Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema ndani ya mwaka mmoja, serikali imefanikiwa kusajili miradi 9,678 yenye thamani ya dola za Marekani milioni 8,658 hali ambayo inaonesha matokeo chanya ya uwekezaji nchini.
“Miradi 9,678 yenye thamani ya dola za Marekani milioni 8,658 ilisajiliwa mwaka 2023 ikilinganishwa na miradi 8,401 yenye thamani ya dola za Marekani milioni 5,558.47 iliyosajiliwa mwaka 2022,” amesema.
Alitoa kauli hiyo jana usiku (Jumatano, Septemba 11, 2024) wakati akizungumza na wadau mbalimbali walioshiriki hafla ya uzinduzi wa Taarifa Tano za Maboresho ya Mazingira ya Biashara na Uwekezaji na Nyenzo za Usimamizi wa Uwekezaji nchini iliyofanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Akifafanua kuhusu taarifa ya kwanza ya uwekezaji ya mwaka 2023 ambayo inaonesha takwimu za matokeo chanya ya uwekezaji nchini, Waziri Mkuu alisema miradi hiyo imeweza kuzalisha ajira za moja kwa moja 195,803 ikilinganishwa na ajira 76,841 zilizozalishwa mwaka 2022.
Akielezea juhudi zilizofanywa na Serikali kwenye mipango ya maendeleo ya uwekezaji wa sekta ya umma na sekta binafsi, pamoja na mazingira ya biashara, Waziri Mkuu alisema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kufanya mageuzi ya uendeshaji na usimamizi wa Taasisi na Mashirika ya Umma ili kuhakikisha kwamba yanaendeshwa kwa ufanisi na tija katika kuwahudumia wananchi.
“Suala hili tayari limetolewa maelekezo na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 28 Agosti, 2024 katika kikao kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Mashirika ya Umma na Taasisi za Serikali. Hivi sasa, Serikali imeridhia mapendekezo ya kutungwa kwa Sheria ya Uwekezaji wa Umma itakayoimarisha na kuweka masharti bora ya usimamizi wa uwekezaji katika Mashirika ya Umma pamoja na kuwa na vyanzo vya uhakika vya fedha kwa ajili ya uwekezaji.”
Alisema Serikali imeendelea kuimarisha matumizi ya mifumo ya TEHAMA ikiwemo Ujenzi wa Mfumo wa Kielektroniki wa Kuhudumia Wawekezaji unaoitwa Tanzania Electronic Investment Window (TeIW) ili kumwezesha mwekezaji kusajili mradi ndani au nje ya nchi na kupata vibali vya uwekezaji ndani ya siku tatu iwapo ametimiza vigezo.
“Awamu kwanza ya ujenzi wa mfumo huu imekamilika na imewezesha kuunganishwa kwa mifumo ya taasisi saba ambazo ni Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA); Idara ya Uhamiaji; Idara ya Kazi; Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA); Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA); Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC),” alisema.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amezitaka taasisi na mamlaka za Serikali ziharakishe marekebisho ya sheria ambazo zinachangia urahisi wa kufanya biashara ili kuhakikisha kwamba sheria mpya zinawezesha mazingira bora ya biashara na uwekezaji.
“Suala hili liende sambamba na kuweka vipaumbele katika kutoa huduma kwa haraka, kwa ufanisi na kwa kukidhi viwango vya kimataifa. Mamlaka zinapaswa kuwa na mifumo rahisi ya kuwasiliana na wawekezaji na kuondoa vikwazo vilivyopo,” amesisitiza.
Alizitaka taasisi na mamlaka za Serikali ziongeze ushirikiano wa karibu na sekta binafsi kwani inaweza kutoa mawazo na mapendekezo yenye thamani kuhusu maboresho yanayohitajika. “Pia, wekeni mipango ya kutoa mafunzo na huduma kwa wadau wa biashara ikiwa ni pamoja na uhamasishaji wa matumizi ya nyenzo mpya za usimamizi wa uwekezaji.”
Aliwataka wahakikishe jamii inashirikishwa katika michakato ya uboreshaji ili kupokea maoni yao na kwamba maamuzi yanayochukuliwa yanawiana na mahitaji yao. “Taasisi zote zinazohusika na mazingira ya biashara, zinapaswa kuwekeza katika mifumo ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) ili kuboresha usimamizi wa uwekezaji, kupunguza urasimu na kuongeza uwazi,” alisisitiza Waziri Mkuu.
Ili kupima ufanisi wa maboresho yaliyofanyika na kubaini maeneo yanayohitaji marekebisho, Waziri Mkuu aliwataka washirikiane na wadau kuweka mifumo ya tathmini ya mara kwa mara. “Wekeni mkazo kwenye umuhimu wa kubadilisha mikakati na mbinu kulingana na tathmini za utekelezaji na maoni kutoka kwa wadau,” alisema.
Taarifa tano zilizozinduliwa jana ni pamoja na Taarifa ya Tathmini ya Utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji; Taarifa ya Taifa ya Uwekezaji kwa Mwaka 2023; Mwongozo wa Kitaifa wa Uendelezaji na Usimamizi wa Maeneo Maalum ya Kiuchumi (SEZ); Mfumo wa Kielektroniki wa Kuhudumia Wawekezaji Kwenye Maeneo Maalum ya Kiuchumi na Mauzo ya Nje (EPZ); na Mpango Mkakati wa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kwa kipindi cha 2024/2025 - 2025/2026.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa hafla hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo alisema kupitia Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (MKUMBI) maboresho ya kisera ya mazingira ya biashara na uwekezaji yamefanyika ikiwemo kufutwa kwa tozo na kodi zaidi ya 374 zilizobainishwa kuwa ni kero katika sekta za uwekezaji, viwanda, biashara, madini, kilimo, mifugo, uvuvi, maliasili na misitu.