Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Mahakama Kushirikiana na Serikali Kutoa Haki

Na Lydia Churi – Mahakama Sengerema

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema Mahakama itaendeleza ushirikiano uliopo kati yake na mihimili mingine ili kurahisisha suala la utoaji na upatikanaji wa haki nchini.

Akizungumza na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Sengerema ikiongozwa na mwenyekiti wake ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Jaji Mkuu alisema Mahakama inapata nguvu zaidi ya kutekeleza majukumu yake ya msingi pale inapopata ushirikiano kutoka mihimili mingine yaani Bunge na Serikali.

Alisema endapo Mihimili yote mitatu ya dola haitashirikiana ni wazi kuwa kazi ya utoaji na upatikanaji wa haki itakuwa ni ngumu. Aliongeza kuwa mihimili hii imewekewa utaratibu wa kutekeleza majukumu yake pasipo kuingiliana.

Aidha, Prof. Juma aliipongeza Mahakama ya wilaya ya Sengerema pamoja na Ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Sengerema kwa kuwa na uhusiano wa karibu na ushirikiano kwenye utekelezaji wa majukumu yao.

Akizungumzia kuhusu rushwa na uvunjifu wa maadili, Jaji Mkuu alisema Mahakama ya Tanzania imeamua kupiga vita rushwa na ukosefu wa maadili kwa watumishi wake ambapo pia alimtaka Mkuu wa wilaya ya Sengerema kutosita kuwaita na watumishi wa Mahakama watakaopotoka kwenye suala la rushwa na maadili.

Alisema Mahakama imeamua kutoa nakala za hukumu bure pamoja na kuingia mkataba na shirika la Posta ili kusambaza nakala hizo pamoja na nyaraka nyingine, kama hatua ya kupambana na vitendo vya rushwa.

Naye Mkuu wa wilaya ya Sengerema Bwana Emmanuel Kipole alisema mahusiano kati ya Serikali na Mahakama kwenye wilaya yake ni mazuri kwani wamekuwa wakifanya kazi kwa kushirikiana na kuheshimiana bila kuingiliana majukumu.

Mkuu huyo wa wilaya pia amemwomba Jaji Mkuu kuongeza idadi ya Mahakimu kwenye Mahakama ya wilaya kwa kuwa hivi sasa Mahakama hiyo ina hakimu  moja ambaye haendani na idadi ya mashauri yaliyopo kwenye Mahakama ya wilaya.

Aidha Mkuu huyo wa wilaya pia alisema kwa kurahisisha hudumu kwa wananchi, wilaya yake imetenga eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 24,282 kwa ajili ya kujenga Mahakama, kituo cha Polisi na Magereza.

Wakati huo huo, Ofisi ya Takukuru wilaya ya Sengerema imetoa pongezi kwa Mahakama kwa kuanzisha program maalum ya kuelimisha Umma kila siku ya Alhamis kuhusu taratibu za Mahakama kwani program hiyo imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza malalamiko ya rushwa wilayani humo.

Jaji Mkuu anaendelea na ziara ya kikazi mkoani Mwanza ambapo leo alitembelea Mahakama ya wilaya ya Sengerema pamoja na Mahakama za Mwanzo za Sima, Busisi, Buyagi na Mahakama ya Mwanzo Sengerema mjini. Jaji Mkuu pia alimtembelea Mkuu wa wilaya ya Sengerema.

79 thoughts on “Mahakama Kushirikiana na Serikali Kutoa Haki

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama