Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

WMA Yachangia Bilioni 24.3 Mfuko Mkuu wa Serikali
Aug 16, 2023
WMA Yachangia Bilioni 24.3 Mfuko Mkuu wa Serikali
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA), Bi. Stella Kahwa akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Wakala hiyo na mwelekeo wake kwa mwaka wa fedha 2023/24.
Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO

Wakala wa Vipimo (WMA) imechangia jumla ya shilingi  24,369,081,142.89  katika Mfuko Mkuu wa Serikali ndani ya  kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2018/19 hadi 2022/2023.

Takwimu hizo zimetajwa leo katika ukumbi wa Idara ya Habari - MAELEZO,  jijini Dodoma wakati Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Vipimo Tanzania, Bi. Stella Kahwa akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Wakala hiyo na mwelekeo wake kwa mwaka wa fedha 2023/24.

"Katika kuonyesha manufaa ya kuanzishwa kwa Wakala wa Vipimo kwa lengo la kupunguza gharama za uendeshaji na kusaidia maeneo mengine ya huduma za kijamii ambayo ya umuhimu na uhitaji mkubwa,  Wakala umechangia shilingi bilioni 24,3 ndani ya miaka mitano katika Mfuko Mkuu wa Serikali", amesema Bi. Stella Kahwa.

Aidha, katika kuendelea kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa watumishi wa WMA, Wakala hiyo ina ofisi katika mikoa yote Tanzania Bara na imeainisha vituo vya muda vya uhakiki vipatavyo 5,030 kwa ajili ya kusogeza huduma ambapo Maafisa huweka vituo vya muda kwa ajili ya uhakiki.

Vilevile, Wakala wa Vipimo imeendelea kuimarisha mazingira ya utendaji kazi kwa kuboresha ofisi za wakala katika mikoa mbalimbali, kuongeza vitendea kazi na mafunzo kwa watumishi.

Aidha, Mkurugenzi Mkuu huyo ameongeza kuwa kwa sasa, Wakala wa Vipimo ina jenga jengo la ghorofa nne katika eneo la medeli  katika jiji la Dodoma ambalo  litatumika kama  Makao Makuu ya Wakala wa Vipimo. Ujenzi wa jengo hilo kwa sasa umefikia zaidi ya asilimia 65 na linatarajiwa kukamilika Disemba, 2024.

Kwa upande mwingine, Bi. Stella amesema kuwa, ili kutoa huduma isiyo na mashaka katika uhakiki wa vipimo, Wakala wa Vipimo imeendelea kununua vifaa vya kitaalam ili kuhakiki vipimo na matokeo ya upimaji huo yasiwe na mashaka katika wigo wa Viwango vinavyokubalika kimataifa.

Katika kipindi cha miaka mitano baadhi ya vifaa vya kitalaam vilivyonunuliwa na Wakala wa Vipimo ni mitambo mitatu ya kuhakikia mita za Umeme, Mtambo mmoja wa kisasa wa kuhakikia mita za maji, mitambo saidizi kumi na tano (15) ya kufanyia uhakiki wa mita na mitambo 12 ya kuhakikia mita za maji zitumikazo majumbani.

Amemalizia kwa kusema kuwa, ununuzi wa vifaa hivyo vya kitaalam umesaidia sana Wakala wa Vipimo kuongeza idadi ya vipimo vinavyohakikiwa kila mwaka ikiwemo kuingia kwenye maeneo mapya yanayohitaji huduma ya uhakiki wa vipimo

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi