Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Majaliwa Apiga Marufuku Usafirishaji wa Mazao ya Kilimo Nje ya Nchi.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akitoa Salamu za Serekali katika Baraza la Eid iliyo fanyika kitaifa katika Msikiti wa Masjidi Riadha Mjini Moshi June 26, 2017 Mkoani Kilimanjaro.(Picha na: Ofisi ya Waziri Mkuu)

Na. Ally Shaban – RS – Kilimanjaro.

Serikali imepiga marufuku uuzaji na usafirishaji wa mazao ya nafaka  nje ya nchi bila kuwa na kibali maalum,  na kuagiza kamati za mikoa kusimamia kikamilifu agizo hilo .

Marufuku hiyo imetolewa leo na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa alipokuwa akiwahutubia waumini wa dini ya Kiislam na wananchi kwa ujumla kwenye baraza la Eidd lililofanyika kitaifa mjini Moshi Mkoani Kilimanjaro.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa Serikali imechukua hatua hiyo ili kuliepusha taifa na upungufu wa chakula kutokana na mahitaji makubwa waliyonayo wananchi kabla ya chakula kusafirishwa kwenda nchi jirani.

“Natumia fursa hii kuwataka wakulima na wafanyabiashara wa mazao ya nafaka kujenga utamaduni wa kuomba vibali vya kusafirisha nje ya nchi bidhaa ambazo tayari zimeshaongezwa thamani ili waweze kupata faida zaidi,”Alisisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.

Akitoa mfano wa zao la mahindi Waziri Mkuu Majaliwa amefafanua kuwa ni vema wafanyabiashara wakasafirisha unga wa mahindi baadala ya kusafirisha mahindi ghafi kwani kwa kufanya hivyo wanapoteza faida katika biashara hiyo na kuhamishia nje ya nchi fursa za ajira kwa watanzani.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiteta jambo na Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally wakati wa stafutahi kwenye Ikulu ndogo ya Moshi, mara baada ya Swala ya Eid el Fitr na Baraza la Eid Kitaifa mkoani Kilimanjaro tarehe 26 Juni, 2017.

Mhe Majaliwa alitoa mfano wa maroli kumi na moja   yanayoshikiliwa na jeshi la polisi Mkoa wa Kilimanjaro kwa tuhuma za kujaribu kusafirisha mahindi nje ya nchi,  amesema iwe mwisho kwani mtu au kikundi chochote kitakachojihusisha na usafirishaji wa mazao ya nafaka nje ya nchi kinyume na sheria, mazao hayo pamoja na vyombo vya usafiri vitakavyotumika vitataifishwa.

Kuhusu vita dhidi ya dawa za kulevya Mhe. Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua na kuthamini  ushirikiano unaotolewa na Baraza Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA) pamoja na madhehebu ya dini nyingine katika kuunga mkono vita dhidi ya dawa za kulevya.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Sheikh Mkuu wa Tanzania Mufti Abubakari Zuberi alipokuwa akiwasili katika sala ya Eid iliyo fanyika kitaifa katika Msikiti wa Masjidi Riadha Mjini Moshi June 26, 2017 Mkoani Kilimanjaro (Picha na: Ofisi ya Waziri Mkuu)

Kuhusu  viashiria vya uvunjifu wa amani katika baadhi ya maeneo hapa nchini ikiwemo wilaya za Kibiti na Rufiji mkoani Pwani, Mhe. Majaliwa amesema Serikali inaendelea kuwasaka, kuwakamata na kuwapeleleza wahusika wote wa vitendo hivyo na watakapoabainika kuhusika watafikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

Awali akiwasilisha taarifa ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza hilo Sheikh Salum Abeid amesema Waislamu nchini wanaunga mkono juhudi za serikali ya Awamu ya Tano katika Vita dhidi ufisadi na ubadhirifu wa rasilimali za umma.

Sheikh Salum Abeid amesema waislamu wanatambua na kuthamini nia njema ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli za kuzirejesha mali zote za Baraza hilo zilizoporwa kinyemela na watu wachache kwa njia za kuwarubuni baadhi ya viongozi wa Baraza hilo.

Kwa upande wake Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania amewataka waislamu nchini na wananchi wote kuwa na mienendo mema ili amani iliyopo nchini iendelee kudumu.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama