Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Mkuu Aitaka Utalii Kuongeza Mbinu Kuvutia Watalii
Aug 24, 2017
Na Msemaji Mkuu

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kutafuta mbinu bora za kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini ili kukuza sekta hiyo.

 Amesema licha ya Tanzania kuwa na vivutio vingi vya utalii lakini idadi ya watalii wanaoingia nchini kwa mwaka ni ndogo, hivyo kuna haja ya kuboresha matangazo.

 Waziri Mkuu aliyasema hayo jana (Jumatano, Agosti 23, 2017) wakati alipofanya ziara katika mji wa kitalii wa Varadero ulioko kwenye mkoa wa Matanzas nchini Cuba.

 Alisema mji wa Varadero tu unaingiza watalii zaidi ya milioni moja kwa mwaka na unategemea kivutio kikubwa kimoja tu cha fukwe ambayo ina urefu wa kilomita 22.

 Alisema idadi  hiyo ni tofauti na Tanzania ambayo imejaliiwa kuwa na vivutio vingi vya utalii huku watalii wanaovitembelea ni wachache. “Tunatakiwa kujitangaza zaidi.”

 Waziri Mkuu alitaja baadhi ya vivutio vya utalii ambavyo ni mlima Kilimanjaro, mbuga za wanyama, miji ya kihistoria ya Kilwa, Bagamoyo, Stone Town pamoja na Mikindani.

 “Vivutio vingine ni eneo la Oldvai George ambako binadamu wa kwanza aliwahi kuishi, hifadhi ya Gombe ambako kuna sokwe ambao wanaishi kama binadamu.”

 Alisema Serikali itahakikisha jitihada zinafanyika katika kukuza sekta ya utalii ikiwa ni pamoja na kutangaza vivutio vilivyoko nchini ili kuweza kuongeza idadi ya watalii.

 Pia Waziri Mkuu aliwahamasisha Watanzania kujenga tabia ya kutembelea vivutio vyeo vya utalii na kujifunza mambo mbalimbali na si kuwaachia wageni pekee.

 Kwa upande wake, Kiongozi wa Sekta ya Utalii katika mkoa wa Matanzas, Bw.  Luis Martinez de Armas alisema mji wa Varadero ni kivutio kikubwa cha utalii nchini Cuba.

 Alisema kivutio kingine cha utalii ni hoteli zilizojengwa ndani ya bahari, maeneo ya kihistoria na migahawa inayouza vyakula vya asili vya nchi hiyo.

 Bw. Luis alisema mwaka 1990 ndio walianza kuendeleza sekta ya utalii katika mkoa wao na ulikuwa na hoteli 4,436 ambazo kwa sasa zimeongeza na kufikia hoteli 20,696.

 Hata hivyo Bw. Luis alisema Tanzania inavivutio vingi vya utalii na kwamba anavutiwa na mlima Kilimanjaro pamoja na wanyama na viumbe vingine vilivyoko katika mbuga mbalimbali. Alisema wako tayari kushirikiana na Serikali katika kukuza sekta ya utalii.

  IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU, 

ALHAMISI, AGOSTI 24, 2017.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi