Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema suala la uhifadhi wa mazingira liwe ajenda ya Kitaifa na jukumu la kila mmoja kuanzia ngazi ya familia mpaka Taifa.
“Na tunapokwenda kuhifadhi mazingira lazima tuanze na ngazi ya familia na tunapopanda juu tupanue wigo hadi kwa wadau mbalimbali. Viongozi wa dini mnayo nafasi kubwa na hii lazima iwe ajenda maalum, iwe ni ofisi za umma, za binafsi au kwenye taasisi.”
Ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Septemba 10, 2024) wakati akifunga mkutano maalum wa viongozi na wadau wa mazingira ulioitishwa ili kujadili mwenendo wa mazingira nchini. Mkutano huo ulifanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.
Amesema kitendo hicho kitakuwa ni kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuendelea kuimarisha uhifadhi na usimamizi wa mazingira nchini, kazi aliyoifanya kwa weledi, ustadi na mafanikio tangu akiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Amemudu kusimamia na kutoa miongozo mahsusi ya kuhakikisha mazingira yanahifadhiwa. Leo hii, yeye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na tunamuona anaendelea kulisimamia ili Taifa lifanikiwe katika uhifadhi wa mazingira kwa vizazi vya sasa na baadaye,” amesema.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwaeleza wajumbe wa mkutano huo juu ya jitihada ambazo Rais Dkt. Samia amekuwa akizichukua ili kuhakikisha suala la nishati safi linakubalika.
"Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuja na dhana mpya ya kukataa kukata miti na kutuhamasisha kuhusu nishati safi ya kupikia. Rais wetu amekuwa kinara wa nishati safi hadi na mwezi Mei alienda Ufaransa kuhutubia kuhusu nishati safi na yeye akiwa ni Mwenyekiti mwenza wa mkutano huo. Hii ni fahari kwa nchi yetu," amesema.
Amesema Serikali imetoa fursa kwa wajasiriamali kuanzisha biashara ya kuuza mitungi na majiko ya gesi hadi kwenye ngazi ya vijiji ili nishati hiyo iweze kupatikana kwa urahisi. “Huko mbele tutaweka ukomo wa matumizi ya mkaa na kuni,” ameongeza.
Katika kukabiliana na changamoto za uchafuzi wa mazingira, Waziri Mkuu amesema Serikali imechukua hatua za kisera na kimkakati ili kuleta matokeo chanya. Amezitaja hatua hizo kuwa ni kuandaliwa kwa Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021; Kutungwa kwa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2014; kuandaa na kutekeleza Mpango Kabambe wa Taifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira wa mwaka 2022 hadi 2032; kuandaa na kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi wa mwaka 2021 hadi 2026; na kutungwa kwa Kanuni na Miongozo inayohusu masuala ya Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu ameitaka wizara inayosimamia mazingira ishirikiane kwa karibu na wizara za kisekta kuhakikisha maadhimisho mbalimbali ya Kitaifa yanayogusa masuala ya mazingira yanatumika kikamilifu kuwezesha jamii kupata uelewa na kuweka alama za kudumu na matokeo yanayopimika kuhusu utunzaji mazingira ikiwemo Siku ya Upandaji Miti, Siku ya Hali ya Hewa, Siku ya Maji, Siku ya ardhi Oevu, Siku ya Mazingira na Siku ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni.
Kuhusu kuimarisha utoaji wa elimu na uhamasishaji kuhusu utunzaji wa mazingira, Waziri Mkuu amezitaka Ofisi za Mikoa na Wilaya zisimamie suala hilo na kusisitiza kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria na kanuni za mazingira na ikibidi watumie mitandao ya kijamii kusambaza elimu hiyo.
"Kuongezeka kwa ufahamu miongoni mwa jamii kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mazingira kutasaidia kupunguza uharibifu na kuimarisha usimamizi wa mazingira. Aidha, elimu ijumuishe matumizi endelevu ya rasilimali za mazingira ikiwemo matumizi bora ya ardhi, maji na nishati ili kuhakikisha kuwa rasilimali hizi zinabaki kuwa za kudumu kwa vizazi vijavyo," amesisitiza.
Mapema, Waziri wa Nchi (OMR - Muungano na Mazingira), Dkt. Ashatu Kijaji alisema mkutano huo maalum ulihudhuriwa na washiriki 2,500 kutoka maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Zanzibar. "Ninauita huu ni mkutano mkuu maalum kwa sababu umehusisha makundi tofauti ya kijamii wakiwemo viongozi wa dini, wa kisiasa, wa kimila, wanafunzi, wabunge na wadau wengine."
Alisema ofisi yake itafuatulia ukamilishajinwa rasimu ya Azimio la Dodoma hadi liwe Azimio kamili kwani linahitaji kufuata utaratibu wa Serikali hadi lije kuzinduliwa rasmi.
Azimio la Dodoma liliwasilishwa mbele ya wajumbe wa mkutano huo na Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu, Balozi Dkt. Bashiru Kakuru. Baadhi ya maeneo yaliyotajwa ni usimamizi na mapitio ya sera na sheria hasa za misitu na uhifadhi; uwajibikaji na ushirikishwaji wa umma kupitia ugatuzi wa madaraka; usimamizi wa taka ngumu na usafi wa mazingira; upandaji wa miti, mabadiliko ya tabianchi na biashara ya kaboni; utoaji wa elimu kuhusu nishati safi; uchumi wa bluu, rasilmali fedha na elimu kwa umma kuhusu mazingira.