Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa leo Februari 29, 2024 amekagua maendeleo ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa Musoma ambapo amesema ni faraja kuona Serikali ikiendelea kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali ya kimkakati ukiwemo uwanja wa ndege wa Musoma.
Amesema kuwa maamuzi ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuidhinisha fedha kwa ajili ya upanuzi wa uwanja huo ni ya kuungwa mkono kwani ni fursa kwa wafanyabiashara na wakazi wa maeneo hayo.
“Uwanja huu utaleta fursa kwa wafanyabiashara na wakazi wa mkoa huu na wilaya zake, kwa sababu itawezesha kuendelea kukua kwa sekta ya utalii kwenye mkoa huu ambao Hifadhi ya Serengeti ndiyo asili yake.”
Amesema kuwa ujenzi wa uwanja huo kama ilivyo kwa ujenzi wa viwanja vingine duniani, viwango na umakini utazingatiwa. “Kwa kuwa TANROADS ndiyo mnasimamia hili, sisi hatuna shaka, tunaamini kazi hii inaendelea, awamu za ulipaji wa fedha hizo hazina shaka, mkandarasi atalipwa ili akamilishe kazi hii kwa wakati.”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amewataka Wana-Mara watumie fursa ya ukarabati wa uwanja huo kwa kufanya uwekezaji mkubwa ikiwemo ujenzi wa hoteli ili kuwe na maeneo ya kutolea huduma. “Jengeni hoteli za kisasa kuanzia nyota tano, nne na kuendelea, wekeni biashara za kuvutia watalii, msisubiri ukarabati wa uwanja huu uishe ndipo muanze kujenga. Mtakuwa mmechelewa.”
Kadhalika Mheshimiwa Majaliwa amewataka walioajiriwa katika mradi huo kufanya kazi hiyo kwa weledi ili ujenzi uwe wa viwango. “Nimeambiwa zaidi ya asilimia 80 walioajiriwa hapa ni Watanzania, ninyi ni wasaidizi wa kusimamia viwango, wakati wote hakikisheni suala la viwango vinavyosisitizwa na Mainjinia linapewa kipaumbele”
Mapema, akitoa taarifa ya ukarabati na ujenzi wa uwanja huo kwa Waziri Mkuu, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mara, Mhandisi Vedastus Maribe alisema mradi huo umefikia asilimia 55 na utagharimu shilingi bilioni 35 hadi kukamilika kwake.
Alisema kazi zilizopangwa kufanyika zinahusisha ukarabati wa njia ya kuruka na kutua ndege (runway) yenye urefu wa mita 1,705 na upana mita 30 kwa kiwango cha lami, ukarabati wa njia ya kiungio (taxiway) kwa kiwango cha lami, ukarabati wa eneo la maegesho ya ndege (Apron) kwa kiwango cha lami, mifereji na uzio.`
Alisema katika awamu ya kwanza, shilingi bilioni 4.1 zimetumika kulipa fidia ya mali na ardhi kwa wananchi 85 na awamu ya pili ya shilingi bilioni 3.9 zimeshaombwa ili kuwalipa wananchi 49 ambao walikuwa hawajalipwa katika awamu ya kwanza.
Waziri Mkuu anaendelea na ziara yake katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma ambako atakutana na madiwani na watumishi na kuzungumza na wananchi. Pia atazungumza na wananchi katika Manispaa ya Musoma.