Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Mkuu Aitaka NHC Kujenga Nyumba Katika Maeneo Mapya ya Utawala
Jul 21, 2017
Na Msemaji Mkuu

[caption id="" align="aligncenter" width="750"] Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiweka jiwe la Msingi la ujenzi wa nyumba 20 za watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Momba katika eneo la Chitete akiwa katika ziara ya mkoa wa Songwe Julai 21, 2017. Wapili kulia ni mkewe Mary na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Chiku Galawa. Kulia kwa Waziri Mkuu ni Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) linalojenga nyumba hizo, Blandina Nyoni.[/caption]  

[caption id="" align="aligncenter" width="750"] Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Mwanachuo wa Chuo cha DIT, Gloria Shoo kuhusu Mradi wa Ujenzi wa Nyumba za watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Momba zinazojengwa na Shirika la Taifa la Nyumba katika eneo la Chitete wilayani Momba Julai 21, 2017. Gloria anafanya kazi kwa muda akijifunza katika shirika hilo. Kushoto kwake ni mkewe Mary na wapili kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Nyumba la Taifa, NHC, Blandina Nyoni.[/caption] (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Na Mwandishi wetu

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameliagiza Shirika la nyumba Nchini kwenda kujenga nyumba bora za makazi katika maeneo yote mapya ya utawala ikiwemo mikoa na wilaya ili kusaidia kutatua changamoto ya makazi kwa watumishi.

Pia ameweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa nyumba 20 za watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Momba mkoani Songwe zinazojengwa katika kijiji cha Tindingoma, unaojengwa na Shirika la Nyumba Nchini.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, Julai 21, 2017) wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha Naming’ongo wilaya ya Momba akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Songwe.

“Nalipongeza Shirika la Nyumba kwa mikakati waliyonayo ndani ya shirika hilo na kwamba waendelee na utekelezaji wa mipango hiyo ya ujenzi wa nyumba ili maeneo yote mapya ya utawala yaweze kuwa na makazi bora ya kuishi watumishi.”

Pia aliwataka wakazi wa kata ya Chitete yaliko makao makuu ya wilaya ya Momba  kuhakikisha wanachangamkia fursa ya uwepo wa makao makuu wa wilaya kwenye kata yao kwa kujenga nyumba za kisasa kwa ajili ya kupangisha watumishi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Bw. Nehemia Mchechu amesema mradi huo wenye thamani ya sh bilioni 2.2 ulianza kujengwa Machi 2016 na unatarajiwa kukamilika Septemba mwaka huu.

Amesema mradi huo ulibuniwa baada kupokea maombi kutoka Halmashauri ya wilaya ya Momba na kwamba unatekelezwa kwa awamu mbili ya kwanza ni ujenzi nyumba nane na tayari zimekamilika.

Ameongeza kwamba ujenzi wa awamu ya pili unajumuisha nyumba tisa ambapo gharama ya ujenzi wa nyumba itatumika kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya ofisi za Halmashauri hiyo.

Naye Mwenyekiti wa bodi ya NHC , Bi. Blandina Nyoni amesema shirika hilo lilianzisha mpango wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu katika maeneo mbalimbali nchini ili kuwawezesha wananchi kuwa na makazi bora.

Amesema katika miradi 54 ya ujenzi wa nyumba inayotekelezwa na shirika hilo katika maeneo mbalimbali nchini kati yake miradi 24 imekamilika ikiwemo 14 ya nyumba za gharama nafuu.

Pia Mbunge wa jimbo la Momba (CHADEMA) Mheshimiwa David Silinde amesema anashukuru Serikali kwa ujenzi wa nyumba hizo na kumueleza Waziri Mkuu kwamba wananchi wa Momba wanaridhishwa na utendaji wa Serikali na kwamba maendeleo hayana chama.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

IJUMAA, JULAI 21, 2017

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi