*Ni katika jopo la wafanyabiashara mahiri wa Marekani
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa sababu 10 zinazoweza kumfanya mfanyabiashara yeyote kutoka Marekani avutiwe kuwekeza nchini.
Amezitaja sababu hizo kuwa ni mahusiano imara, sera thabiti za kiuchumi, mazingira ya amani na uthabiti, nafasi ya kijiografia ya nchi, uwepo wa masoko makubwa, uwepo wa nguvu kazi ya vijana na miundombinu ya kidijitali. Nyingine ni miundombinu ya kisasa ya mawasiliano, uchumi mpana na utawala bora na mfumo wa kodi wa haki.
Akifungua jukwaa la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Marekani lililofanyika jana (Septemba 26, 2024) katika makao makuu ya ofisi za CITI, jijini New York, Marekani, Waziri Mkuu aliwaeleza wafanyabiashara hao kwamba Tanzania ni mahali sahihi pa kuwekeza mitaji yao na pana mvuto ambao hakuna mwekezaji anaweza kuukwepa.
Akielezea kuhusu uimara wa mahusiano, Waziri Mkuu alisema uhusiano wa muda mrefu baina ya nchi hizo mbili ambao umedumu kwa zaidi ya nusu karne, unathibitisha mazingira rafiki kwa uwekezaji.
Kuhusu sera thabiti za kiuchumi, Waziri Mkuu alisema kwa zaidi ya miongo miwili wastani wa ukuaji wa uchumi ulikuwa asilimia 7 na mfumuko wa bei wa chini ulikuwa wastani wa asilimia 3.8 hadi kufikia Desemba, 2023. “IMF inakadiria kuwa kwa kiwango hiki cha ukuaji, Tanzania itakuwa na uchumi mkubwa zaidi Afrika Mashariki ifikapo mwaka 2028.”
Kuhusu suala la amani, alisema mazingira ya biashara ya Tanzania ni ya kutabirika, ya uwazi na yenye ulinzi dhidi ya kutaifisha mali, huku wawekezaji wakiruhusiwa kurudisha faida zao baada ya kulipa kodi. “Tanzania iko kwenye eneo la kistratejia kutokana na nafasi yake ya kijiografia. Inapakana na nchi nane, jambo ambalo linatoa fursa bora za biashara na kuwa kitovu cha biashara cha kikanda,” alisisitiza.
Kwenye upatikanaji wa masoko makubwa, Waziri Mkuu alisema Tanzania inafikia soko la ndani lenye zaidi ya watu milioni 62, na zaidi ya watu milioni 500 kupitia jumuiya za kikanda kama vile SADC na EAC. Kuhusu nguvu kazi ya vijana, alisema Tanzania ina idadi kubwa ya vijana, ikitoa nguvu kazi ya kutosha inayoungwa mkono na uwekezaji katika elimu.
Akifafanua kuhusu miundombinu ya kidijitali, alisema Serikali inafanya uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya kidijitali, jambo linaloifanya nchi kuvutia wawekezaji wa teknolojia. Kuhusu miundombinu ya kisasa ya mawasiliano, Waziri Mkuu alisema Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR), maboresho ya Shirika la Ndege la Tanzania (Air Tanzania) na uwekezaji katika usafiri wa maji ni hatua zinazolenga kuimarisha biashara na usafirishaji nchini.
Akiwaelezea kukua kwa uchumi, Waziri Mkuu alisema Tanzania ina sekta mbalimbali zikiwemo kilimo, madini, utalii, viwanda na utoaji wa huduma ambazo zote zinachangia ukuaji wa uchumi. Kuhusu utawala bora na mfumo wa kodi wa haki, alisema mabadiliko ya hivi karibuni yameboresha taratibu za kodi na kupunguza mizigo ya kodi kwa wawekezaji, huku nchi ikijitolea kwa uwazi na haki katika utawala.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alisema kupitia Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA), makampuni ya kimarekani yamewekeza kwenye taasisi tano ambazo ni Tanchoice, Kibidula Farm Limited, Africado Limited, Kokoa Kamili Limited na Next Gen Solawazi Limited ambapo uwekezaji wao kwa pamoja unafikia dola za Marekani milioni 31.51 na umesaidia kuzalisha ajira 866.
“Makampuni haya yanauza bidhaa nje ya nchi zenye thamani ya dola za Marekani milioni 28.6 na hasa Amerika Kaskazini, Ulaya, Masharki ya Kati na Afrika Kusini. Makampuni haya yamewekeza kwenye usindikaji wa nyama, mazao ya parachichi na kakao pamoja na kufua umeme wa jua.”
Akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na wafanyabiashara hao, Waziri wa Nchi (OR-Mipango na Uwekezaji), Prof. Kitila Mkumbo alisema Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya kuvutia wawekezaji na kuimarisha mahusiano ya kiuchumi na washirika wa maendeleo kote duniani ikiwemo Marekani.
“Rais Dkt. Samia anawaona wawekezaji na viongozi kwenye sekta ya biashara siyo tu wawekezaji muhimu lakini pia sehemu muhimu ya kuvutia wawekezaji wengine duniani.”