Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Mhandisi Kamwelwe Atoa Miezi Mitatu kwa TEMESA
Jul 16, 2019
Na Msemaji Mkuu

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, ametoa miezi mitatu kwa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kutopeleka magari ya Serikali kwenye karakana binafsi kwani Wakala unajitosheleza kwa kuwa na wataalamu  na vifaa vya kutosha.

Mhandisi Kamwelwe, amesisitiza kwa Wakala huo kuhakikisha unatengeneza magari kwa bei nafuu na muda na mfupi ili kupunguza malalamiko kutoka kwa wateja wao.

Waziri Mhandisi Kamwelwe ametoa agizo hilo jijini Dar es Salaam katika kikao kazi na uongozi pamoja na wafanyakazi wa Wakala huo ambapo pamoja na mambo mengine alikagua vitendea kazi vya kisasa vilivyofungwa katika karakana ya MT. Depot iliyopo jijini hapo.

"Ninyi ni taasisi ya Serikali fanyeni vitu viwe nafuu na mtengeneze kwa viwango ili watu wafurahie huduma zenu", amesisitiza Waziri Mhandisi Kamwelwe.

Aidha,  ametoa wito kwa Wakala huo kutoa ushauri wa magari ya Serikali kwa umahiri na weledi na kutokubali kutengeneza magari ya Serikali endapo gari hilo litaonekana gharama yake  ni sawa na kununua gari nyingine.

Waziri Kamwelwe ameupongeza Wakala huo kwa kupunguza gharama za kutengeneza taa za barabarani ambazo zinatumia mfumo wa dakika.

"Wakala umetumia kiasi cha shilingi milioni 150 katika kitengeneza taa hizo badala ya milioni 250 na tayari zimeanza kufungwa katika mikoa mbalimbali ikiwemo mkoa wa Morogoro" amesema Waziri Kamwelwe.

katika bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2019/20 Waziri Kamwelwe amefafanua kuwa Serikali imetenga kiasi cha Shilingi milioni 800 kwa ajili ya kununua boti za uokoaji kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi kwa urahisi katika visiwa vya Ukerewe (Ilugwa, Nafuba na Gana).

Awali akitoa taarifa ya utendaji kazi wa TEMESA kwa Waziri huyo, Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Mhandisi Japhet Masele, amemueleza kuwa Wakala umejipanga kipindi cha mwaka wa fedha 2019/20 kuanzisha karakana katika ngazi za Wilaya ikiwemo Wilaya ya Kahama, Simanjiro, Same, na Chato lengo likiwa ni kupeleka huduma karibu na wateja hasa kwa walio mbali na karakana za mikoa.

Ameendelea kueleza kuwa hadi sasa Wakala umeshafanya uwekezaji wa shilingi bilioni 66 kwa ajili ya kununua vivuko 18 na hivyo kufanya kufikia jumla ya vivuko 31 na boti ndogo tano hapa nchini.

Kuhusu kukamilisha ujenzi wa vivuko  nchini Mhandisi Masele amesema kuwa tayari wakala umekamilisha ujenzi wa kivuko kipya cha MV Mwanza kinachotoa huduma eneo la kigongo-Busisi, ujenzi wa miundombinu katika kivuko cha Lindi Kitunda na inaendelea kukamilisha ujenzi wa Kivuko cha Kayenze- Bezi kitakachotoa huduma kati ya Kayenze na kisiwa cha Bezi mkoani Mwanza.

Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) ulianzishwa chini ya sheria ya Wakala Na.30 ya mwaka 1997 ikiwa na majukumu ya kufanya matengenezo ya magari na mitambo ya Serikali, matengenezo ya usimikaji wa mifumo ya umeme, uendeshaji wa vivuko vya Serikali, utoaji huduma za ukodishaji wa mitambo ya Serikali, kufanya usanifu na usimamizi wa usimikaji wa mifumo ya uhandisi wa mitambo, umeme na elektroniki.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi