Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imekutana na wadau wa sekta binafsi katika mkutano wa kujadili masuala ya diaspora na ushirikishwaji wao katika maendeleo ya Taifa unaofanyika tarehe 26 na 27 Septemba, 2022 jijini Dodoma.
Akifungua mkutano huo, Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Agness Kayola ameeleza kuwa dhumuni la mkutano ni kuwakutanisha wadau kutoka katika sekta ya umma na binafsi ili wapate nafasi ya kujadili namna wanavyoweza kuongeza huduma za taasisi zao kwa diaspora ili kuleta ushirikiswaji wenye tija katika maendeleo ya Taifa.
“Mkutano huu umewakutanisha wadau wanaotoa huduma mbalimbali kwa Diaspora na wale ambao hawana huduma bado, lakini ni Wadau wanaoweza kuwa na mchango muhimu katika kuongeza ushiriki wa Diaspora wa Tanzania kwenye masuala ya maendeleo ya taifa’’, alisema Balozi Kayola.
Pia akaeleza kuwa kupitia mkutano huo, wadau watapata fursa ya kushirikishana juu ya masuala mbalimbali muhimu, kama vile fursa za uwekezaji nchini, vigezo vya kusajili Wawekezaji Wazawa na Wawekezaji Wageni, wakiwemo Diaspora wenye uraia wa nchi nyingine, fursa za uwekezaji kwa Diaspora na nini kifanyike kuongeza Uwekezaji kutoka kwa Diaspora wa Tanzania.
Naye Mkurugenzi wa Masuala ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi James Bwana ameeleza kuwa mkutano huo umezikutanisha taasisi za fedha, kampuni za simu za mikononi, taasisi za umma na binafsi za ujenzi wa nyumba za makazi kama vile Shirika la nyumba la Taifa (NHC), Hamidu City Park, KC Land na wengine.
Vilevile ameeleza kuwa, kupitia mkutano huo Serikali na wadau wa sekta binafsi wataweza kujadili namna mataifa mengine duniani yalivyofanikiwa katika eneo la ushirikishwaji wa diaspora ikiwa ni hatua ya kuboresha huduma za sekta binafsi katika kuchagiza ari na hamasa ya diaspora kuchangia katika maendeleo ya Taifa.
"Takwimu zinaonesha nchi kama China, India, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Ghana, Nigeria zilivyofanikiwa katika eneo la dispora hivyo, hatuna budi kuongeza ubunifu ili kufanikisha mikakati yetu ya kitaifa kwa kuunganisha nguvu ya diaspora na sekta binafsi", alisema Balozi Bwana.
Kwa upande wa Naibu Mkurugenzi, Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na Diaspora, Ofisi ya Rais – Ikulu, Zanzibar, Bi. Maryam Ramadhan Hamoud ameeleza kuwa mkutano huo utawafahamisha wadau kuhusiana na mchango wa Diaspora katika sekta mbalimbali hususan afya, elimu, uwekezaji na umuhimu wa Diaspora katika kuchangia maendeleo ya nchi kupitia fedha wanazotuma nyumbani (Remittances).
Mbali na hayo, Bi. Maryam aliongeza kuwa, wadau watapata fursa ya kutambua huduma mbalimbali za misaada ya kijamii, Sayansi na Ubunifu, ambayo huletwa nchini na Wafadhili kupitia uratibu wa Diaspora.
Mwaka 2010, Serikali ilianzisha Kitengo cha Diaspora chini ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ilianzishwa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na Uratibu wa Masuala ya Diaspora katika Ofisi ya Rais Ikulu – Zanzibar.
Jukumu kubwa la Ofisi hizi mbili, ni kusimamia, kuratibu na kushughulikia masuala yanayohusu Ushiriki wa Diaspora katika shughuli za maendeleo nchini.