Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wizara Yaendelea Kuifikia Mikoa Isiyofanya Vizuri Anwani za Makazi
Apr 27, 2022
Na Jacquiline Mrisho

  • Mkoa wa Singida Wapewa Siku Nane Kujinasua Kabla ya Uhakiki

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohammed Khamis Abdulla ametoa siku nane kuanzia tarehe 29/4/2022 hadi tarehe 05/05/2022 kwa Watendaji wa Mkoa wa Singida kusimika nguzo zenye majina ya barabara na mitaa pamoja na namba za nyumba katika halmashauri zote saba za Mkoa huo

Akizungumza katika ziara yake mkoani hapo mara baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa operesheni ya Anwani za Makazi, Naibu Katibu Mkuu amesema eneo pekee ambalo mkoa huo umefanya vizuri ni ukusanyaji wa taarifa za wakazi na makazi, na maeneo mawili yaliyosababisha wawe katika nafasi za mkiani ni kutokuweka nguzo zenye majina ya barabara na mitaa pamoja na namba za nyumba.

“Nikiangalia muda uliobaki na nilichokisikia hapa haviendi sawa, Wakurugenzi na Watendaji wa Halmashauri hakikisheni ifikapo tarehe 5 ya mwezi Mei, 2022 nguzo zenye majina ya barabara na mitaa zisimikwe na namba za nyumba ziwekwe, kuanzia tarehe 6 ya mwezi Mei, 2022 timu ya wataalamu ya Wizara itakuja kufanya uhakiki “physical verification” ya uwekaji wa miundombinu ya Anwani za Makazi katika mkoa huu”, Amezungumza Abdulla.

Ameongeza kuwa, zoezi la uwekaji wa Anwani za Makazi lisipokamilika kwa muda uliopangwa litakwamisha zoezi la Sensa ya Watu na Makazi, na akiangalia mwenendo wa uwekaji wa nguzo zenye majina ya barabara na mitaa na uwekaji wa namba za nyumba kwa halmashauri zote za Mkoa wa Singida utekelezaji wake ni  wastani wa asilimia 3 hadi 4.

“Ni aibu hata sie watekelezaji wa operesheni hii bado hatuna Anwani za Makazi, mpaka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida hauna kibao cha Anwani ya Ofisi, tuhakikishe ndani ya siku mbili hadi tatu kuanzia leo tarehe 27, Mei, 2022 ofisi zote za Serikali ndani ya Mkoa wa Singida zimewekwa Anwani za Makazi, na taarifa ya utekelezaji iwasilishwe Wizarani kupitia Meneja wa Mkoa wa Singida wa Shirika la Posta Tanzania”. Amesisitiza

Awali, taarifa za utekelezaji wa operesheni ya Anwani za Makazi katika Mkoa wa Singida ziliainisha changamoto za utekelezaji zilizojitokeza ikiwemo uhaba wa fedha ambapo Naibu Katibu Mkuu aliipangua hoja hiyo kwa kuwakumbusha kuwa Mamlaka ya juu inapotoa agizo hakuna visingizio kwenye utekelezaji.

“Muongozo upo, bajeti ni ndogo lakini ni lazima zoezi hili likamilike, ukishakusanya taarifa kwenye kuandika namba za nyumba tafuteni rangi, chaki au mkaa ili mradi namba ikiandikwa ionekane ili watu wa sensa wakija wajue hii ni nyumba namba fulani, iliyopo mtaa fulani na mwananchi atakayetaka kuweka namba yake kulingana na muongozo aruhusiwe.”

Viongozi na watendaji wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wameendelea na ziara ya kukagua utekelezaji wa operesheni ya Anwani za Makazi hasa katika mikoa ambayo haifanyi vizuri.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi