Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema Zanzibar inahitaji wadau zaidi kuunga mkono juhudi za kuutunza, kuuhifadhi na kuuendeleza Mji Mkongwe wa Zanzibar kutokana na umuhimu wake kwa uchumi wa nchi.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo, Ikulu Zanzibar alipozungumza na ujumbe kutoka Taasisi ya “International National Trust Organization” ya Uingereza iliyomueleza mafanikio waliyoyapata katika kulifanyia ukarabati jengo la “Custom House” lililopo Forodhani maarufu jengo la Mizingani.
Amesema Mji Mkongwe mbali ya kuwa ni eneo la urithi wa dunia pia ni muhimu kwa kukuza uchumi wa Zanzibar kupitia Sekta ya Utalii kwani ni eneo linalotembelewa na wageni wengi.
Dkt. Mwinyi ameeleza kufarijika kwake na juhudi na hatua zilizochukuliwa na taasisi hiyo kwa kushirikiana na Jumuiya ya Uhifadhi wa Mji Mkongwe (JUHIMKO) kwa kulifanyia ukarabati mkubwa jengo la Mizingani.
Pia, amezisisitiza taasisi na wadau wengine kujitokeza kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuyahifadhi maeneo ya urithi kwani Mji Mkongwe una majengo mengi yanayohitaji ukarabati na kutunzwa kwa fedha na utaalamu.
Akizungumzia changamoto za mabadiliko ya Tabianchi, ikiwemo kuongezeka kwa kina cha bahari, Meneja miradi wa Taasisi ya “International National Trust Organization,” David Antony Simpson amesema ni miongoni mwa changamoto inayoikabili miji mingi ya urithi duniani iliyopo pembezoni mwa bahari kama ilivyo kwa Mji Mkongwe wa Zanzibar, na kuahidi taasisi yake kuendeleza ushirikiano na Zanzibar kuhakikisha Mji Mkongwe kubaki kwenye ramani ya dunia.
Ameeleza kuwa taasisi hiyo ina uzoefu kwa nchi 102 duniani walizozifanyia ukarabati wa miji mikongwe.
Zaidi ya paundi 80,000 sawa na takriban shilingi milioni 240 zilitumika kulifanyia ukarabati mkubwa jengo la Mizingani chini ya ufadhili wa Mfuko wa Baraza la urithi la Uingereza.
Ujumbe huo uliosheheni wataalamu wa masuala ya uhifadhi wa miji ya urithi, uliongozwa na Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrik Ramadhan Soraga ulijumuisha taasisi za uhifadhi miji ya urithi kutoka Uingereza, Jordan, Misri na Uganda.