Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Zungu awataka wawekezaji kutimza matakwa ya Sheria ya uhifadhi wa mazingira
Mar 01, 2020
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_51293" align="aligncenter" width="800"] Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu (mwenye kofia) akipata maelezo kutoka kwa Meneja Uzalishaji Hinduka Kamalamo wa kiwanda cha cha kutengeneza mifuko mbadala aina ya ‘non woven’ cha Jin Yuan Investment kilichopo Nyakato wilayani Ilemela mkoani Mwanza wakati wa ziara yake ya kikazi.[/caption]

Na Robert Hokororo, Mwanza

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu amesema wawekezaji wanapaswa kutimza matakwa ya sheria ya uhifadhi wa mazingira sambamba na kuleta maendeleo kwa Taifa.

Zungu ametoa kauli hiyo leo alipofanya ziara ya kikazi mkoani Mwanza katika viwanda vya kutengeneza mifuko mbadala aina ya non woven vya Jin Yuan Investment, CMG Pyramid na Hoteli ya Malaika katika Wilaya ya Ilemela.

Alikagua uzalishaji wa mifuko hiyo na kujionea shughuli za uhifadhi wa mazingira alisema kuwa nia ya Serikali ni kujenga urafiki na wawekezaji katika sekta ya viwanda na ndio maana imeweka masharti yasiyo magumu ili waweze kuendelea kuwekeza na hivyo maendeleo yapatikane.

“Viwanda vinachangia ajira na pato la ndani kwa kulipa kodi lakini vinapaswa kuzingatia matakwa ya sheria na tunasisitiza mifuko mbadala yenye ubora ambayo ni rafiki wa mazingira na pia inaongeza pato la nchi kwani wanalipa kodi.

[caption id="attachment_51294" align="aligncenter" width="800"] Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu akiangalia namna changamoto ya kimazingira iliyopo katika ufukwe wa Hoteli ya Malaika jijini Mwanza ambapo aliagiza mwekezaji huyo azishughulikie.[/caption]

“Niwapongeze kiwanda hiki kwa kuzalisha mifuko hii mbadala lakini tutachukua sample ya mifuko hii tukapime maabara kama zina standard iliyowekwa na GSM 70 na tukikuta kweli tutawapongeza zaidi maana mifuko mingi inayoingia kutoka nje inakosa ubora na hawalipi kodi na inachafua mazingira kutokana na kushindwa kurejelezeka,” alisema Zungu.

Katika hatua nyingine waziri huyo ambaye pia aliambatana na wataalamu kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Ziwa alimtaka mwekezaji wa Hoteli ya Malaika kurekebisha dosari zilizobainika.

Aliiagiza NEMC kumpa muda mwekezaji huyo ili afanye marekebisho ya mfumo wa majitaka ili kukidhi mazingira kwa wageni wanaofika hotelini hapo na Taifa kwa ujumla.

“Ni kosa kujenga ndani ya mita 60 za chanzo cha maji na yeye amejenga bila kupata cheti cha tathmini ya athari ya mazingira na matokeo yake ndio kama hivi sasa kanuni mpya zitatoka tusubiri zitasemaje lakini kwa sasa mpeni muda arekebishe,” alisisitiza Waziri Zungu.

[caption id="attachment_51295" align="aligncenter" width="800"] Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu akiwasili katika eneo la Mwaloni jijini Mwanza kwa ajili ya kutoa elimu kuhusu magugu maji na kutoa elimu ya uzingatiaji sheria ya mazingira yam waka 2004.[/caption]

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Dkt. Severine Lalika alimuhakikishia Waziri Zungu kusimamia na kuhakikisha maagizo hayo yanatekelezwa.

Dkt. Lalika aliongeza kuwa suala la kufuata sheria za nchi halina mjadala na kuwa wao kama viongozi wanao wajibu wa kuhakikisha linasimamiwa ipasavyo.

Waziri Zungu yuko katika ziara mikoa ya Kanda ya Ziwa kukagua shughuli mbalimbali za mazingira katika maeneo mbalimbali ya uwekezaji kuona kama wanafuata Sheria ya Mazingira yam waka 2004 na kutoa elimu kuhusu matumizi ya mifuko mbadala aina ya non woven inayokidhi viwango vilivyowekwa na Serikali.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi