Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Silaa Asimamisha Matumizi ya Kituo cha Mafuta cha Barrel Dar es Salaam
Dec 23, 2023
Waziri Silaa Asimamisha Matumizi ya Kituo cha Mafuta cha Barrel Dar es Salaam
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Jerry Silaa akizungumza na wananchi wa Mikocheni na kusimamisha matumizi ya Kituo cha Mafuta cha Barrel Petrol Energy cha Mikocheni Desemba 23, 2023 jijini Dar es salaam.
Na Eleuteri Mangi, WANMM

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Jerry Silaa amesimamisha matumizi ya Kituo cha Mafuta cha Barrel Petrol Energy cha Mikocheni jijini Dar es salaam na kupiga marufuku ujenzi holela wa vituo vya mafuta nchi nzima vinavyojengwa kwenye makazi ya watu hatua inayohatarisha usalama wa watu na mali zao.

 

Waziri Silaa ametoa agizo hilo Desemba 23, 2023 alipoenda kukagua eneo kilipojengwa kituo hicho na aliambatana na Kamati ya Ulizi na Usalama ya Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es salaam.

 

"Kufuatia agizo hili, nawaagiza Wakuu wote wa Idara ya Ardhi na Mipango Miji nchi nzima wafanye uhakiki wa vituo vya mafuta kwa maana ya viwanja, mabadiliko ya matumizi ya ardhi, mchakato uliotumika, ukubwa wa viwanja, ukaribu wa kituo kimoja na vituo vingine na ukaribu wa maeneo mengine ya kutolea huduma za jamii, hali ya uendeshaji wa vituo hivyo, taarifa hiyo ifike ofisini Januari 31, 2024" amesema Waziri Silaa.

 

Pia Waziri Silaa amewaagiza wafanyabiashara ya mafuta nchini wafanye uhakiki wa vituo vyao na Mafuta, mchakato wa namna walivyopata ardhi wanayotumia na kuwasilisha taarifa hiyo Ofisini kwake ifikapo Januari 31, 2024.

 

Aidha, Waziri Silaa amesema ni vema watumishi wa Ardhi na wafanyabiashara hiyo waheshimu Sheria za nchi kwa vitendo kwa kuwasikiliza watu wasio na sauti ili wapate haki zao katika masuala ya ardhi.

 

"Rais Samia Suluhu Hassan ni mtu wa haki, anataka watu wapate haki, ameniteua mimi kusimamia haki, hebu tusimamie Sheria, kwa mdomo tukisema tunamuunga mkono Dkt.Samia Suluhu Hasan, lakini tufanye kwa vitendo kwa kuwasililiza wale 'the voiceless, sisi tumewekwa hapa kuwa voice of the voiceless" amesema Waziri Silaa.

 

Naye mkaazi wa eneo hilo la Mikocheni Bw. Stephen Rupia amesema wananchi wa eneo hilo hawakushirikishwa kwenye hatua yeyote ambayo ilitakiwa wananchi washirikishwe.

 

"Tupo hapa eneo hili lilikuwa na ukuta na miti mbele na lilikuwa eneo la mtu kwa matumizi yake, hatukuona bango la kubadilisha matumizi ya eneo hili kujenga kituo hiki cha mafuta" amesema Bw. Rupia.

 

Akizungumza kwa niaba ya mmiliki wa kituo hicho cha Mafuta Mhandisi Stanley Kitundu  amesema wameyapokea maelekezo ya Mhe. Waziri mwenye dhamana ya ardhi na watayatekeleza na kuongeza kuwa kituo chao kimekamilika kwa asilimia 100 lakini kilikuwa hakijaanza kufanyakazi.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi