Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Kampuni ya TGDC Yafanya Semina kwa Wabunge wa Kamati ya Nishati na Madini Mjini Dodoma.

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani akifungua Semina ya Kuwajengea Uwezo Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini jijini Dodoma hivi karibuni. Wengine katika Picha ni Viongozi Waandamizi kutoka Wizara ya Nishati na Madini na Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC).

Na Rhoda James.

Imeelezwa kuwa Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC) itazalisha Megawati 200-600 kutokana na Jotoardhi ifikapo 2025.

Kauli hiyo imetolewa mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dkt. Medard Kalemani katika Semina ya siku moja ya kuwajengea uwezo Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

Dkt. Kalemani ameielezea Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Nishati na Madini kuwa TGDC ina jukumu la kuendeleza nishati ya Jotoardhi kwa niaba ya Serikali ya Tanzania ili kukuza uchumi na kuongeza ajira.

Baadhi ya Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wakiwa katika Semina ya siku moja jijini Dodoma.

Aliongeza kuwa, Tanzania ina reserve ya Jotoardhi inayokadiliwa kuzidi Megawati 5,000 na inapatikana maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na Mbeya, Songwe, Rukwa, Dodoma, Singida, Shinyanga, Morogoro, Pwani, Mara, Kagera na Arusha.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC), Mhandisi Kato Kabaka ameieleza Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini kuwa, Kampuni ya TGDC ina majukumu mengi likiwemo jukumu la kuendelea kuhimiza matumizi mengine ya nishati ya Jotoardhi (direct heat use).

Aliongeza kuwa TGDC itaanza kuzalisha megawati 30 ifikapo 2018 kutoka Mradi wa Ngozi ambapo utafiti umefanyika kwa kiasi kikubwa.

Baadhi ya Viongozi Waandamizi kutoka Wizara ya Nishati na Madini na Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC) wakiwa katika Semina ya siku moja ya kuwajengea Uwezo Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

Mhandisi Kabaka ameelezea upatikanaji wa jotoardhi ambao unatokana na mchakato wa kinyukilia ndani ya tufe la dunia, ambalo ni endelevu na mchakato huu hutokea kwenye nyufa zilizopo kwenye gamba la dunia.

Aidha, ameeleza kuwa tofauti na upatikanaji wa nishati ya umeme, jotoardhi inajumuisha vitu vingi ikiwa ni pamoja na gesi ya Carbon oxide, sulphur na madini mbalimbali ambayo hutumika viwandani na manyumbani.

“Jotoardhi hutumika katika ukaushaji mazao ya kilimo, uzalishaji wa mbogamboga, ufugaji wa samaki, utalii wa kibiashara, mabwawa ya kuogelea na usambazaji wa Joto kwenye Nyuma,” Alisema Mhadisi Kabaka.

Pia, Mhandisi Kabaka alisema kuwa uzalishaji wa Jotoardhi ni rafiki kwa mazingira ukilinganisha na vyanzo vingine vya nishati ya umeme.

Kutoka kushoto ni Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani, Kaimu Katibu Mkuu wa Nishati na Madini Profesa James Mdoe, Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC), Mhandisi Kato Kabaka na Kaimu Kamishna wa Nishati na Masuala ya Petroli, Mhandisi Innocent Luoga. Wengine katika picha ni Viongozi Waandamizi kutoka Wizara ya Nishati na Madini na Kampuni ya TGDC.

Mara baada ya Semina hiyo Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na Mbuge wa Ludewa, Deo Ngalawa amesema kuwa anaishukuru Wizara ya Nishati na Madini kupitia Kampuni ya TGDC kwa kuwajengea uwezo katika nishati ya Jotoardhi na kufahamu faida za nishati hiyo nchini.

Aliongeza kuwa ipo haja ya Kampuni ya TGDC kuwa na Sheria ambayo itasaidia katika Uendelezaji wa Jotoardhi na kuagiza Wizara, sasa kuhakikisha kuwa TGDC hailipia leseni ya utafiti ili kufanikisha zoezi la upatikanaji wa nishati hiyo.

Jotoardhi inazalishwa katika nchi zaidi ya 26 duniani na zaidi ya Gigawati 12.6 zilipatika mwaka 2015, na zaidi ya nchi 90 zina maeneo yenye rasilimali ya jotoardhi.

67 thoughts on “Kampuni ya TGDC Yafanya Semina kwa Wabunge wa Kamati ya Nishati na Madini Mjini Dodoma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama