Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Zoezi la Uwekaji Alama kwa Faru eneo la Hifadhi ya Ngorongoro Lazinduliwa
Aug 17, 2021
Na Jacquiline Mrisho

Na Kassim Nyaki-NCAA

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro amezindua zoezi la uwekaji wa alama kwa Faru katika hifadhi ya Ngorongoro kwa lengo la kuimarisha ulinzi na uhifadhi wa wanyama hao ambao ni zao kubwa la Utalii nchini

Dkt. Ndumbaro ameeleza kuwa wanyama aina ya Faru ni adimu na muhimu sana katika utalii na uhifadhi hivyo, ulinzi wao kwa kutumia teknolojia ya kisasa ni kipaumbele kuwezesha ufuatiliaji wa mienendo yao hasa wanapozunguka maeneo mbalimbali ndani ya Hifadhi.

“Faru ni zao muhimu katika utalii na uhifadhi, katika kuimarisha zao hili nawapongeza NCAA kwa hatua hii ya kushirikiana na wadau kubuni mfumo wa teknolojia ya kisasa unaosaidia kulinda na kufuatilia mienendo ya Faru hasa wanapotoka nje ya Hifadhi na kuingia kwenye mashamba ya watu” alisema Dkt. Ndumbaro.

Waziri Dkt. Ndumaro ameongeza kuwa Utalii wa Faru ni zao muhimu katika kuongeza pato la Nchi na idadi kubwa ya wageni wanaokuja Ngorongoro moja ya kivutio kikubwa kwao ni Faru hivyo teknolojia ya kuwalinda faru inasaidia kuongeza idadi yao kwa haraka zaidi.

Mkurugenzi wa Wanyamapori kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Maurus Msuha ameeleza kuwa zoezi la kuweka alama kwa Faru ni utekelezaji wa mpango wa kimataifa wa kuhakikisha kuwa maeneo yote yanayopatikana Faru yanalindwa kwa mbinu za kisasa na faru hao  kuwekewa alama za utambuzi ili kuwafuatilia mienendo yao kwa urahisi zaidi.

Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Dkt. Freddy Manongi amebainisha kuwa Hifadhi ya Ngorongoro ndio eneo pekee Tanzania na duniani kote ambako mtalii anaweza kuwaona faru weusi wakiwa katika maeneo yao ya asili. 

Ameahidi kuwa NCAA itaendelea kuhakikisha kuwa wanatumia mbinu zote za kisasa kuwalinda na kuwahifadhi Faru hao ili waweze kuishi kwa mda mrefu zaidi kama ilivyokuwa kwa Faru mkongwe zaidi ambaye alikufa katika hifadhi ya Ngorongoro mwaka 2019 akiwa na umri wa miaka 57.

Kiongozi wa mradi wa Frankfurt zoological Society, Bw. Riam Labuschagne ambao ni wadau muhimu katika miradi ya uhifadhi wa mnyama Faru nchini ameahidi kuendelea kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii kuwezesha teknolojia za kidijitali na mafunzo kwa askari wanyamapori ili kuendeleza juhudi za muda mrefu za uhifadhi ambazo matunda yake yanaonekana kutokana na ongezeko la Faru nchini kila mwaka. 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi