Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Mulamula: Washirika wa Maendeleo Msielekeze Miradi Upande Mmoja wa Nchi
Jul 26, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula ametoa wito kwa washirika wa maendeleo nchini kuelekeza miradi na programu zao katika sehemu mbalimbali za nchi kulingana na mahitaji ya walengwa na vipaumbele vya taifa.

Waziri Mulamula ametoa wito huo alipokuwa akifanya mazungumzo ya Balozi wa Austria nchini Tanzania, Mhe. Christian Fellner mwenye makazi yake jijini Nairobi, Kenya.  

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika katika Ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es Salaam, Waziri Mulamula ameeleza kuwa mara nyingi programu na miradi kutoka kwa washirikia wa maendeleo zinazolenga kuwawezesha wananchi katika shughuli za uzalishaji mali zimekuwa zikielekezwa upande mmoja wa nchi na kusahau maeneo mengine. 

Tanzania ni nchi kubwa na kila sehemu ya nchi ni muhimu na inamchango wake katika maendeleo ya Taifa letu kulingana na mazingira yanayowazunguka, hivyo ni vyema miradi na programu zinazoandaliwa na washirika wetu wa maendeleo zilenge kuwawezesha wananchi wa pande zote za nchi badala ya kuelekeza nguvu upande mmoja. Alipendekeza michango hiyo ielekezwe kupitia Serikali Kuu. Alisema Waziri Mulamula.

Sambamba na hayo, Waziri Mulamula amemshukuru Balozi Fellner kwa msaada wa vifaa tiba kutoka Serikali ya Austria wenye thamani ya Euro 50,000 uliokabidhiwa nchini jana tarehe 25 Julai 2022, na kupongeza mchango wa Serikali hiyo katika kuchangia maendeleo ya nchi kupitia programu mbalimbali wanazozifanya hapa nchini ikiwemo katika sekta ya afya, elimu, utalii, kilimo, usafirishaji na teknolojia. 

Vilevile Waziri Mulamula amemweleza Balozi Fellner kuhusu utayari wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kuendelea kushirikiana na Austria na hasa katika kipindi hiki ambacho Tanzania inaendelea kufungua na kuongeza maeneo ya ushirikiano na Dunia. Aliongeza kusema kuwa bado kuna fursa ya kuongeza maeneo ushirikiano hasa katika biashara, uwekezaji na utalii baina ya Tanzania na Austria.

Kwa upande wake Balozi wa Austria nchini, Mhe. Christian Fellner ameeleza kuwa Austria itaendelea kushirikiana na Tanzania sambamba na kuongeza nguvu zaidi katika kusaidia sekta ya elimu, ikiwemo kuanzisha na kuendesha programu za kuwajengea uwezo Wanafunzi na Taasisi za Elimu wa kufanya utafiti wa masuala mbalimbali kwa maendeleo ya nchi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi