Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Mwakyembe Apongeza TBC kwa Kuimarisha Usikivu Nyanda za Juu Kusini
Aug 14, 2020
Na Msemaji Mkuu

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt.Harrison Mwakymbe akizungumza na Wadau wa Habari mkoani Ruvuma alipofanya  mkutano na wadau hao ambapo amesisitiza ifikapo mwaka 2021 itakuwa mwisho kwa wanahabari wasiokua na vigezo vilivyoanishwa katika Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 mnamo Agosti 13,2020

Na Shamimu Nyaki – WHUSM, Songea

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe ametoa pongezi kwa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kwa kuimarisha usikivu wa redio TBC Taifa na TBC FM katika Mikoa ya Nyanda za juu Kusini.

Waziri Mwakyembe ametoa pongezi hizo Agosti 13,202 alipotembelea mitambo ya shirika hilo iliyopo Matogolo wilayani Songea mkoani Ruvuma ambapo amesema kuwa nyanda za juu kusini ni eneo ambalo lina miinuko na mabonde ambayo huleta changamoto ya usikivu kwa masafa ya FM changamoto hiyo imetatuliwa baada ya mitambo kuwekwa kwenye mwinuko mkubwa.

“Nawapongeza sana TBC kwa uwekezaji huu ambao mmeufanya katika eneo hili, umesaidia wananchi kupata habari kwa wakati kutoka katika chombo cha umma ambacho ndio kInaaminika katika utoaji wa habari sahihi”, alisema, Dkt. Mwakymbe.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo  Dkt.Harrison Mwakymbe akizungumza na Uongozi wa Mkoa wa Ruvuma pamoja na Mhandisi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania  (TBC) Bibi.  Upendo Mbelle (alievaa sweta) wakati Waziri huyo alipotembelea mitambo ya shirika hilo iliyopo Matogolo mkoani Ruvuma mnamo Agosti 13, 2020 ambapo amepongeza shirika hilo kwa kuimarisha usikivu katika Nyanda za juu kusini.

Dkt. Mwakymbe ameongeza kuwa suala la miundombinu katika maeneo iliposimikwa mitambo ni changamoto ambayo inatakiwa kutafutiwa ufumbuzi wa haraka ili kurahisisha huduma zinazotolewa katika maeneo hayo, hivyo suala hilo ataliwasilisha katika ngazi ya juu Serikalini.

Kwa upande wake Mhandisi Mkuu wa shirika hilo, Bibi.Upendo Mbelle  amesema kuwa, mtambo huo ni wa kilo wati moja (KW 1) ambao uwezo wake wa kurusha matangazo ni wa kiwango cha juu huku akieleza kuwa lengo la TBC ni kuhakikisha maeneo yote yenye changamoto ya usikivu  yanashughulikiwa ikwemo kununua vipuri na kufanya matengenezo kwa mitambo ambayo imechakaa.

“Mtambo huu ni miongoni mwa mitambo 60 iliyofungwa nchi zima ambayo inasaidia redio za shirika kusikika na katika eneo hili la Matogolo limesaidia maeneo ya Nyasa, Mbambabay, Tunduru   ambayo yalikua na usikivu hafifu kuimarika”, alisema Bibi.Upendo.

Katika hatua nyingine Waziri huyo amefanya mkutano  na Wadau wa Habari wa mkoa huo  ambapo amewataka kuzingatia weledi katika taaluma ya habari ikiwemo kuandika habari zenye ukweli, zilichokatwa vizuri  ambazo zitasaidia jamii kuelewa mambo mbalimbali ya nchi.

Dkt.Mwakyembe pia amesisitiza kuwa ifikapo mwaka 2021 hakuna Mwandishi wa Habari yoyote ambaye atakuwa hajakidhi vigezo vya Sheria ya Huduma ya Habari ya mwaka 2016 pamoja na kanuni zake za mwaka 2017, hataruhusiwa kufanya kazi ya uandishi wa habari.

“Mwanahabari ni mwalimu, mkalimani, mfasili, mchambuzi hivyo ni lazima aheshimike na kulindwa kama ajira zingine. Lakini pia mwanahabri anapaswa kutambua kuwa hakuna uhuru wa habari usiokuwa na mipaka” alisisitiza Dkt.Mwakyembe.

Vile vile Mhe Waziri amewataka viongozi kutoa habari kwa wananchi zinazoelezea utekelezaji katika maeneo hayo ili wananchi wafahamu serikali imeafanya nini,huku akisistiza matumizi ya Kitambulisho cha wanahabri popote wanapokuwa wanatimiza majuku yao.

Hata hivyo Waziri Mwakyembe alitembelea Makumbusho ya Majimaji Songea ambayo yana kumbukumbu ya mashujaa waliopigania uhuru kutoka kwa wajerumani katika vita ya Majimaji ya mwaka 1906 hadi 1907 ambapo amepongeza namna historia ilivyohifadhiwa katika eneo hilo ambalo ni kivutio cha utalii wa kiutamaduni pamoja na mali kale.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi