Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Magufuli: Ikulu ni Kazi Tu Sikuja Kutafuta Mchumba

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akionyesha flash ambayo inataarifa muhimu kuhusu biashara ya madini ya Almasi na Tanzanite alipokuwa akizungumza katika hafla ya kukabidhiwa ripoti ya Kamati Maalum za Bunge zilizoundwa kuchunguza mwenendo ya biashara hizo leo Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Na: Mwandishi Wetu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo amepokea ripoti mbili za Kamati Maalum za Bunge za Uchunguzi wa madini ya Tanzanite na Almasi na kusisitiza kuwa yeye yupo Ikulu kufanya kazi wala si kutafuta mchumba.

“Watanzania tumechezewa kwa miaka 50, sasa ni wakati wa kufanya kazi; lazima tuamke tukatae kuibiwa huku tunakoimbiwa sasa kama kwamba tumerogwa” alisema Dkt. Magufuli mara baada ya kukabidhiwa ripoti hizo.

Aliwaambia  viongozi na wananchi waliokuwa wakifuatilia tukio hilo kupitia vituo vya televisheni, redio na mitandao ya kijamii kuwa Ikulu ni sehemu ya kupita na yuko radhi aonekane mwanasiasa mkorofi asiyependwa lakini lazima atatekeleza jukumu lake la kutetea na kulinda rasilimali za taifa kwa manufaa watanzania wote wa leo, kesho na mtondogoo.

Alibanisha kuwa fedha zinazoibiwa kwa matrilioni zingetosha kubadili maisha ya watanzania wengi kwa kuwapatia huduma za jamii na hata kulipana mishahara mikubwa hivyo akiwa Rais hawezi kukubali hilo liendelee.

“Tuangalie maisha yetu yalivyo kila mmoja amuangalie jirani yake anavyoishi maisha ya shida huku rasilimali zote zikiibiwa na watu wakituacha katika umasikini”alieleza Rais Magufuli na kuongeza kuwa wanyonyaji hao hawana huruma kabisa na watanzania.

Akionesha kuchukizwa na matokeo ya ripoti hizo, Rais Mafuguli alisema kama baadhi iliyoelezwa kuwa udhaifu huo unatokana na mfumo basi huo mfumo lazima ufumuliwe.

“Unaposaini mikataba ya aina hii na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu inahusika basi kama ni mfumo tuufue ili tufikie mahala maslahi yetu ya nchi yapewe kipaumbele” alisisistiza Rais Magufuli na kuongeza kuwa “Tukienda kwa utaratibu huu, tutakuwa watumwa milele”

Katika hotuba yake hiyo, Rais alisema mambo mengine ni aibu kuyasema na kusisitiza kuwa yeye hataki baada ya kumaliza muda wake kuwa miongoni mwa wale wanaotajwa kuwa “Nae alikuwepo hapa“

Alisema yeye binafsi angependa kuona watanzania wanakuwa matajiri kutokana na rasilimali zao si kuwanufaisha watu wa nje na makuwadi wao wa ndani ambao aliwaeleza kuwa watu waliokosa uzalendo.

Alizipongeza ripoti hizo kuwa zimekidhi matarajio yake na kwamba zimempunguzia kazi ya kutafuta wataalamu wengine kuchunguza jambo hilo na kulipongeza Bunge kwa kutimiza wajibu wake huo vyema.

Katika mnasaba huo alimuagiza Waziri Mkuu kuwaita wataalamu wa sheria washirikiane na Bunge kukaa pamoja na kufanya marekebisho ya sheria.

“Tusiulizwe kwa nini tunabadili sheria hivi sasa kwani jibu ni wazi kuwa huu ndio wakati unaofaa kufanya hivyo” alisisitiza Rais Magufuli.

Katika mkutano huo alivipongeza vyombo vya habari kwa kazi nzuri wanayoifanya kuhabarisha wananchi na akatoa wito kwa vyombo hivyo kuendelea kuelimisha wananchi wajitambue na kuwa wazalendo.

31 thoughts on “Magufuli: Ikulu ni Kazi Tu Sikuja Kutafuta Mchumba

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama