Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Wang: China Samaki kutoka Tanzania
Jan 10, 2021
Na Msemaji Mkuu

Na  Immaculate Makilika- MAELEZO, Chato

Waziri wa Mambo ya Nje wa China,Wang Yi amesema kuwa nchi yake inakaribisha    samaki kutoka Tanzania kuuzwa moja kwa moja nchini humo ili kusaidia sekta ya   maendeleo  ya uvuvi nchini.

Akizungumza jana (Januari 8, 2021) wakati alipotembelea Mwalo wa Chato beach uliopo katika Wilaya ya Chato mkoani Geita, na kukutana na wavuvi  Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa China alisema kuwa  soko la samaki China ni kubwa na hivyo anakaribisha samaki kutoka Tanzania kuuzwa nchini kwake.

“Nimeambiwa wakati wa mvua Tanzania hali inakuwa ngumu sana na soko la samaki huko China ni kubwa. Kwa hiyo ningependa kutangaza kwamba China inakaribisha samaki kutoka Tanzania na pia tungependa kuwasaidia kuongeza mapato na kuboresha maisha yenu”.

Alisisitiza “Tunapenda kusaidia kuuza bei ya samaki watanzania kupitia mkataba husika ili mazao kutoka Ziwa Victoria yaende China kwa urahisi zaidi.”

Vilevile, Waziri Wang  alisema kuwa   Ubalozi wa China nchini  utatoa  kiasi cha dola za Marekani 20,000 kwa ajili ya kusaidia wavuvi wa mwalo wa Chato kununua vifaa vya uvuvi.

Aidha, alionesha kufurahishwa  na  zawadi ya samaki aliyopewa na wavuvui wa mwalo huo .

“ Leo nyinyi mmenizawadia samaki wazuri na wakubwa sana,  nimefurahi sana na nashukuru sana, kitendo  hili  kinaonesha  hisia zenu na urafiki wa kweli.”

Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashamba Ndakialisema  kuwa Tanzania imejaliwa rasilimali za uvuvi katika maeneo mbalimbali ya maziwa, mito na  bahari ambazo zinachangia pato  la taifa, ambapo asilimia 75 ya mazoa ya uvuvi yanayozalishwa hapa nchini yanavunwa kutoka Ziwa Victoria.

Waziri Ndaki alitaja mazao hayo matatu ya kibiashara kuwa ni samaki aina ya sangara, sato na dagaa.

“Mazao yatokanayo na samaki aina sangara yanayojumuisha minofu na mabondo ndio husafirishwa kwa wingi kwenda kwenye soko la kimataifa ikiwemo China, kwa kupitia Hong Kong. Ni lengo la serikali yetu kuuza zao hili moja kwa moja nchini China.”alisema Waziri Ndaki

Alifafanua kuwa matarajia ya Serikali ni kusaini  mkataba utakaowezesha kuuza bidhaa hizo moja kwa moja katika soko la China.

“Tunaomba mheshimiwa  Waziri Wang mara tutakapowasilisha rasmi maombi ya soko la mabondo tuungwe mkono na Serikali ya China. Tuna imani kwamba kufunguliwa kwa soko hilo kutasaidia sana jitihada za wananchi kujikwamua na umasikini” alisisitiza Waziri Ndaki.

Tanzania ina mialo 1,373 ikiwamo mwalo wa Chato licha ya Serikali kufanya  juhudi za kuendelea mialo hiyo hapa nchini bado kuna fursa ya kuboresha miundombinu ya kupokea, kuhifadhi na kuchakata mazao ya samaki.

Aidha, Waziri Ndaki aliiomba Serikali ya China kuhamasisha makampuni binafasi kutoka nchini humo kuja kuwekeza katika viwanda na miundombinu ya vuvuvi ili kuongeza uzalishaji kupunguza upotevu wa rasilimali za uvuvi na kuongeza ubora na usalama wa mazao ya uvuvi hapa nchini.

 “Zaidi ya wananchi milioni 4.5 wanajishughulisha na shughuli mbalimbali katika mialo, na sekta ya uvuvi inawapatia kipato na lishe wananchi na kuchangia pato la taifa.”alisema Waziri Ndaki

Asilimia 85 ya mazao ya uvuvi yakiwamo yale yanayosafirishwa nje ya nchi yanatokana na wavuvi wadogo wadogo ambao hutumia vyombo vidogo vya kuanzia mita tatu hadi mita 10.

Naye, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wavuvi katika mwalo wa Chato Beach, Kamese Kalima alisema mwalo  huo umeanzishwa mwaka 1999  ukiwa na wavuvi 500 na mitumbwi 125, na kati ya hiyo mitumbwi 110 ni ya makasia na mitumbwi 15 ni ya injini.

Bw. Kalima aliiomba Serikali ya China kuwasaidia kutatua changamoto za miundombinu  zinazowakabili ambazo ni vyombo vya uvuvi, jengo ambalo litajumuisha soko la uvuvi, mitambo ya kuzalisha tani 5 za barafu, chumba cha ubaridi chenye uwezo wa kuhifadhi tani 10 za samaki, na mashine ya umeme yenye uwezo wa kukaushia tani 5 za dagaa kwa siku.

 “Tunatambu China ni vinara wa viwanda vya samaki duniani, hivyo tunaomba miundombinu ya uchakataji samaki na China kuja kuwekeza viwanda vya kuchakata samaki angalau tani 35 kwa siku.” Alisema  Bw. Kalima

Mwalo wa Chato na Mkoa wa Geita kwa ujumla unazalisha zaidi ya tani 23,844  za samaki kwa mwaka ambao husafirishwa umbali mrefu kwenda viwanda vilivyopo Kagera na Mwanza kwa ajili ya kuchakata samaki.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi