Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Zoezi la Utambuzi wa Mifugo Kielektroniki Mwisho Oktoba, 31
Oct 18, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Mbaraka Kambona 

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, imetoa taarifa ya ukomo wa zoezi la utambuzi wa mifugo kwa kutumia hereni za kielektroniki kuwa ni Oktoba 31, 2022 na baada ya hapo wafugaji wote ambao bado hawajatekeleza zoezi hilo kwa hiyari mpaka kufikia  Novemba 1, 2022 watakumbana na mkono wa sheria.

Taarifa hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Hezron Nonga alipokuwa akiongea na Waandishi wa Habari  jijini Dodoma Oktoba 18, 2022.

“Kwa mujibu wa Sheria ya Utambuzi, Usajili na Ufuatiliaji wa Mifugo ya Mwaka 2010 na Kanuni zake za Mwaka 2011, mifugo isiyotambuliwa haitaruhusiwa kupelekwa minadani, machinjioni au kusafirishwa na atakayekiuka atachukuliwa hatua ikiwemo ni pamoja na kutozwa faini ya Shilingi 2,000,000”, alisema

Alisema kuwa suala la utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo ni muhimu kwa ustawi na maendeleo ya Sekta ya Mifugo nchini na pia ni sharti la kisheria hivyo, kila mfugaji anawajibika kufuga mifugo iliyowekwa alama za utambuzi na kusajiliwa kwenye mfumo wa utambuzi wa taifa.

Prof. Nonga alifafanua kuwa lengo ni kuweka alama za utambuzi kwa mifugo 45,920,000 lakini mpaka kufikia Oktoba 15, 2022 ikiwa ni miezi 11 tangu zoezi hilo lianze, jumla ya mifugo 4,153,856 ambayo ni sawa na 10% ya lengo ndio imeshawekwa hereni za utambuzi.

Aliendelea kusema kuwa katika utekelezaji wa zoezi hilo, kuna changamoto kadhaa ambazo zinaweza kuwa zimechangia kuwa na asilimia ndogo ya mifugo iliyowekwa alama za utambuzi zikiwemo baadhi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa kutotenga fedha kwa ajili ya kuwezesha zoezi hilo, baadhi ya wafugaji kulalamikia bei elekezi ya Shilingi 1,750 kwa hereni za ng’ombe na punda na  Shilingi 1000 kwa mbuzi na kondoo.

Changamoto nyingine, alisema ni uelewa na mtazamo hasi wa baadhi ya wafugaji kuhusu hereni za utambuzi na ukame kwa mwezi Julai 2021 mpaka Januari, 2022 uliosababisha mifugo kuathirika.

“Mkoa wa Mbeya ndio unaoongoza kwa kuweka alama za utambuzi kwa kuwa na jumla ya mifugo 1,014,569, na  zoezi hili linaendelea nchi nzima, hivyo niziombe Idara za Mifugo kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuwa wao ni Waratibu Wakuu wa zoezi la utambuzi, kuhakikisha mifugo yote inawekwa alama za utambuzi,” alisisitiza

Aidha, aliwataka wataalamu wa mifugo katika maeneo yao kuendelea kutoa elimu na kuhamasisha zoezi la  utambuzi wa mifugo kwa wafugaji kwa kuwa ni suala endelevu kwa manufaa ya wafugaji na taifa kwa ujumla.

Prof. Nonga alisema kuwa zoezi la utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo ni muhimu kwa sababu litasaidia nchi kukabiliana na magonjwa ya milipuko, kuimarisha koosafu za mifugo, kuongeza thamani ya mifugo kwenye masoko, kuwezesha bima na mikopo kwa wafugaji, kuwezesha kupatikana kwa mifugo iliyoibiwa au kupotea na inarahisisha zoezi la sensa ya mifugo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi