Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Mkuu Ataka Watumishi na Madiwani Kushirikiana
Jan 20, 2018
Na Msemaji Mkuu

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na watumishi wa umma, madiwani na wakuu wa Taasisi kwenye ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Bunda  (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa amewataka watumishi wa Halmashauri na Mji wa Bunda pamoja na Madiwani washirikiane katika utekelezaji wa ujenzi wa miradi ya maendeleo.

Pia amewaagiza watumishi wa umma katika halmashauri ya wilaya na mji wa Bunda wafanye kazi kwa bidii na wawahudumie wananchi bila ya ubaguzi wa aina yoyote.

Waziri Mkuu aliyasema hayo jana wakati akizungumza na watumishi na Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya na wa Halmashauri Mji wa Bunda, katika ukumbi wa Halmashauri ya Bunda.

“Watumishi wa umma  acheni kukaa sana maofisini tengeni muda wa kuwatembelea wananchi katika maeneo yao na shirikianneni nao katika kutatua kero zinazowakabili. Madiwani na watumishi lazima mshirikiane ili kuwaletea wananchi maendeleo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa Saba Saba katika mji mdogo wa Bunda (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Alisema watumishi na madiwani wakishirikiana katika usimamizi wa utekelezaji wa miradi mbalimbali  ya maendeleo, wilaya itafanikiwa katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Pia Waziri Mkuu aliwasisitiza watumishi hao kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na taratibu za utumishi  na wajiepushe na vitendo vya rushwa, wizi , ufisadi na uzembe kwa sababu vinarudisha nyuma maendeleo ya wananchi.

Baadhi ya wananchi wa mji mdogo wa Bunda wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipohutubia mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa Saba Saba katika mji mdogo wa Bunda Januari (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Awali, Waziri Mkuu alikagua mradi wa maji wa Bunda na baadae alizindua kikundi cha Ushirika cha Igembe Sabo na kukagua skimu ya umwagiliaji wa zao la mpunga ya Nyatwali wilayani Bunda.

Waziri Mkuu alihitimisha ziara yake wilayani humo kwa kuhutubia mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Stendi Mpya katika mji mdogo wa Bunda.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU

JUMAMOSI, JANUARI 20, 2018.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi