Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri wa Nishati Afanya Mazungumzo na Mwakilishi wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza
Jun 24, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Teresia Mhagama

Waziri wa Nishati, Mhe.January Makamba amekutana na kufanya mazungumzo kuhusu mabadiliko ya tabianchi na Balozi wa Masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi Kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika, Janet Rogan ambaye amemwakilisha Rais wa Mkutano wa 26 wa Mabadiliko ya Tabia Nchi (COP26)  pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza.

Mkutano wa viongozi hao umefanyika jijini Dodoma tarehe 23 Juni, 2022 na kuhudhuriwa na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, David Concar,  Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali pamoja na watendaji wengine kutoka Ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania.

Majadiliano ya viongozi hao yalihusu mabadiliko ya tabianchi pamoja na  jinsi Tanzania ilivyojipanga katika kutekeleza maazimio ya Mkutano wa 26 wa Mabadiliko ya Tabia Nchi uliofanyika mwaka 2021 nchini Uingereza ambapo Tanzania ni Nchi mwanachama.

Baadhi ya maazimio ya Mkutano huo wa COP26 ni pamoja na uhamasishaji wa matumizi ya nishati mbadala, matumizi ya umeme kwenye magari pamoja na kupunguza ukataji miti.

Katika mazungumzo hayo, Waziri wa Nishati, Mhe.January Makamba, alimweleza Balozi huyo kuwa, Tanzania inafanya juhudi mbalimbali kutekeleza maazimio hayo kwa kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala mijini na vijijini pamoja na magari kutumia gesi asilia na umeme.

Aidha, alimweleza Balozi huyo juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa na nishati ya kutosha kwa kuendeleza vyanzo mbalimbali vya nishati ikiwemo  Jotoardhi, Jua na Gesi Asilia.

Pia alimweleza kuwa,  Serikali ina mpango wa kuandaa na kuboresha mikakati mbalimbali ya kisekta  pamoja na kuboresha mfumo wa Gridi ya Taifa ili kuhakikisha kuwa nchi inakuwa na nishati ya uhakika.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi