Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Nanauka amekutana na Waandishi wa Habari na kuweka bayana masuala muhimu yanayogusa vijana wa nchi ya Tanzania na kuahidi kuwafikia popote walipo ili kuweza kutatua na kusikiliza kero zao.
Amesema hayo leo Desemba 23, 2025 wakati akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam kuhusu mwelekeo wa Serikali katika kuwezesha vijana kiuchumi na kijamii ikiwa ni muendelezo wa mikutano ya Mawaziri iliyoandaliwa na Idara ya Habari - MAELEZO.

Ameongeza kuwa Serikali inawahakikishia vijana wote kuwa Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana iko wazi muda wote katika kuwahudumia vijana, kutoa huduma kwa kasi, viongozi wote kufikika kirahisi na kutumia teknolojia katika kuwasiliana na vijana.
"Sitosubiri Vijana wanifuate ofisini mimi na timu yangu tutawafuata vijana walipo." Amesema Mhe. Waziri Nanauka.
Vilevile, ametaja sehemu ambazo atazitumia kukutana na vijana ili kujadili masuala yao zikiwemo za shuleni, vyuoni, vijijini, mijini, sokoni, maeneo ya kazi pamoja na majukwaa ya kidijitali ili kuweza kutatua changamoto za vijana.

Pia, amezitaja baadhi changamoto zinazowakabili vijana ikiwemo ukosefu wa ajira, ajira zisizokuwa na tija, upungufu wa ujuzi na ukosefu wa mitaji na ameahidi kuzitatua changamoto hizo.
Mhe. Nanauka amesisitiza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha majukwaa ya kuwakutanisha vijana ikiwemo VIJANA Platform ambayo ni jukwaa la kusikiliza sauti za vijana, kujadili changamoto kuunganisha vijana na wadau. Jukwaa hilo linaenda sambamba na hatua za kisheria na kiutendaji kuelekea ukamilishwaji wa mfumo wa ushiriki wa vijana kitaifa ikiwemo taratibu za utekelezaji wa Baraza la Vijana.
Waziri Nanauka amesema kuwa wizara ina kauli mbiu inayowataka vijana kutumia utamaduni wa kuzungumza kwa kujadiliana ili kuleta mipango ya kimaendeleo inayosema, "Vijana Tuyajenge,Tanzania ni Yetu" ambapo ameeleza kuwa hayo si maneno matupu bali ni wito wa vitendo kwa kila kijana kutambua kuwa Taifa hilo ni lao na wana wajibu wa kulijenga.