Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

JPM Azindua Mradi wa Kuunganisha Matrekta ya URSUS.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli (wa tano kulia) akikata utepe unaoashiria uzinduzi wa mradi wa matrekta ya URSUS SA unaosimamiwa na Shirika la Taifa la Maendeleo la Taifa (NDC) 21 Juni, 2017 katika eneo la TAMCO lililopo Kibaha, Mkoani Pwani.

Na. Benedict Liwenga-WHUSM.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amelipongeza Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) kwa ufanisi mkubwa walioufanya wa kuanza kuunganisha matrekta aina ya URSUS ambayo vifaa vyake hutengenezwa nchini Poland.

Pongezi hizo amezitoa leo Wilayani Kibaha Mkoani Pwani wakati akizindua mradi wa matrekta hayo pamoja na uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa Kiwanda cha Kuunganisha matrekta katika eneo la TAMCO, ambapo baadhi ya mambo aliyoyaongea ni kuutetea mradi huo ili ulete maendeleo kwa Watanzania.

Rais Magufuli ameeleza kuwa muda mwingi miradi ya NDC imekuwa ikikwama lakini amefurahishwa na suala la uunganishaji matrekta na kuona kuwa sasa shirika hilo limekuwa jipya huku akiwataka watendaji wa shirika hilo kuchapa kazi kwa bidii ili.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiwasha moja ya matrekta mara baada ya kuzindua ya mradi wa matrekta ya URSUS SA unaosimamiwa na Shirika la Taifa la Maendeleo la Taifa (NDC) 21 Juni, 2017 katika eneo la TAMCO lililopo Kibaha, Mkoani Pwani.

“Sasa naiona NDC hii mpya, nawapongeza, naomba sasa msinirudishie mawazo yale mabaya niliyokuwa nawazia kuhusu NDC. Sasa yale mawazo nayabadilisha, kwa hiyo tuwe na NDC mpya yenye kutoa matunda. Anzeni sasa kubadilika na muwe Shirika kweli la Taifa”, alisema Dkt. Magufuli.

Sambamba na hayo, Rais Magufuli amewapongeza Marais Wastaafu, Mhe. Benjamini William Mkapa pamoja na Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete huku akilitaka shirika hilo kuendelea na mipango mingine ya baadaye ikiwemo ya kuunganisha magari makubwa yakiwemo mabasi ili kukuza maendeleo ya viwanda nchini na kutengeneza ajira kwa Watanzania.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiwa (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Kampuni ya Matrekta ya URSUS SA pamoja na Viongozi mbalimbali wa Serikali ya Tanzania mara baada ya kuzindua ya mradi wa matrekta ya URSUS SA unaosimamiwa na Shirika la Taifa la Maendeleo la Taifa (NDC) 21 Juni, 2017 katika eneo la TAMCO lililopo Kibaha, Mkoani Pwani.

Kuhusu madai yanayodaiwa na Kampuni ya URSUS ya nchini Poland, Rais Magufuli ameitoa wasiwasi kampuni hiyo kwamba madai hayo atayamaliza katika utawala wake na kuwataka waendelee na awamu ya pili ya uunganishaji wa matrekta hayo.

“Huu mradi mimi nimeshaubeba kikamilifu na wala hautakwama, na hii nataka niwaeleze ukweli tu, labda nyie ndo muukwamishe, kwahiyo haya matrekta yatasaidia katika kilimo”, alisema Dkt. Magufuli.

Amesema kwamba, kuanza kutumika kwa matrekta hayo kutaisaidia sekta ya kilimo nchini kusonga mbele kwani asilimia 80 ya Watanzania wanategemea kilimo lakini kimekuwa hakiendi kwa haraka kutokana na matumizi ya jembe la mkono, hivyo matumizi ya matrekta yataondoa adha hiyo kwa wakulima na kuleta ajira yenye manufaa nchini.

Aidha, Rais Magufuli amewataka Wizara ya Kilimo na wawekezaji wa Kampuni hiyo ya URSUS kuangalia suala la bei za matrekta hayo ziwe nafuu ili kuwawezesha wakulima kumudu bei na pia waruhusu kuyauza kwa mkopo utakaolipwa kidogo kidogo.

Kuhusu suala la Kodi, amesema kwamba Serikali imetoa utitili wa kodi ambapo tayari kodi na tozo zipatazo 80 katika kilimo zimeondolewa lengo likiwa kuwavutia watu kuthamini kilimo.

“Suala la pembejeo katika nchi hii ni hovyo, tumeanza kufuatilia na tumebaini kuwa kuna pembejeo hewa nyingi, lakini hili tunalishughulikia na tayari kuna watu wanalifanyia kazi”, alisema Dkt. Magufuli.

Kwa upande wake Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage amesema kuwa, Serikali sasa inaleta viwanda vya nguo na vya kuunganisha magari ambapo tayari Kampuni ya TATA imeshakubali kufanya hilo na kwamba tayari fedha ya kutosha imetengea katika bajeti ya mwaka 2017/2018 kwa ajili ya kuweka mazingira mazuri ya viwanda.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiwa (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Watendaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) mara baada ya kuzindua ya mradi wa matrekta ya URSUS SA unaosimamiwa na NDC 21 Juni, 2017 katika eneo la TAMCO lililopo Kibaha, Mkoani Pwani.

“Naibu Balozi wa Poland amenieleza kuwa anataka kushirikiana na sisi ili katika kipindi kisichizidi miaka miwili kuwe hakuna mtu anayelima kwa jembe la mkono”, alisema Mwijage.

Naye Naibu Mwenyekiti wa Bodi ya NDC, Bw. Peter Chisawillo alisema kuwa, kiwanda hiko kitaunganisha jumla ya matrekta 2,400 ambapo kuna aina tatu za matrekta yanayounganishwa kiwandani hapo yenye uwezo wa ‘horse power’ 50, 65, 75 na 85.

Ameongeza kuwa, kiwanda hiko kinatarajia kuajiri wafanyakazi 100 na kwa kuanzia kiwanda kimeajili wafanyakazi 18 na baadhi yao wanatarajiwa kupelekwa nchini Poland kwa ajili ya kupatiwa mafunzo kuhusu masuala ya matrekta.

Mradi wa matrekta ya URSUS ni mradi kati ya Serikali ya Tanzania kupitia Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) na Serikali ya Poland, unahusisha mkopo wa riba nafuu wa Dola za Kimarekani milioni 55 kutokana na mkataba uliosainiwa mwaka 2015 nchini Poland wenye ushirikiano katika masuala ya kiuchumi ambapo Kampuni ya Utengenezaji Matrekta ya URSUS SA ya nchini humo imedhamiria kuisaidia Tanzania katika sekta ya kilimo.

(PICHA ZOTE NA BENEDICT LIWENGA-WHUSM)

19 thoughts on “JPM Azindua Mradi wa Kuunganisha Matrekta ya URSUS.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama