Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wizara ya Utamaduni Yajipanga Kufikia Matarajio ya Serikali
Aug 16, 2023
Wizara ya Utamaduni Yajipanga Kufikia Matarajio ya Serikali
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana akizungumza wakati akifungua Kikao cha faragha cha viongozi wa Wizara na Wakuu wa Taasisi leo mkoani Morogoro.
Na Shamimu Nyaki

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amefungua Kikao cha faragha cha viongozi wa Wizara na Wakuu wa Taasisi leo mkoani Morogoro.

Mhe. Chana ameeleza  kuwa vikao vya aina hiyo, vinatoa fursa ya kujitafakari kukumbushana namna ya kutekeleza majukumu ya Wizara na Taasisi ili kusaidia mabadiliko zaidi katika nchi.

"Natambua kuwa majukumu ya wizara kwa mujibu wa muundo ni kuhudumia wadau wa sekta tunazozisimamia ili kuhakikisha kuwa matarajio ya Serikali ya Awamu ya Sita pamoja na ya wadau wetu yanafikiwa kwa kiwango kikubwa," amesema Mhe. Chana.

Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Hamis Mwinjuma akizungumza wakati wa Kikao cha faragha cha viongozi wa Wizara na Wakuu wa Taasisi leo mkoani Morogoro.


Awali, Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Hamis Mwinjuma amesema wizara hiyo inamgusa kila mtu katika kupata burudani, ajira, uhusiano na kipato, ambapo amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye ligi bora Duniani, Wanamuziki wengi  wanaounganishwa na lugha ya Kiswahili na kwa sasa  inakamilisha maboresho katika Sera ya Utamaduni ili iendane na wakati wa sasa,

Aidha,  Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Malima amesitiza muendelezo  wa  kuutangaza Utamaduni wa Taifa ili ujulikane kwa mila, desturi na utu wetu bila kusahau sekta yetu ya michezo ambayo inaendelea kukua siku hadi siku.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Saidi Yakubu amesema 
Mkutano huo ni Utekekezaji wa maagizo ya Rais  Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa mwezi Machi, 2023 jijini Arusha wakati wa kikao cha faragha cha viongozi, na kitakua na  mada mbalimbali ikiwemo Vipaumbele na Utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2023/24, pamoja na Mabadiliko ya Taasisi.

Kikao hicho kitafanyika kwa siku tatu kuanzia Agosti 16 hadi 18, 2023 ambacho kinahudhuriwa na  Wakurugenzi, Wakuu wa Vitengo, Wakuu wa Taasisi na Wakurugenzi Wasaidizi wa Wizara hiyo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi