Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

WMA Kuhakikisha Kilimo Kinakuza Uchumi
Aug 15, 2023
WMA Kuhakikisha Kilimo Kinakuza Uchumi
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Wakala wa Vipimo Tanzania, Bi. Stella Kahwa akizungumza na Waandishi wa Habari leo katika ukumbi wa Idara ya Habari - MAELEZO jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Wakala hiyo na mwelekeo wake kwa mwaka wa fedha 2023/24
Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO

Katika kuhakikisha Kilimo kinaendelea kuwa nguzo muhimu katika kuchochea uchumi wa nchi, Wakala wa Vipimo (WMA) imeendelea kufanya uhakiki wa vipimo vinavyotumika katika kilimo ambavyo kwa sehemu kubwa ni mizani.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Wakala wa Vipimo Tanzania, Bi. Stella Kahwa ameyasema hayo leo katika ukumbi wa Idara ya Habari - MAELEZO jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Wakala hiyo na mwelekeo wake kwa mwaka wa fedha 2023/24 ambapo ameeleza kuwa, katika mazao ya kimkakati katika kipindi cha mwaka 2022/23, Wakala ilihakiki jumla ya mizani 4,254 ambapo kati yake, ya Pamba 1,566, Korosho 2,286 na Kahawa 402 .

"Ili kuchangia katika kuleta mageuzi ya kilimo na kuwa na uhakika wa chakula utakayoiwezesha nchi kujitegemea kwa chakula wakati wote na ili kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya uchumi, matumizi ya vipimo vilivyohakikiwa kupitia Wakala wa Vipimo ni muhimu sana", alisema Bi. Stella.

Amefafanua kuwa, vipimo ndivyo vinavyotumika kwenye hatua mbalimbali za kilimo mfano kuandaa eneo la kulima ni lazima ujue ukubwa wa eneo kwa kutumia vipimo vya urefu na kujua kiasi cha mbolea itakayotumika kwa kupima kwa mzani au vipimo vya ujazo.

Ameongeza kuwa, Ili kuleta ufanisi katika zoezi hilo, Wakala hutoa elimu juu ya umuhimu wa kufanya uhakiki wa Mizani inayotarajiwa kutumika katika kufanya ununuzi wa mazao kwa kushirikiana na Vyama vya Ushirika vya Msingi, Sekretariati za Mikoa na kufuatiwa na zoezi la uhakiki na baadaye kufuatiwa na kaguzi za kustukiza wakati ununuzi wa mazao unaendelea ili kubaini watumiaji wa mizani wasiozingatia matumizi sahihi ya vipimo, taratibu na Sheria.

Wakala wa Vipimo katika utekelezaji wa majukumu yake imeendelea kutoa mchango katika kuchochea maendeleo ya sekta za kiuchumi na kijamii nchini, kuchochea uzalishaji wa bidhaa unaozingatia vipimo sahihi na kuendelea kuchangia katika mfuko mkuu wa Serikali.

Kadhalika, katika kuendelea kuboresha na kufikisha huduma bora kwa wananchi, WMA imeanza kutumia Mfumo wa Huduma za Serikali kupitia Simu za Mkononi (mGov), mfumo ambao umetengenezwa kwa lengo la kujumuisha huduma zote za simu za mkononi Serikalini.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi