Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Zoezi la Tathmini Wakazi wa Kipawa Kuanza Karibuni
Jul 08, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Serikali imewahakikishia Wakazi wa Kata ya Kipunguni, jijini Dar es Salaam kuwa itaanza zoezi la tathmini kwa wakazi wote wa maeneo hayo ndani ya wiki moja ijayo ili kupisha upanuzi wa kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere.

Akizungumza katika Mkutano wa hadhara jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete, amefafanua kuwa zoezi hilo litasaidia wakazi hao kufahamu kiasi ambacho Serikali itawalipa.

“Niwahakikishie kuwa pamoja na muda mrefu mliosubiri Serikali sikivu ya Mama Samia inatekeleza yale yote inayoahidi na sasa inaanza na zoezi la tathmini na baada ya hapo zoezi la malipo litafuata”, amesisitiza Naibu Waziri Mwakibete.

Naibu Waziri Mwakibete amewataka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) pamoja na Taasisi zinazohusika kuhakikisha inatoa elimu kabla ya zoezi la tathmini ili kupunguza malalamiko mara baada ya zoezi la tathmini kukamilika.

Naye Mbunge wa Segerea, Bona Kamoli, ameishukuru Serikali kwa kutimiza ahadi na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano wakati wa zoezi hilo ili likamilike kwa wakati.

Aidha, Bona ameisisitiza TAA kuhakikisha wanapitia nyumba zote ili kujua wahusika halisi kwa lengo la kuepuka changamoto za udanganyifu wakati wa malipo ya waathirika.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Mussa Mbura, ametoa wito kwa wananchi kuanza kuwa na taarifa zote muhimu ili kurahisisha la tathmini na kulifanya kuwa taarifa muhimu.

“Niwasihi wananchi wa kata ya Kipawa kwakuwa zoezi hili ni la muhimu na linahusisha watu wengi ni muhimu kuwa na taarifa muhimu ili kupunguza muda wa kulikamilisha’ amesisitiza Mussa.

Zoezi la tathmini ambalo litahusisha uhakiki, tathmini na uthamini wananchi wa Kipunguni jijini Dar es Salaam linatarajiwa kufanywa kwa zaidi ya watu 1,100.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi