Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Nape Atoa Maelekezo kwa TCRA, Makampuni ya Simu
Jun 01, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Mwandishi wetu, DODOMA

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye ametoa maelekezo kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na makampuni ya simu kutatua kero na malalamiko ya wananchi kuhusu huduma za mawasiliano pamoja na kuangalia namna ya kuwawezesha watanzania kuongeza matumizi ya simu janja.

Maelekezo hayo ameyatoa leo Juni 1, jijini Dodoma wakati akipokea taarifa ya tathmini ya hali ya mawasiliano pamoja na hatua mbalimbali zilizochukuliwa kufuatia malalamiko ya watumiaji wa huduma za kampuni ya simu ya Vodacom Tanzania.

“Kumekuwa na kero kwa wananchi kuingizwa kwenye huduma ambazo hawakuziomba, TCRA na makampuni ya simu kaeni mtafute utatuzi walikomeshe hili mara moja “, amesema Waziri Nape.

Ameongeza kuwa, “Kila mtoa huduma ya mawasiliano aende kwa wateja wake pamoja na wadau wanaowasaidia kutoa huduma kwa wananchi ili wasikilize malalamiko na kuyatatua, haiwezekani Serikali pekee ndio iwe inasikiliza na nyie makampuni ya simu mna wajibu wa kufanya hivyo”.

Waziri Nape ameilekeza TCRA na makampuni ya simu kukaa na kutatua malalamiko ya matumizi ya bando ambayo mtumiaji hajui limetumikaje ambapo ameelekeza makampuni ya simu kuboresha programu tumizi (mobile application) ili iwe rahisi kuisoma na itoe taarifa nyingi zaidi ili kupunguza malalamiko ya watu kutojua wametumiaje data zao

Katika hatua nyingine, Waziri huyo ameitaka TCRA na makampuni ya simu kuona namna ya kumsaidia kila mtanzania kumiliki na kutumia simu janja kwa kuangalia namna ya upatikanaji wa simu janja kwa bei nafuu na ikiwezekana ufanyike utaratibu wa mwananchi kununua simu kwa mfumo wa kulipia kwa awamu ndani ya mwaka mmoja au miwili ili kuongeza matumizi ya intaneti nchini

“Ikumbukwe kuwa Serikali iliondoa kodi kwenye simu janja lakini takwimu zinaonesha matumizi ya simu janja yameongezeka kwa asilimia mbili tu, kwa kuwezesha wananchi kutumia simu janja itaongeza watumiaji wa huduma ya intaneti, makampuni mtapata fedha Serikali itaongeza mapato na mwananchi atapata huduma anayostahili”, amezungumza Waziri huyo.

Aidha, Waziri Nape ameipongeza Kampuni ya Vodacom Tanzania kwa kuwa wa kwanza kwenda kufanyia kazi malalamiko ya wananchi na kuyashauri makampuni mengine kutekeleza hilo huku akiwashukuru wote waliowekeza katika sekta ya mawasiliano na kuwahakikishia kuwa Serikali inaendelea kushirikiana na sekta binafsi ili kumhudumia mtanzania

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Vodacom Tanzania, Sitholizwe Mdlalose Vodacom Tanzania amesema walifanya kazi kwa ushirikiano na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na kujenga minara ya mawasiliano 23 ili kupanua wigo wa mtandao wa simu kufikia asilimia 93 ya watu watanzania wanaopata huduma ya mawasiliano ya simu ikiwa pia ni sehemu ya kampeni ya kampuni hiyo ya kuiunganisha Afrika ambayo inatambua fursa za zinazotolewa na maunganisho ya kidijitali katika bara la Afrika 

Ameongeza kuwa Kampuni hiyo ya simu ilifanya ukaguzi wa kina kwenye huduma zao zote za kidijitali zinazotolewa na mawakala wasimamizi, na kugundua baadhi ya changamoto ambazo zimeshughulikiwa na tayari simu za malalamiko kutoka kwa wateja zimepungua kwa asilimia 30

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi