneo ya mijini.

Hii ina maana kuwa kundi kubwa la vijana wa kitanzania wana fursa ya kutumia mitandao ya kijamii katika kufanya shughuli mbalimbali ambazo zinaweza kuwaletea faida faida katika maisha yao ya kila siku pamoja na kukuza uchumi wa Taifa.

Mmoja wa watumiaji wa simu za kisasa zenye uwezo wa kutumia mitandao ya kijamii.

Hivi karibuni ulifanyika mkutano wa siku moja jijini Dar es Salaam kuhusu mitandao ya kijamii ambao uliwashirikisha wajumbe kutoka Tanzania na China ambapo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame  Mbarawa  alisema kuwa maendeleo makubwa katika TEHAMA na kuwepo kwa simu za mkononi kumesababisha kuzaliwa kwa ‘Taifa la mitandao’

“ Wananchi wengi wanaotumia simu za mkononi wanaweza kupata habari kirahisi kutoka katika vyombo mbalimbali vya habari, iwe radio, mitandao ya kijamii, majukwaa ya habari na hata televisheni” alisema Profesa Mbarawa.

Aliendelea kusema kuwa serikali inaendelea kufanya  jitihada za kujenga miundombinu na kuweka mazingira wezeshi ili watanzania wengi waweze kutumia mitandao kujifunza na kushiriki katika mijadala itakayowasaidia kuwaongezea ujuzi na maarifa ili kuinua kiwango chao cha maisha katika nyanja mbalimbali.

Anabainisha kuwa pamoja na kufanya uwekezaji mkubwa katika kujenga mkongo wa Taifa wa mawasiliano, serikali pia imekuwa ikichukua hatua mbali mbali kuhakikisha kuwa mitandao iko salama.

“Serikali yetu inaendelea kuchukua hatua za kutekeleza mpango wake wa kuimarisha upatikanaji wa intaneti na usafirishaji wa data ikiwemo kuanzisha vituo vya data (data centres) ambapo kituo cha Dar es Salaam kimekwisha anza kufanya kazi”alisema Waziri Mbarawa..

Kutokana na matumizi makubwa ya simu za mikononi nchini Tanzania ambapo inakisiwa kuwa zaidi ya watu milioni 39, wanatumia simu hizi huku zaidi ya milioni 20 wakiwa ni  vijana ambao hutumia intaneti.

Serikali imekuwa ikichukua hatua stahiki kuhakikisha usalama wa mitandao hiyo ili kuepuka madhara ya kutumika vibaya.

Hii ni ishara kwamba serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa vijana ili kuweza kutumia mitandao ya kijamii katika kujiletea maendeleo yao na taifa kwa ujumla kama ambavyo wananchi wa China hasa wa vijijini  wamekuwa watumiaji wazuri wa mitandao hiyo kwa matumizi mbalimbali yenye manufaa kwao.

Majukwaa haya ya TEHAMA yanaweza kutumika kama fursa kwa kushirikishana ujuzi na kujifunza mambo mbalimbali kama vile kufanya biashara, kilimo,uvuvi, useremala ikiwa ikiwa ni pamoja na kujifunza masuala mbali mbali kutoka katika kila kona ya dunia.

Pamoja na kuwepo kwa matumizi ya mitandao yenye tija kwa vijana pia kumekuwepo na matumizi yasiyo na tija ambapo tumeshuhudia baadhi yao  wakitumia mitandao hiyo kama vile  Facebook, Instagram, Twitter vibaya.

Halikadhalika inaonekana kuwa  wanafunzi wa shule za sekondari na vyuo nchini wameendelea kutumia mitandao ya kijamii kwa kutafuta habari za wasanii na watu maarufu duniani  kuliko kutafuta taarifa zinazohusiana na masomo ama masuala mbalimbali ya kujiongezea elimu hasa ikizingatiwa kuwa wao ni vijana wasomi wa taifa hili.

Licha ya kuwa vijana wanatumia gharama kubwa za fedha kwa ajili ya kununua vifurushi katika mitandao ya simu, lakini pia wanapoteza muda mwingi ambao wangeweza kutumia katika masomo yao.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Steven Ngonyani anatoa  wito kwa wananchi  na hasa vijana kutotumia vibaya mitandao ya kijamii badala yake waitumie kujiletea maendeleo, huku akisisitiza kuwa  Kituo cha Data kilichopo Jijini Dar es Salaam ni  kituo muhimu katika kudhibiti mawasiliano yetu kama nchi.

“ Vijana wengi tunaona wakitumia mitandao ya kijamii kutazama mambo yasiyokuwa na maadili na kupoteza muda wao, hali inayowazuia kuzingatia masomo yao au kufanya shughuli za kujiongezea kipato” anasema  Naibu Waziri Ngonyani.

Aliongeza kusema kuwa serikali kwa kutambua umuhimu wa mawasiliano ipo katika mchakato wa kuanzisha vituo vingine vya kuhifadhi kumbukumbu  Zanzibar na Dodoma ambapo ni makao makuu ya nchi.

Mwanafunzi wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma katika Chuo kikuu cha Dar es salaam,(SJMC) Agness Moshi anasema anatumia mitandao ya kijamii kwa kupata taarifa za matukio mbalimbali yanayoendelea ndani na nje ya nchi, kubadilishana mawazao na watu mbalimbali ulimwenguni pamoja na kujiburudisha.

Aidha, Agness anasema vijana walio wengi hasa wasio na elimu wanatumia mitandao ya kijamii kutumiana jumbe, kufuatilia habari za watu maarufu, kutoleana lugha za matusi pamoja na kushiriki kusambaza taarifa, picha ama video za uchochezi.

Baadhi ya aina ya simu za kisasa ambazo vijana wanaweza kutumia kupata taarifa mbalimbali.

“Hivi sasa watu wengi wamefikia hatua ya kutumia mitandao ya kijamii kwa kutuma picha ama habari za matukio ya ajali ama majeruhi bila uthibitisho wa daktari ama mamlaka husika”, anasema Agness.

Ahmed Hassan, ambaye ni mfanyabiashara wa simu Jijini Dar es salaam, anasema mitandao ya kijamii imeweza kumsaidia kuongeza idadi ya wateja kutokana na kutangaza  biashara yake katika mtandao wa Instagram.

“Hapo awali sikuwa natumia mitandao ya kijamii, badala yake nilikuwa nikimfuata  mteja pale alipo,  na hivyo nilitumia muda na fedha nyingi kumfikia mteja na  nilikuwa nauza simu tatu kwa siku, lakini baada ya kujiunga na mtandao huo nimepata mafanikio makubwa, ambapo sasa nauza zaidi ya simu nane kwa siku” anasema Hassan.

Faida ya matumizi ya mitandao ya kijamii inadhihirika si tu kwa wafanyabiashara na vijana lakini pia katika Wizara, Taasisi na Mashirika mbalimbali nchini ambapo wahusika wanatumia mitandao ya kijamii kuimarisha, kurahisha na kuwezesha mawasiliano kwa kutumia barua pepe, ama kuwa na  tovuti katika mitandao hiyo.

Aidha mitandao hiyo imesaidia kwa kiasi kikubwa katika suala zima za kufanya miamala ya fedha kwa sababu kwa sasa hakuna mtu anayelazimika kutembea na kiasi kikubwa cha fedha badala yake mitandao hii inatumika katika kutuma na kupokea fedha kwa usalama na urahisi. Hii imesaidia katika kuokoa muda kwa wahusika na hivyo kupata nafasi ya kufanya shughuli nyingine za maendeleo.

Matumizi ya TEHAMA na mitandao ya kijamii kwa ujumla yamewezesha wana taaluma kwa  wanafunzi  kutuma taarifa zao, kuwasiliana pia kuwa na jukwaa muhimu la majadiliano baina yao kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii.

Aidha, Makamu Waziri wa Habari na Masuala ya Mitandao wa Jamhuri ya Watu wa China   Ren  Xianling  anawaomba Watanzania  hasa vijana na Watu wa China kuwa na matumizi sahihi ya   mitandao ya kijamii kama kichocheo cha maendeleo na  mahusiano yenye kuleta manufaa kwa pande zote mbili.

“Ni jambo lililozoeleka kufikiria kwa jinsi gani vyombo vya habari vikiwemo  mitandao ya kijamii vinaweza kutumiwa kusaidia nchi zote mbili kuimarisha mahusiano na kukuza pato la mtu mmoja mmoja na uchumi wa Taifa kwa ujumla” anasema Makamu Waziri Xianling.

Vijana wa kitanzania na jamii kwa ujumla wanatakiwa kufanya mapinduzi ya  matumizi ya TEHAMA hasa mitandao ya kijamii  ili iweze kuwaletea manufaa na maendeleo katika shughuli zao za kila siku kama  kilimo, biashara, siasa na uchumi.

Mapinduzi ya matumizi ya TEHAMA hasa mitandao ya kijamii kwa vijana yanalenga kuzalisha vijana wabunifu wa masuala ya TEHAMA ambao  watatengeneza  mifumo ya kimtandao ama maunzi laini (Applications) zitakazowezesha jamii kupata na kutumia katika  huduma mbalimbali,  mfano   mfumo wa mtandao wa Maxmalipo umewezesha jamii kufanya malipo ya huduma za kijamii ikiwemo maji na umeme bila mteja kwenda kwenye kituo cha huduma husika hivyo kuokoa muda na kutatua dharura.

Halikadhalika, serikali inaweza kutumia fursa hiyo ya mitandao ya kijamii  kwa kuchochea maendeleo kwa wananchi, kwa kuweka mazingira wezeshi na rafiki kwa vijana kuwa wabunifu na kufanya matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii.

Mitandao ya kijamii ilianza kutumika nchini mwanzoni mwa miaka ya 2000, ambapo inatumika kwa kiasi kikubwa katika kuwasiliana, kubadilishana ujuzi na kutumika katika miamala mbalimbali ya fedha. Mitandao hii imebadilisha kwa kiasi kikubwa maisha ya watu katika nyanja mbalimbali mfano kitaaluma, biashara na mawasiliano.

 

 

One thought on “Mapinduzi ya Matumizi ya Tehama na Mitandao ya Kijamii Yatakavyowasaidia Vijana

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama