Wajumbe Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira wamefanya ziara ya kutembelea Mradi wa Hifadhi Endelevu ya Ardhi katika Bonde la ziwa Nyasa (SLM-Nyasa) unaotekelezwa na ofisi ya Makamu wa Rais katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma Machi 16, 2024.
Wakiongozwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe. Jackson Kiswaga, wajumbe hao wamekagua moja ya boti za injini za uvuvi zilizotolewa kwa vikundi vya wavuvi katika ziwa Nyasa ili kuwawezesha kujipatia kipato pasipo kuharibu mazingira.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhe. Kiswaga amesema kamati imeridhishwa na mradi huo na kuishukuru Serikali kupitia ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuratibu mradi huo ambao umeleta manufaa kwa wananchi na hifadhi ya mazingira.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Khamis Hamza Khamis aliyeambatana na kamati hiyo ameendelea kuwahimiza wananchi kuitunza miradi hiyo.
Mradi wa SLM–Nyasa unalenga kuwajengea wananchi uwezo wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuboresha maisha yao kwa kuwapa njia mbadala ya kujipatia kipato na hivyo kuachana na ukataji wa miti hovyo na uvuvi usio endelevu.
Kupitia mradi huo, Halmashauri ya Nyasa imefanikiwa kupanda miti takriban 3,500 rafiki kwa vyanzo vya maji, kupunguza ukataji holela wa miti kwa kutoa elimu ya matumizi ya majiko banifu yanayotumia kuni chache.
Mradi huo unatekelezwa katika halmashauri za wilaya zingine za Mbinga (Ruvuma), Kyela (Mbeya), Ludewa na Makete (Njombe) ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Kuenea kwa Jangwa na Ukame.