Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Ndumbaro Aagiza BASATA na Bodi ya Filamu Kusimamia Sekta ya Sanaa Kukuza Uchumi wa Nchi
Oct 17, 2023
Waziri Ndumbaro Aagiza BASATA na Bodi ya Filamu Kusimamia Sekta ya Sanaa Kukuza Uchumi wa Nchi
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro akizungumza leo Oktoba 17, 2023 wakati wa hafla ya kukabidhi Tuzo za Hollywood and African Prestigious Awards (HAPAWards) 2023 walizoshinda Wasanii kutoka Tanzania
Na Shamimu Nyaki

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro ameliagiza Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na Bodi ya Filamu nchini kuhakikisha wanasimamia vyema Sekta ya Sanaa ili iweze kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi na kunufaisha Wasanii.

Dkt. Ndumbaro ametoa maagizo hayo Oktoba 17, 2023 wakati wa hafla ya kukabidhi Tuzo za Hollywood and African Prestigious Awards (HAPAWards) 2023 walizoshinda Wasanii kutoka Tanzania, Jacob Steven aliyeshinda kipengele  cha Best Bongo Movie Actor na Saraphina Michael ( Phina) aliyeshinda kipengele cha Best  Female in Bongo Fleva East Africa zilizofanyika hivi karibuni nchini Marekani.



"Rais Dkt. Samia ameendelea kafanya juhudi ili Sekta hii ikue, hivi karibuni katika ziara yake nchini India ameshuhudia Utiaji Saini wa Mkataba wa Ushirikiano kati ya Tanzania na India katika Sekta ya Utamaduni na Sanaa, na tayari tumepokea maombi ya ushirikiano na Uturuki na Urusi. Hivyo jukumu letu ni kuhakikisha Wasanii wetu wanatengeneza kazi zitakazoleta ushindani duniani" amesema Dkt. Ndumbaro.

Ameiagiza Ofisi ya Hakimiliki nchini (COSOSTA) ihakikishe inasimamia Sheria ya CMO'S kikamilifu ili Wasanii wanufaike na kazi zao, huku akiwaagiza Wasanii kutengeneza kazi zenye ubora zinazotangaza utamaduni na lugha ya Kiswahili.



Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa BASATA, Dkt. Kedmon Mapana amesema Tuzo hizo zimeanzishwa na Mtanzania anayeishi Marekani Mawinny Casey  ambapo hadi sasa zimefanyika kwa miaka Saba mfululizo zikijikita katika Burudani na Filamu.

Naye Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu, Dkt. Kiagho Kilonzo ameeleza kuwa katika ziara yao nchini Marekani pamoja na kupokea Tuzo za Wasanii hao pia walishiriki Majukwaa mbalimbali ya biashara, kukutana na wawekezaji wa Sekta hizo na kukubaliana kushirikiana katika kuanzisha Shule ya Filamu,  uzalishaji na usambazaji wa filamu, kazi za kitamaduni pamoja na ujenzi wa jumba changamani la Filamu.



Wasanii wengine  kutoka Tanzania ambao waliwahi kushinda Tuzo hizo ni Wema Sepetu na Lady Jaydee ambao Tuzo zao zimeshafika nchini tayari kwa kukabidhiwa.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi